Elimu ya mipaka ya uongozi itolewe

Usipofikiria kwa kina unaweza kudhani Waswahili tuna dharau sana. Huku kwetu watu wanakariri mambo kutokana na maisha ya kila siku. Hawana muda wa kuuliza wala data za kusomea mitandaoni.

Wakati wote tuna mchakamchaka wa kutafuta chakula, kodi ya nyumba, ada za watoto na marejesho ya mikopo, Sh500 ya kununulia bando inaweza kusababisha watoto wakanywa chai ya mkandaa bila kitafunwa.

Waswahili tunakosa hata muda wa kucheki afya zetu. Si kwamba hatujui umuhimu, lakini tunapata muda lini na saa ngapi kufanya hivyo.

Usishangae ukiambiwa kuwa watu walijiandikisha kwa wingi kupiga kura si kwa sababu waliielewa vizuri elimu ya mpigakura, bali waligundua kuwa kitambulisho cha kura kingewasaidia kwenye mambo kadhaa, ikiwemo kusajili laini za simu!
Hivi sasa kila mmoja wetu analipa kodi ya majengo si kwa sababu wameelewa somo, bali ni kwa sababu inakatwa moja kwa moja kila mwezi kupitia kwenye manunuzi ya umeme wa Luku.

Niwapongeze wabunifu waliofanikisha jambo hilo kwa kuwa si kwamba hatutaki kulipia majengo, bali muda wa kukimbizana na mabasi na kupanga foleni kupata huduma umekuwa si rafiki kwetu.

Lakini pia ningewashauri Serikali kubuni elimu mbadala wa haki za raia, tena somo hilo lingekuwa tamu zaidi iwapo elimu ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano ingejumuishwa. Si kwamba hatutaki kujifunza, ila tunaogopa muda tuliopoteza ujanani usije kuwakosti watoto wetu.

Hatuna budi kujituma kila nukta ili nao wapate elimu na maisha bora katika wakati wao. Sisi tulizikosa ngazi kadhaa katika kupanda ghorofa.
Tulizoea enzi za mfumo wa chama kimoja, mjumbe wa chama tawala alituletea taarifa na maagizo yote kutoka ngazi za juu. Huyu ndiye aliyekuwa daraja kati ya nyumba 10 za mtaani na Serikali.

Hii ilitokana na marekebisho ya Katiba ya mwaka 1984, kufuatia sheria iliyopitishwa bungeni mwaka huo. Sheria hii ilikipa chama mamlaka ya kusimamia shughuli zote za Serikali, au kwa lugha nyingine “kushika hatamu za uongozi”.

Lakini mwaka 1992, mfumo ukabadilika baada ya Bunge kuridhia demokrasia ya vyama vingi. Katiba ikafanyiwa marekebisho tena mwaka huo na kukiondoa kipengele kilichokipa nguvu chama kushika hatamu. Zile nguvu na shughuli za wajumbe wa nyumba 10 zikarasimiwa na Serikali za mitaa.

Mpaka hapo watu hatukuwa tumepata elimu ya kutosha kuhusu muundo wa Serikali ya Mtaa, bali tulikariri vyeo vya “mtendaji”, “mwenyekiti”, “katibu” na kadhalika bila kuelewa nani ni nani katika chama, Serikali au vyote viwili; chama na Serikali.

Ikumbukwe kuwa wakati uliopita ni mjumbe mmoja kutoka chama pekee cha siasa ndiye aliyeshughulika na kila kitu mtaani kwetu. Sasa swali likabaki jambo lipi linashughulikiwa na nani katika Ofisi ya Serikali ya Mtaa.

Hilo likawafanya watu waendelee na mazoea kwa mjumbe wao. Walipotaka kuidhinishiwa fomu zao na Serikali, waliendelea kumtumia mjumbe yuleyule wa zamani. Lakini pamoja na kuwa walipata walichohitaji, baadhi ya wanamtaa wanahisi “kupigwa” pale wanapolipia huduma kwenye Ofisi ya Serikali bila kupatiwa risiti, au kupewa risiti zisizotambulika na Mamlaka ya Mapato.

Wanachojua ni kwamba wao ndio waendeshaji wa ofisi za Serikali kupitia kodi wanazolipa.

Ni jambo jema na ni majukumu ya mjumbe wa chama kuwa daraja la wanachama wake kwa Serikali. Lakini ni jambo la msingi kwake na kwa wananchi kuelewa uhusiano, nguvu na mipaka ya vyama vya siasa katika Serikali. Nasema hivi kwa sababu matukio na mijadala inayoendelea huko mitandaoni inatupa wasiwasi. Kuna hisia kwamba elimu haitolewi kwa makusudi ili “mambo fulani” yaendelee kama zamani.

Hakihitajiki cheti kwa mtu yeyote kuelewa kwamba nchi yetu inaendeshwa na Katiba na Sheria za Jamhuri za Muungano. Wala kujua kwamba Bunge ndilo linaloidhinisha vitu hivyo viwili kwenda kusimamiwa na Serikali.

Kwa mantiki hiyo, Serikali inajipambanua kuwa baba wa vyama vyote vya siasa, kwani ndiyo iliyovisajili, kama wewe Mheshimiwa ulivyo, Rais wa Watanzania wote bila kujali itikadi zao za vyama.

Kwa uelewa wetu, viongozi wa vyama vya siasa wanapaswa kuwaheshimu wateule wa Serikali. Lakini mambo yanayoendelea uswahilini na kwenye mitandao ya kijamii yanaongeza sintofahamu miongoni mwetu. Si hivyo tu, lakini pia yanatutia wasiwasi kwamba yanaweza kuibua taharuki miongoni mwetu. Ipo hii ya kiongozi mteule wa chama aliyemsimamisha mkuu wa mkoa na kumwamuru kukimbia mchakamchaka.

Mama, kwanza niseme sijawahi kukuona ukifanya kitendo kama kile. Lakini pia naogopa kisijezua taharuki, kwani mkuu wa mkoa ni mwenyekiti wa kamati ya ulinzi na usalama mkoani pake. Heshima yake ni kubwa kwa vyombo vya ulinzi na usalama zaidi ya yule mtoa amri. Asije naye akajibu mapigo kwa kuviamrisha vyombo hivyo kuchukua hatua dhidi ya kiongozi mwenzake.

Hii ndiyo sababu nasisitiza elimu zaidi juu ya mipaka ya viongozi wa vyama kwa wale wa Serikali. Labda sisi hatuelewi, basi tunaomba tueleweshwe ili amani na usalama vizidi kustawi nchini mwetu, na kuepusha jeuri, chuki na uhasama.