CCM Zanzibar yampinga Dk Dimwa Rais Mwinyi kuongezewa muda

Katibu wa Idara ya Itikadi na Uenezi CCM Zanzibar, Khamis Mbetto akizungumza na waandishi wa habari katika Ofisi Kuu ya CCM Kisiwandui. Picha na Zuleikha Fatawi
Muktasari:
- Khamis Mbetto, Katibu wa NEC, Itikadi, Uenezi na Mafunzo Zanzibar, asisitiza kauli ya Dk Dimwa ni maoni binafsi, si msimamo wa CCM.
Dar es Salaam. Baada ya Chama cha Mapinduzi (CCM) Bara kudai nia ya kumwongezea Rais wa Zanzibar, Hussein Mwinyi muda wa kukaa madarakani si msimamo wa chama hicho, Katibu wa NEC, Itikadi, Uenezi na Mafunzo visiwani humo, Khamis Mbetto naye amepigia msumari kauli hiyo.
Katika kauli yake, Mbetto amesema kilichozungumzwa na Naibu Katibu Mkuu wa CCM Zanzibar, Dk Mohamed Dimwa ni maoni yake binafsi, si msimamo wa Sekretarieti ya Kamati Maalumu wala wa chama hicho.
Hayo yanatokea ikiwa ni siku moja tangu Dk Dimwa aeleze sekretarieti hiyo imejadili na kutathmini utendaji wa Rais Mwinyi na kujiridhisha kuwa hakuna mbadala wake, hivyo anastahili aongoze nchini kwa miaka saba badala ya mitano.
Mbetto ametoa kauli hiyo leo Jumatatu, Juni 24, 2024 alipozungumza na Mwananchi Digital na kuongeza kilichozungumzwa na Dk Dimwa ni maoni yake binafsi, haukuwa msimamo wa chama kama inavyoaminiwa na wengi.
Maoni hayo ya Dk Dimwa, amesema yametokana na ziara ya Sekretarieti ya Kamati Maalumu ya chama hicho iliyohusisha kupokea taarifa za utekelezaji wa Ilani ya CCM.
“Yalikuwa maoni yake, lakini msimamo wa CCM ni kwamba Rais Mwinyi ameapa kutumikia kwa miaka mitano na Katiba ya nchi na chama inasema hivyo,” amesema.
Kuhusu kauli ya Dk Dimwa, amesema ni kama aliteleza, isipokuwa bado ana nafasi ya kupeleka pendekezo lake hilo katika vikao vya juu ambavyo yeye ni mjumbe.
Kwa sababu suala la kumuongezea kiongozi muda linahusisha mabadiliko ya Katiba ya nchi na chama, amesema kuna michakato mingi kufanikisha hayo.
Kuhusu alichokijibu Makala, Mbetto amesema ni kweli utaratibu wa CCM hufanya maamuzi yake kwa vikao na jambo hilo halikupitia mchakato huo, hivyo ni maoni tu bado haujawa msimamo.