Atakayemrithi Chongolo CCM hadharani leo

Muktasari:

  • Shauku na kiu ya makada na wafuasi wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) kumfahamu Katibu Mkuu wao mpya itakatwa muda wowote kuanzia sasa, wakati huu ambao Rais Samia Suluhu Hassan anaongoza kikao cha kamati kuu mjini Unguja.


Dar es Salaam. Kamati Kuu ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) imekutana leo mjini Unguja, Zanzibar kujadili masuala mbalimbali zikiwemo ajenda zitakazowasilishwa baadaye leo Jumatatu Januari 15,2024 kwenye kikao cha Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC).

Hata hivyo, pamoja na mambo mengine kikao hicho kinatarajiwa kutoka na jina la Katibu Mkuu mpya wa CCM, atakayechukua mikoba ya Daniel Chongolo aliyejiuzulu wadhifa huo Novemba, mwaka jana.

Chongolo aliachia wadhifa huo kwa kile kilichodaiwa kuwa ni kuchafuliwa kwenye mitandao ya kijamii kwa tuhuma mbalimbali.

Mara baada ya kuwasilisha barua ya kujiuzulu, Rais Samia Suluhu Hassan aliwatangazia wajumbe wa NEC kwamba, Chongolo ameachia wadhifa huo na yeye ameridia ombi lake hilo.

Pamoja na kuridhia huko, Rais Samia ambaye pia ni Mwenyekiti wa CCM Taifa, aliagiza vyombo vya dola kuchunguza tuhuma hizo ili kubaini ukweli.

Hata hivyo, macho na masikio ya wanachama, wafuasi na makada wa CCM ni kwenye kikao hicho cha Kamati Kuu leo Jumatatu Januari 15, 2024, ni  kujua jina la mtendaji huyo mpya atakayeteuliwa kabla ya kuwasilishwa kwenye kikao cha NEC kwa ajili ya kuthibitishwa na wajumbe.

Kabla ya Chongolo kuandika barua ya kujiuzulu, kulikuwa na vuguvugu la muda mrefu ndani ya CCM kuhusu kiti chake hicho.

Taarifa za sirisiri kutoka kwa makada na kwenye mitandao ya kijamii zilikuwa zikidai kuwa, kuna mpango wa Chongolo kubadilishwa kwenye wadhifa huo.

Taarifa hizo zilichagizwa zaidi kila kunapokaribia vikao vya juu vya CCM ambapo, utabiri wa kwamba safari ya Chongolo imeiva zilikuwa zikisikika kila kona, lakini mwisho wa siku alibaki salama hadi alipoamua mwenyewe kuandika barua ya kujiuzulu.

Mwananchi limedokezwa kuwa moja ya sababu zilizokuwa zikitajwa na ambazo pia zinadaiwa kuchangia Chongolo kuachia ngazi ni makundi ya urais mwaka 2030 na wasaka madaraka ambapo, kila upande umekuwa ukipambana kuweka mtu wao.

Yapo makundi kadhaa yamekuwa yakihusishwa kuendesha siasa ndani ya CCM kutokana na mbio za urais mwaka 2030 huku 2025 ikitajwa kutokuwa na vurugu nyingi kwa sababu ya utamaduni wa rais kumaliza vipindi viwili vya uongozi.

Tayari, Makamu Mwenyekiti wa CCM (Bara), Abdulrahman Kinana na Waziri Mkuu Kassim Majaliwa kwa nyakati tofauti wamedai kuwa mwaka 2025 fomu itakayotolewa na CCM ni moja tu na itakabidhiwa kwa Rais Samia pekee.

Makada wanaotajwa tajwa

Mwananchi limedokezwa kuwa katika vuguvugu hilo kumekuwa na majina kadhaa ambayo yanachomoza kupigiwa chapuo kwenda kukalia kiti hicho akiwemo waziri wa zamani katika Serikali ya awamu ya nne, Balozi Emmanuel Nchimbi, wakuu wa mikoa, Amos Makalla (Mwanza) na Martin Shigella (Geita).

Kwa nyakati tofauti Makalla mbali ya kuwa mkuu wa mkoa, pia amepata kuwa Mweka Hazina wa CCM, naibu waziri katika wizara kadhaa na mbunge wa Mvomero.

