CCM watofautiana Mwinyi kuongezewa muda wa urais

Katibu wa Halmashauri Kuu ya CCM, Itikadi, Uenezi na Mafunzo, Amos Makala (kushoto) na Naibu Katibu Mkuu wa CCM, Zanzibar, Dk Mohamed Dimwa (kulia).
Muktasari:
- Makala asema bajeti ya uchaguzi imeshapangwa na chaguzi zitaendelea kama kawaida, asisitiza maamuzi hufanywa na vikao rasmi vya chama.
Dar es Salaam. Wakati Sekretarieti ya Kamati Maalumu ya CCM, Zanzibar ikipitisha pendekezo la kuishauri Kamati Maalumu kuridhia kuongeza muda wa Rais Hussein Mwinyi, Katibu wa Halmashauri Kuu ya CCM, Itikadi, Uenezi na Mafunzo, Amos Makala amesema jambo hilo halipo.
Jana, Naibu Katibu Mkuu wa CCM, Zanzibar, Dk Mohamed Dimwa aliweka wazi nia ya kumwongezea muda Rais Mwinyi mpaka saba.
Dk Dimwa alisema wajumbe wa Sekretarieti ya Kamati Maalumu ya CCM wamepitisha pendekezo la kuishauri Kamati Maalumu kuridhia kuongeza muda wa Rais Mwinyi kuongoza nchi katika muhula wake wa kwanza kwa kipindi cha miaka saba badala ya miaka mitano.
"Wajumbe wa sektetarieti tumejadili na kutathmini kwa kina juu ya utendaji wa Rais Mwinyi, tukajiridhisha kuwa hakuna mbadala wake na anastahili aongoze nchi kwa kipindi cha miaka saba, ili apate muda mzuri wa kufanya mapinduzi ya kimaendeleo katika nyanja za kiuchumi na kijamii,” alisema Dk Dimwa wakati wa hotuba yake ya kufunga Mkutano wa Baraza Kuu la UVCCM Wilaya Dimami.
Akizungumza leo Jumatatu Juni 24, 2024 katika kipindi cha Power Breakfast kinachoendeshwa na Kituo cha Redio cha Clouds, jijini Dar es Salaam, Makala amesema tayari bajeti ya kugharimia chaguzi zote imeshapangwa, hivyo chaguzi zitafanyika kama kawaida.
“Kwa ufupi sana niseme, hilo jambo halipo,” amesema huku akisisitiza CCM inaendeshwa na vikao na kwamba kikao kilichotoa msimamo huo si kile kinachoongozwa na viongozi wa juu.
Ameeleza vikao vya chama hicho vinavyofanya maamuzi ni Sekretarieti inayoongozwa na Katibu Mkuu, Kamati Kuu inayoongozwa na Mwenyekiti wa Taifa na Kamati Maalumu ya Zanzibar inayoongozwa na Makamu Mwenyekiti Zanzibar.
Katika vikao vyote hivyo, amesema yeye ni mmoja wa wajumbe na taarifa zote zinazotokana na vikao hivyo zinapaswa kutolewa naye, lakini kuhusu suala hilo hakusikia na halipo kwenye utaratibu wake.
“Nimelisoma kwenye mitandao kama ninyi mlivyosoma. Mimi ndiye Katibu Mwenezi wa CCM, ndiyo msemaji wa CCM, kwa hiyo vikao vyote vya CCM vikimalizika mimi ndiye napaswa kusema, kwa hiyo hilo halipo katika utaratibu wangu,” amesema Makala.
Hata hivyo, amesisitiza kilichozungumzwa katika kikao hicho (alichokisema Dk Dimwa) ni wazo ambalo hata hivyo halijafikishwa katika vikao vikubwa na halikupaswa kuwekwa wazi.
Lakini, msisitizo wa maelezo yake umejikita katika hoja kuwa, bajeti ya mwaka ujao wa fedha, pamoja na mambo mengine fedha imetengwa kwa ajili ya kugharimia chaguzi na hivyo uchaguzi utafanyika kama ilivyopangwa.
“Tumeongelea bajeti hapa, tumeweka hela ya uchaguzi wa mitaa, tumeweka hela ya uchaguzi mkuu, uchaguzi upo kama kawaida,” amesisitiza.