Aliyekuwa rais wa Zambia, Edgar Lungu afariki dunia
Muktasari:
- Lungu aliiongoza Zambia kwa miaka sita kuanzia mwaka 2015 na kushindwa katika uchaguzi ambao wananchi walimchagua rais wa sasa, Hakainde Hichilema kwa kura nyingi.
Lusaka. Rais wa zamani wa Zambia, Edgar Lungu amefariki dunia akiwa na umri wa miaka 68, chama chake kimethibitisha.
Kwa mujibu wa taarifa iliyoripotiwa na shirika la habari la Uingereza (BBC), Lungu amefariki dunia wakati akipatiwa matibabu nchini Afrika Kusini.
“Amekuwa akipokea matibabu maalumu nchini Afrika Kusini” kwa ugonjwa ambao haujatajwa, chama cha Patriotic Front kimesema kikithibitisha habari hiyo.
Lungu aliiongoza Zambia kwa miaka sita kuanzia mwaka 2015 na kushindwa katika uchaguzi ambao wananchi walimchagua rais wa sasa, Hakainde Hichilema kwa kura nyingi.
Baada ya kushindwa katika uchaguzi huo, alijiondoa kwenye siasa lakini baadaye akarejea na kuonekana kuwa na nia ya kugombea tena urais.
Shirika la Habari la DW, pia, limemnukuu mtoto wake akisema Lungu alifariki leo Alhamisi Juni 5, 2025 asubuhi baada ya kupata matibabu maalumu katika kliniki moja jijini Pretoria, Afrika Kusini.
“Baba yangu alikuwa chini ya uangalizi wa kitabibu katika wiki za hivi karibuni,” binti yake, Tasila Lungu-Mwansa ametangaza kupitia video iliyosambazwa kwenye mitandao ya kijamii.
“Hali yake ilisimamiwa kwa heshima na faragha, kwa msaada kutoka kwa wote waliomuombea mema,” ameongeza bila kutoa maelezo zaidi.
Atakavyokumbukwa
Lungu alitambulika kwa kuboresha hadhi ya kimataifa ya Zambia, kuimarisha uhusiano wa kidiplomasia na nchi jirani pamoja na zile za mbali, hatua iliyosaidia kuinua taswira ya Zambia duniani.
“Sote ni mabalozi wa nchi yetu kwa namna yetu,” Lungu alisema wakati wa utawala wake, akisisitiza juu ya mshikamano wa kitaifa na uzalendo. “Haijalishi kama uko kwenye chama tawala au upinzani, una nchi moja tu unayoweza kuiita yako kwa fahari.”
Alijitahidi kuondoa utegemezi wa kiuchumi wa Zambia kwenye madini ya shaba, akihamasisha maendeleo ya miundombinu na kuboresha usalama wa binadamu.
Aidha, alimteua Makamu wa Rais wa Kwanza mwanamke nchini Zambia, Inonge Wina, na alianzisha mipango kama kupunguza hukumu za kifo na kuanzisha siku ya kitaifa ya maombi.
Utawala wa ukandamizaji
Urais wa Lungu ulikumbwa na changamoto kubwa za kiuchumi, zikiwemo mdororo wa uchumi na ongezeko la deni la taifa, sambamba na kuongezeka kwa mvutano wa kisiasa.
Serikali yake ilitumia mara kwa mara mamlaka ya dharura kudhibiti machafuko, kama ilivyoshuhudiwa wakati wa ghasia zilizochochewa na uvumi wa mauaji ya kishirikina uliosababisha mashambulizi ya chuki dhidi ya wageni. Wakosoaji wake walimlaumu kwa kukandamiza upinzani na kukiuka uhuru wa kujieleza, kukusanyika na wa vyombo vya habari.
Sheria kama ile ya Usalama Mtandaoni na Uhalifu wa Kimtandao (Cyber Security and Cyber Crimes Act) zilitungwa kwa haraka, na kusababisha hofu ya kukandamiza upinzani mtandaoni.
Vyombo vya habari vilivyokuwa vikiikosoa serikali vilifungiwa, huku wanaharakati wakikumbwa na vitisho na kukamatwa. Vyama vya upinzani na mashirika ya haki za binadamu vililaani matumizi ya sheria za kashfa kuwanyamazisha wakosoaji na kudhoofisha uhuru wa polisi.
Lungu alitetea matumizi ya mbinu hizo kali za kiusalama, akisema alitangaza hali ya hatari “kuleta utulivu” wakati wa misukosuko ya kijamii.
Endelea kufuatilia tovuti ya Mwananchi na mitandao yake ya kijamii kwa taarifa zaidi.