Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Chadema yasubiri uamuzi wa Msajili, yeye asema…

Muktasari:

  • Chadema imesema imekamilisha mchakato wa kujibu hoja zote zilizoainishwa katika barua ya Msajili ya Mei 26,2026 ambayo ilikitaka chama hicho hadi leo saa tisa na nusu alasiri kiwe kimeshawasilisha majibu yake.

Dar es Salaam. Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) kinasubiri uamuzi wa Msajili wa Vyama vya Siasa baada ya kuwasilisha majibu ya tuhuma zote zilizoelekezwa dhidi yake na Ofisi ya Msajili.

Chadema imesema imekamilisha mchakato wa kujibu hoja zote zilizoainishwa katika barua ya Msajili, ambayo ilikitaka chama hicho hadi leo saa tisa na nusu alasiri kiwe kimeshawasilisha majibu yake.

Hata hivyo, Naibu Msajili wa Vyama vya Siasa, Sisty Nyahoza, akizungumza na Mwananchi amesema ukomo wa muda uliotolewa kwa Chadema kujibu barua hiyo unaisha leo Jumatatu, Juni 8, 2026 saa tisa na nusu alasiri.

“Nipo nje ya ofisi, bado sijaona majibu yao, lakini muda tuliowapa kuwasilisha majibu unaisha leo saa 9:30 alasiri. Kesho nitakuwa katika nafasi nzuri ya kuzungumzia baada ya muda huo kuisha,” amesema Nyahoza.

Majibu hayo yanatokana na barua ya Mei 26, 2026, iliyotolewa na Msajili wa Vyama vya Siasa, ikiitaka Chadema kujieleza kwa nini kisichukuliwe hatua kwa madai ya kukiuka Sheria ya Vyama vya Siasa.

Chama hicho kilipokea barua hiyo wiki chache baada ya barua ya Mei 7, 2026, ambayo pia ilikitaka Chadema kutoa maelezo kwa nini isichukuliwe hatua za kisheria, zikiwemo kusimamishwa usajili wake au kutozwa faini kutokana na tuhuma za ukiukaji wa sheria hizo.

Katika barua ya Mei 26, 2026, ambayo Chadema inasema tayari imeijibu, Msajili kupitia Naibu wake Sisty Nyahoza alieleza kuwa chama hicho kilitakiwa kutoa maelezo kuhusu utekelezaji wa masharti ya Sheria ya Vyama vya Siasa Sura ya 258 (toleo la urekebu la mwaka 2023) katika shughuli zake.

Msajili alidai katika mitandao ya kijamii kuna video zinazoonesha Mwenyekiti wa Chadema Kanda ya Nyasa, Joseph Mbilinyi, akitoa kauli zenye matusi, kashfa na dhihaka dhidi ya wanasiasa wenzake katika mkutano wa hadhara wa chama hicho.

Kitendo hicho kilielezwa na Msajili kuwa kinakiuka Kifungu cha 9(2) na 19(2)(f) vya Sheria ya Vyama vya Siasa, pamoja na Kanuni ya 8(a) ya Kanuni za Kuratibu Mikutano ya Hadhara ya Vyama vya Siasa za mwaka 2023 (TSN. 209).

Nyahoza alinukuu pia baadhi ya kauli zilizodaiwa kutamkwa na Mbilinyi katika mkutano huo, ikiwemo maneno ya kejeli dhidi ya wapinzani wake wa kisiasa.

Pia, katika barua hiyo Msajili aliwataja viongozi wengine wa Chadema, akiwemo Mwenyekiti wa Kanda ya Kaskazini, Samwell Welweli na Mjumbe wa Kamati Kuu ya Chadema Taifa, Godbless Lema, kwa madai ya kutoa maneno yanayochochea uadui na kuhamasisha kupambana na Jeshi la Polisi badala ya kuheshimu sheria za nchi.

Msajili alieleza kuwa kauli hizo zinakiuka vifungu vya 9(2) na 19(2)(1) vya Sheria ya Vyama vya Siasa, hivyo chama kilitakiwa kutoa maelezo ya kujieleza.

Akizungumza na Mwananchi, Dar es Salaam leo Juni 8, 2026, Kaimu Katibu Mkuu wa Chadema, Pamela Maassay, amesema chama kimekamilisha kujibu barua hiyo kwa kuzingatia hoja zote zilizoelekezwa.

“Hoja zote tumezijibu kama zilivyoainishwa katika barua hiyo, na tumeshawasilisha majibu yetu jana katika Ofisi ya Msajili kupitia nakala tepe na barua pepe, zote Dar es Salaam na Dodoma,” amesema Maassay.

Maassay, ambaye pia ni Katibu Mkuu wa Baraza la Wanawake Chadema (Bawacha), amesema sasa wanasubiri uamuzi wa Msajili na kuwahimiza wanachama kuendelea kukijenga chama.

Katika barua hiyo ya Mei 26, 2026, Msajili ametaja vifungu mbalimbali vya sheria, ikiwemo kifungu cha 7, 39(2)(a), 45 cha Sheria ya Vyama vya Siasa pamoja na marekebisho ya Sheria Namba 3 ya mwaka 2024, pamoja na Kanuni ya 11(2) ya Kanuni za Kuratibu Mikutano ya Hadhara ya Vyama vya Siasa za mwaka 2023, kama msingi wa maelekezo yaliyotolewa.

Maelekezo hayo ni pamoja na kuitaka Chadema kutoa maelezo kwa nini usajili wake usisimamishwe au kutozwa faini kwa madai ya kukiuka masharti ya sheria na kanuni zinazosimamia shughuli za vyama vya siasa.

“Maelezo yenu yawasilishwe Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa si zaidi ya tarehe 08 Juni 2026 saa tisa na nusu alasiri,” ilieleza barua hiyo, ikibainisha pia kuwa video husika zilitumwa kwa barua pepe na WhatsApp ya chama na viongozi wake.

Barua hiyo iliisha kwa Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa kutoa wito wa kuwasihi Chadema kufuata Katiba ya Tanzania ya mwaka 1977 na sheria za nchi katika utekelezaji wa shughuli zake za kisiasa.