Cuf yajipanga kudai tume huru za uchaguzi
Kaimu Naibu Katibu Mkuu wa CUF bara, Joram Bashange (katikati) akizungumza na waandishi wa habari juzi katika Ofisi za Makao Makuu ya chama hicho Vuga mjini Unguja. Kushuto ni Naibu Katibu Mkuu wa chama hicho Zanzibar, Nassoro Ahmed Mazrui na kulia ni Kaimu Naibu Mkurugenzi Habari, Uenezi na Uhusiano wa Umma, Mbarara Maharagande. Na Mpigapicha Wetu
Muktasari:
- Akizungumza na waandishi wa habari katika ofisi za chama hicho zilizopo Vuga, Zanzibar juzi, Kaimu Naibu Katibu Mkuu wa Cuf -Bara, Joram Bashange alisema maandalizi yanaendelea na hivi karibu watatoa tamko.
Zanzibar. Chama cha Cuf kimesema kinajipanga kuvishawishi vyama vingine vya siasa na taasisi binafsi kuunganisha nguvu kudai tume huru za uchaguzi kabla ya mwaka 2020.
Akizungumza na waandishi wa habari katika ofisi za chama hicho zilizopo Vuga, Zanzibar juzi, Kaimu Naibu Katibu Mkuu wa Cuf -Bara, Joram Bashange alisema maandalizi yanaendelea na hivi karibu watatoa tamko.
Bashange alisema wajumbe wa kamati ya utendaji ya chama hicho chini ya Katibu Mkuu, Maalim Seif Sharif Hamad katika kikao walichofanya walikubaliana kusukuma suala hilo ili kuhakikisha uchaguzi ujao unakuwa huru na wa haki.
Alisema ikiundwa tume huru ni wazi itasaidia kufanikisha uchaguzi ujao na kwamba, mawakala hawatatolewa vituoni, kura zitahesabiwa kwa uhuru na matokeo yatatangazwa kwa mujibu wa sheria.
Pia, alisema walikubaliana mchakato huo uhusishe makundi yote ya kisiasa na kijamii ili kuonyesha umoja wao.