'Walioshangilia marufuku ya mikutano, wameshangilia kuruhusiwa’
Muktasari:
- Mhariri wa Dawati la siasa la Mwananchi, asema zuio la kuondoa zuio la mikutano ya hadhara uliofanywa na Rais Samia Suluhu Hassan ni sahihi lakini umechelewa.
Dar es Salaam. Mhariri wa dawati la siasa wa gazeti la Mwananchi, Salehe Mohamed amesema uamuzi wa kuondoa zuio la mikutano ya hadhara uliofanywa na Rais Samia Suluhu Hassan ni sahihi lakini umechelewa.
Mohamed amesema hayo leo Jumatano Januari 4, 2023 katika mjadala wa ‘Twitter Space’ uliokuwa na mada ya ‘kuruhusiwa kwa mikutano ya hadhara na kuukwamua mchakato wa Katiba je ni mwelekeo mpya wa siasa nchini?
Jana, Januari 3, 2023, Rais Samia akizungumza na viongozi wa vyama vya siasa 19 vyenye usajili wa kudumu Ikulu Dar es Salaam, aliruhusu mikutano ya hadhara iiliyokuwa ikililiwa kwa muda mrefu na vyama vya upinzani kutaka ruhusiwe.
"Uwepo wangu leo (jana) hapa mahali nimekuja kufanya ruhusa ya mikutano hii, nimekuja kutangaza kuondoa zuio la kuzuia mikutano ya hadhara na ninasema kwamba, sasa linaondoka,” alisema.
Akichangia mjadala huo, Mohamed amesema licha ya uamuzi huo ni wakati kwa viongozi au kiongozi aliyeko madarakani kuheshimu sheria mbalimbali zinazoongoza Taifa.
“Akitokea kiongozi anakiuka sheria hizo sio jambo jema lakini alichokifanya Rais Samia ni jambo jema. Lakini tulitegemea uamuzi huu ungetolewa mapema maana kila mmoja wetu alijua sheria imekiukwa wakati wa zuio hili limewekwa mwaka 2016,” amesema
“Sikutarajia zuio likae muda mrefu, nilitarajia tu alipoingia madarakani kwa sababu Katiba au sheria imevunjwa uamuzi huu ungekuja mapema,” amesema Mohamed.
Amewataka Watanzania lazima kuwa tayari kuitetea Katiba, akisema hakuna mtu aliyepo juu ya Katiba.
Amesema watu wanashangalia uamuzi wa Rais Samia, lakini je kuna mikakati gani ya imewekwa kwamba asitokee kiongozi yoyote atakayevunja sheria.
“Jana nimeshaangaa kuna viongozi walikuwa wanashangilia uamuzi, lakini ndio hawa hawa walishangilia wakati zuio hili linawekwa. Sasa lazima tufike sehemu demokrasia ichukue nafasi,” amesema
Mohamed amesema mikutano ya kisiasa mbali na vyama kujiimarisha pia ni fursa ya kiuchumi katika kila sehemu inapofanyika.
Kuhusu Katiba Mpya, Mohemed amesema vuguvugu lake lilianza muda mrefu na mchakato huo ulipoanza kulikuwa na sintofahamu baina ya pande mbili hata hivyo, uamuzi wa Rais Samia umeonekana kuwa na dalili njema.
Jana, katika hotuba yake, Rais Samia alisema Serikali inadhamilia kuukwamua mchakato wa marekebisho ya Katiba Mpya kwa namna watakavyokubaliana kwa siku za usoni.
“Tupo tayari kuukwamua ili tuanze sasa kwa kamati kadhaa kufanya kazi kadhaa za kuangalia mambo kadhaa. Tumekuwa tukiumiza vichwa wengine wanasema tuanze na kamati ya Jaji Joseph Warioba na wengine Katiba pendekezwa ya Bunge Maalumu la Katiba.