Balozi Ali Karume ahojiwa CCM, yeye aweka msimamo

Dar es Salaam. Chama cha Mapinduzi (CCM) kimeanza ‘kumshughulikia’ mwanachama wake mashuhuri, Balozi Ali Abeid Karume kwa tuhuma za kuwatukana viongozi wa chama hicho na Serikali.

Mara kadhaa, mwanadiplomasia huyo ambaye ni mtoto wa Rais wa kwanza wa Zanzibar, Hayati Abeid Aman Karume amekuwa akitoa kauli kwamba chama hicho kimekosa uhalali wa wananchi kuongoza visiwani humo.

Katika moja ya kauli hizo, Balozi Karume amekituhumu chama chake kuingia madarakani kwa wizi wa kura, akidai CCM haijawahi kushinda uchaguzi wa urais Zanzibar, bali kwa wizi wa kura. Kauli hizo zimeibua mijadala ndani na nje ya chama hicho na juzi, Makamu Mwenyekiti wa CCM-Zanzibar, Rais Hussein Ali Mwinyi akizungumza na wanachama wa chama hizo wa Kusini Unguja wakati akikagua miradi ya maendeleo alisema: “wakati mwingine watu wanavunja maadili lakini wanatazamwa na kusubiriwa kwenye uchaguzi.”

“Huo sio utaratibu tuanze sasa, wanaofanya hivyo washughulikiwe kwa mujibu wa taratibu na ndiyo maana kuna kamati za maadili ndiyo kazi yao.”

Kutokana na hilo alilolisema Rais Mwinyi, gazeti hili lilimtafuta Balozi Karume ambaye alisema alikuwa na mazungumzo marefu na uongozi wa tawi CCM katika tawi lake la Mwera, wamekubaliana kwamba hakutukana.

Mwanasiasa huyo alikiri mwanachama yeyote atakayekiuka maadili kwa kutukana chama na viongozi wake lazima ashughulikiwe.

“Jana (juzi) niliitwa na uongozi wa tawi langu. Baada ya mazungumzo marefu tumekubaliana sijatukana chama wala viongozi. Mhusika asubiri ripoti ya hao aliowatuma kushughulikia suala hilo.”

Alipoulizwa iwapo atakuwa tayari kuomba radhi iwapo atatakiwa kufanya hivyo, Balozi Karume alijibu atafanya hivyo baada ya kuambiwa kosa lake na kama litakidhi kuwa tusi kwa CCM na viongozi wake.

“Nikiambiwa kosa langu na kukidhi kuwa hilo nililosema ni tusi au matusi kwa chama na viongozi wake, kuomba radhi ni uungwana,” alisema.

Kwa mujibu wa Balozi Karume, amewasiliana na Katibu wa Kamati Maalumu ya Idara ya Itikadi na Uenezi Zanzibar, Khamis Mbeto na kukubaliana utayari wake wa kwenda kutoa maoni yake. Gazeti hili lilimtafuta Mbeto kuhusu kuitwa kuhojiwa kwa Balozi Karume ambapo alisema kwa kuwa mwanachama wake huyo kwa sasa hana uongozi wowote ndani ya CCM na Serikali, mchakato wa kuhojiwa kwake unaanzia ngazi ya tawini kwake.

Alieleza tawi litatoa mapendekezo yake kwa wadi juu ya adhabu anayopaswa kuchukuliwa na ngazi ya mwisho ya kumchukulia hatua ni Halmashauri Kuu ya CCM Mkoa anaoishi.

“Halmashauri Kuu ya Mkoa ina nguvu ya kumchukulia hatua hata ya kumfukuza uanachama,” alisema. Alieleza angekuwa ni kiongozi kati ya Mjumbe wa Halmashauri Kuu Taifa (NEC), Mwakilishi au CCM Wilaya, uamuzi wowote dhidi yake ungefanyika na mamlaka za chama hicho kitaifa.