Kwa upande wa Shigella amewahi kuwa Katibu Mkuu wa Umoja wa Vijana wa CCM (UVCCM) kabla ya kuteuliwa kuwa mkuu wa wilaya ya baadaye kupandishwa. Naye Balozi Nchimbi kabla ya kuwa na wadhifa huo wa kidiplomasia, amewahi kuwa Mwenyekiti wa UVCCM, Waziri katika wizara za Ulinzi, Mambo ya Ndani na Habari. Ni mwanasiasa mkongwe aliyeanzia harakati zake ndani ya umoja wa vijana, akitajwa kuwa na uzoefu mkubwa.

Mara ya mwisho alisimama mbele ya waandishi wa habari kwenye makao makuu ya CCM mjini Dodoma, akitangaza kujitenga na uamuzi wa Kamati Kuu ya chama hicho wakati wa uteuzi wa wagombea urais.

Pia, wamo washauri wa Rais (Siasa na Uhusiano wa Jamii), Abdallah Bulembo aliyewahi pia kuwa Mwenyekiti wa Jumuiya ya Wazazi. Bulembo ndiye alikuwa kampeni meneja wa Hayati John Magufuli wakati wa kampeni za kusaka urais mwaka 2015.  Pia, yumo William Lukuvi, ambaye pia ni mbunge wa Ismani na waziri mwandamizi mstaafu pamoja na Anthony Mtaka (mkuu wa mkoa Njombe) nalo limekuwa likichomoza.

Mzigo unaomsubiri Katibu mkuu mpya

Kwa hali ilivyo, mbali ya majukumu ya kikatiba, Mwananchi linatambua kuwa mtendaji ajaye, atakuwa na kibarua cha kukiuhisha chama kuelekea katika uchaguzi wa serikali za mitaa, kuratibu mchakato wa Ilani ya uchaguzi wa CCM ya mwaka 2025/30.

Majukumu mengine ni kudhibiti ukuaji wa makundi ndani ya chama hicho yanayopigana vikumbo kupanga safu za viongozi kuelekea katika chaguzi zijazo.

Pia, atakuwa na kibarua cha kuhakikisha anashindana kwa hoja na wapinzani waliobeba ajenda ya ugumu wa maisha, Katiba Mpya na maboresho ya miswada sheria ya uchaguzi na vyama vya siasa.

Baadhi ya wachambuzi wa siasa, walisema ingawa ajenda ya vikao hivyo havijawekwa wazi, huenda suala la kumpata katibu mkuu mpya likajadiliwa na kuthibitishwa.

“Kuna tangazo la CCM limeliona mtandaoni linasema wajumbe wote wa halmashauri kuu waende Zanzibar kuhudhuria mapinduzi, kisha kushiriki vikao vya chama, sasa unaposema kujenga chama si pamoja na kuwa na mtendaji mkuu wa chama?

“Kutokuwa na mtendaji mkuu wa chama tangu mwaka 2023 hadi leo sio afya, yeye ndio kila kitu ni kiongozi anayetakiwa kuwepo, huenda ajenda hii ikajadiliwa,” amesema Dk Aviti Mushi, Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM).

Dk Mushi amesema kuna watu wengi wanaotajwa tajwa kumrithi Chongolo, lakini yeye anafikiri huenda Balozi Nchimbi akachukua nafasi hiyo, ingawa CCM ni chama kikubwa chenye hazina ya watu wengi.

Kwa upande wake, mchambuzi wa masuala ya siasa Zanzibar, Ali Makame Issa, amesema katika vikao hivyo kuna mambo matatu yanaweza kujadiliwa ambayo suala la kumteua na kumthibitisha katibu mkuu, watendaji wa Serikali wasioendana na kasi ya Rais Samia, miswada mitatu ya sheria ya uchaguzi na sheria vya siasa ya mwaka 2023 iliyowasilishwa bungeni mwaka jana.

“Kwa hatua tuliyoifikia sasa na kuelekea katika chaguzi za Serikali za mitaa, ni vigumu chama kukaa bila katibu mkuu, inawezekana vikao hivyo vikafanya uamuzi nani atakuwa katibu mkuu pamoja na kupanga mikakati kuhusu miswada ya sheria ya uchaguzi na sheria ya vyama vya siasa,’’ amesema na kuongeza:

“Miswada hii ni moja ya mambo ambayo huenda CCM wakajadili ili kuweka msimamo kama chama utakaodumu kutokana na mapendekezo ya wadau wa demokrasia kuhusu sheria hizo.

Hata hivyo, Issa hakutaka kuweka wazi makada wanaotajwa kuwania kiti cha Chongolo, akisema CCM ina hazina ya watu ambao wakipewa nafasi wanaweza kuwa bora katika utekelezaji wa majukumu yao.