Chatanda apongeza ukomavu wa demokrasia ndani ya CCM

Muktasari:

Mwenyekiti wa Umoja wa Wanawake wa CCM (UWT), Mary Chatanda, amesifu ukomavu wa demokrasia ndani ya chama hicho huku akipigia chapuo asilimia 30 ya nafasi kutengwa kwa jinsia kike kuingia kwenye vyombo vya uamuzi ndani ya chama hicho. 

Dar es Salaam. Mwenyekiti wa Umoja wa Wanawake wa CCM (UWT), Mary Chatanda, amesifu ukomavu wa demokrasia ndani ya chama hicho huku akipigia chapuo asilimia 30 ya nafasi kutengwa kwa jinsia kike kuingia kwenye vyombo vya uamuzi ndani ya chama hicho. 

Amesema hayo ni mapinduzi makubwa mno katika agenda ya usawa wa kijinsia katika uongozi kama inavyosisitizwa na Ilani ya chama hicho ya 2020/2025.

Akizungumza Dodoma leo Desemba 08/2022, wakati akitoa pongezi kwa viongozi waliochanguliwa kwenye nafasi mbalimbali, Chatanda amesema kiongozi wa chama hicho, Rais Rais Samia Suluhu Hassan amekuwa mdau wa usawa wa kijinsia katika uongozi wake.

“Tunampongeza na tunajivunia kuwa na Rais mwanamke wa kwanza tangu tupate uhuru mwaka 1961 ambaye hamungunyi maneno lipokuja suala la usawa wa kijinsia. Vitendo vyake vinazungumza kwa sauti kubwa,” amesema.

Aidha amesema UWT inawapongeza wanawake wote 12 walioshinda katika nafasi ya ujumbe wa Halmashauri Kuu ya CCM Taifa kati ya Wanawake 80 walioteuliwa kugombea nafasi hiyo katika uchaguzi huo wa mwaka 2022.

“Wanawake wote ambao kura hazikutosha, tunawaomba wasife moyo, kuna kushinda siku nyingine, uchaguzi umeisha sote tuwe wamoja, tuvunje makundi, tujenge Chama chetu na tuimarishe UWT yetu,” amesema.


Chatanda amesema katika kuzingatia usawa wa kijinsia, wanaamini huo ni mwanzo mzuri katika kupanua demokrasia.