Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

CCM Mara yamvua uanachama diwani wake

Muktasari:

  • Diwani huyo amevuliwa uanachama ikiwa ni takriban miezi tisa tangu ateuliwe na Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi (INEC) kuwa diwani wa viti maalum katika halmashauri ya wilaya ya Rorya akiwakilisha tarafa ya Luoimbo.



Musoma. Halmashauri Kuu ya Chama cha Mapinduzi (CCM) Mkoa wa Mara imemvua uanachama Diwani wa viti maalumu wilayani Rorya, Rosemary Achieng' kwa kile kinachodaiwa ni utovu wa nidhamu.

Diwani huyo amevuliwa uanachama ikiwa ni takriban miezi tisa tangu ateuliwe na Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi (INEC) kuwa diwani wa viti maalum katika halmashauri ya wilaya ya Rorya akiwakilisha tarafa ya Luoimbo.

Rosemary amepokea barua ya kuvuliwa uanachama kutoka ofisi za CCM Rorya jana Jumanne, Julai 21, 2026.

Kwa mujibu wa taarifa diwani huyo amevuliwa uanachama kutokana na masuala ya uchaguzi mkuu uliofanyika Oktoba 2025 ingawa uongozi wa chama hicho mkoa umesema uamuzi huo umefanywa kutokana na utovu wa nidhamu.

Taarifa kutoka Rorya na ndani ya CCM zinadai lengo la kuvuliwa uanachama diwani huyo ni kutaka aliyekuwa mgombea wa udiwani viti maalumu katika uchaguzi huo anayetoka tarafa ya Nyancha (jina linahifadhiwa) apate nafasi hiyo ya uwakilishi wa wanawake.

Taarifa zinaeleza wakati wa mchakato wa kura za maoni kupitia CCM, Rosemary alikuwa mshindi wa pili katika tarafa yake ya Luoimbo baada ya kupata kura zaidi ya 400 huku nafasi ya kwanza kwa tarafa hiyo ikishikwa na Dinna Charles aliyepata kura zaidi ya 500 ambaye pia aliteuliwa na tume kuwa diwani viti maalumu katika halmashauri hiyo.

Inaelezwa baada ya diwani huyo kuteuliwa na tume kuwa diwani wa viti maalumu aliyekuwa mgombea udiwani viti maalumu kutoka tarafa ya Nyancha aliwasilisha malalamiko katika uongozi wa chama akidai nafasi hiyo ilikuwa ni ya kwake hivyo alistahili kuteuliwa yeye.

"Kwanza inashangaza huyu anayedai alitakiwa kuteuliwa, kwenye kura za maoni katika tarafa yake ya Nyancha alishika nafasi ya nne wakati Rosemary alikuwa wa pili katika tarafa yake, lakini pia utaratibu wa kuteuliwa madiwani wa viti maalumu kwa sasa umebadilika na unafanywa na tume sio chama tena," amesema mtoa taarifa ambaye hakutaka jina lake liandikwe.

Amesema baada ya malalamiko hayo kuwasilishwa kwenye uongozi wa chama, Rosemary aliitwa na uongozi uliomtaka aandike barua ya kujiuzulu nafasi yake lakini alikataa kwa maelezo uteuzi wake umefanywa na tume na sio chama.

"Aliwaambia hawezi kujiuzulu labda tume imuandikie barua na kueleza kwa nini anatakiwa kufanya hivyo hapo ilikuwa ni mwaka jana na sakata hilo likatulia hadi Mei mwaka huu alipoitwa tena na chama na juzi tukapata taarifa kuwa amevuliwa uanachama," amesema.

Amesema awali kabla ya tume kuanza utaratibu wa kuteua madiwani, uteuzi huo ulikuwa ukifanywa na chama kwa kuzingatia mgombea aliyeongoza katika kura za maoni na mgao huo pia ulikuwa ukizingatia uwakilishi wa tarafa.

Amesema hata kama chama kingepewa jukumu la kuteua madiwani kwa kufuata utaratibu huo basi mgombea ambaye anadai ana sifa ya kuwa diwani asingeweza kuteuliwa kwani katika tarafa yake alikuwa wa nne.

"Tarafa ya Nyancha ina kata 11 na kama CCM wangeshinda udiwani katika kata zote basi wangepewa nafasi nne za viti maalum lakini katika uchaguzi uliopita kata moja katika tarafa hii ilikwenda upinzani, hivyo CCM kubaki na nafasi tatu za viti maalumu ambazo ingewateua washindi wa kwanza hadi wa tatu kuwakilisha wanawake katika tarafa hiyo na sio huyu wa nne," amesema.

Mwananchi limemtafuta Katibu wa CCM Wilaya ya Rorya, Moshi Hassan ambaye amekiri diwani huyo kuvuliwa uanachama akisema taarifa zaidi zinaweza kutolewa na uongozi wa chama mkoa.

"Ni kweli hili jambo lipo lakini uamuzi umefanywa na mamlaka ya juu yangu hivyo nikuombe utafute uongozi wa mkoa kwa ufafanuzi zaidi," amesema.

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Mara, Patrick Chandi amekiri chama hicho kumvua uanachama diwani huyo huku akikataa kueleza kwa undani makosa aliyofanya.

"Wewe si umesikia ni utovu wa nidhamu, andika hivyo hivyo, ni kweli tumemvua uanachama kwa sababu ya utovu wa nidhamu ila siwezi kueleza kwa undani zaidi kuhusu huo utovu wa nidhamu, kwa sasa tuishie hapo," amesema

Amesema kabla chama hicho hakijafanya uamuzi wa kumvua uanachama diwani huyo aliitwa kwenye vikao kwa ajili ya majadiliano na utetezi dhidi ya tuhuma zilizokuwa zikimkabili, lakini alikataa kuhudhuria kikao hicho.

"Tulimuita aje kwenye kikao akagoma pamoja na taratibu zingine ikabidi tumvue uanachama na kuhusu nafasi yake kuzibwa kwa sasa hebu tusubiri kwanza kila kitu kitafanyika kwa mujibu wa utaratibu, kilichopo ni kwamba tumemvua uanachama," amesema Chandi.

Alipotafutwa kuzungumzia suala hilo diwani huyo alikiri kupokea barua ya kuvuliwa uanachama na kuahidi kuzungumzia suala hilo kwa undani baadaye.

"Tangu jana kuna mambo nafuatilia, kwa sasa sina muda wa kuliongelea hili, nitaongea baadaye labda kesho au siku nikipata nafasi," amesema.