NIKWAMBIE MAMA: Hawawezi kutumikia mabwana wawili eti!

Ulisema wakati ukilihutubia Bunge la Kenya kuwa ni wakati sasa wa viongozi kubadilika na kuwa daraja kwa wafanyabiashara, na si kuwa vikwazo kwao. Nilivyoelewa mimi ni kwamba viongozi wakifuata kanuni kama zilivyo, njia ya wafanyabiashara na wawekezaji huwa nyepesi sana. Lakini, iwapo viongozi wanafanya kwa kujinufaisha wao binafsi, wawekezaji wanapata wakati mgumu na kuamua kutowekeza katika nchi zetu.

Tatizo la watu wetu ni kudhani kwamba kupata uongozi ndio fursa ya utajiri.

Kitu cha kwanza atakachofikiria kiongozi ni maisha ya kifahari. Atafanya kila awezavyo kujipatia majumba na magari ya fahari, mahoteli na ikiwezekana zaidi ya hivyo. Atasomesha watoto wake Ulaya, familia yake itakwenda kupumzika na kutibiwa nje, atafanya manunuzi yake kwenye masoko maarufu duniani, na fujo nyingine chungu nzima.

Ili afanikishe azma yake, kiongozi huyu atatafuta chaka la kufichia utajiri. Katika nchi zetu masikini, njia rahisi ni kutumia fursa alizonazo kupata msingi wa biashara. Kwa fursa hizohizo ataifanya biashara yake kumeza hata bajeti nzima ya Serikali bila yeyote kuhisi ukiukwaji wa maadili. Ni kawaida gari ya kifahari mbele ya nyumba masikini kuzua maswali, lakini helikopta ikiwa kwenye paa la hoteli ya nyota tano haina ubaya.

Mwalimu Nyerere alikataza watumishi hasa viongozi wa Serikali kuwa wafanyabiashara. Alihofia kwamba kujichanganya kwenye biashara kungemfanya ashindwe kufanya majukumu yake kwa uadilifu. Wafanyabiashara wana dunia yao inayowakutanisha kwenye shughuli zao, hivyo kiongozi anaweza akajikuta yupo njia panda katika maamuzi magumu dhidi ya wafanyabiashara wenzake.

Sisemi kwamba kiongozi akifanya biashara anatenda dhambi, bali awe na ukomo katika biashara kiasi cha kutoa nafasi ya kutekeleza majukumu yake ya uongozi. Achague aina ya biashara itakayompa nafasi.

Anaweza kuwa mkulima wa mazao yanayoweza kuingia sokoni, hivyo akapanga safu yake ya wakulima na wafanyabiashara wakati akiendelea kushughulika na majukumu ya kitaifa bila kudhibitiwa na biashara yake.

Kuna viongozi ambao walishindwa kuzingatia hilo wakajikuta hawana muda wa kukaa majimboni mwao, wala kwenye makao makuu ya Serikali huko Dodoma.

Kila siku wapo Dar es Salaam, China na Dubai kwenye pilikapilika za biashara zao. Kwa mtu aliyepewa dhamana ya uongozi, kufanya hivyo ni makosa kwa sababu Tanzania haihitaji viongozi wabinafsi. Hawa walipaswa kuachana na moja kati ya biashara au uongozi.

Hatari nyingine ni pale kiongozi anapotumia cheo chake kama nyenzo ya kufanikisha biashara zake.

Mara nyingi rasilimali za Taifa zimekuwa zikitumiwa vibaya na viongozi wasio waadilifu.

Kodi ya wananchi imekuwa ikitumika kuneemesha biashara za mtu mmoja mmoja badala ya Taifa zima.

Hili limesababisha wao kuneemeka ilhali sisi tukiendelea kudhoofika kiuchumi.

Wengi ni wafanyabiashara wakubwa kwenye sekta nyeti kama mafuta, madini, nyara, mazao ya baharini na kadhalika. Kwa kuondoa sintofahamu kwa wakuu wake na miongoni mwa wananchi, huzisajili biashara hizo kupitia majina tofauti.

Lakini wengine hutumia vyeo walivyonavyo kubadilisha fursa walizonazo kwa mlungula. Ndio pale unapokuta wafanyabiashara wakikwamishwa kwa vikwazo visivyo vya lazima wanapogoma kutoa rushwa.

Cheo ni dhamana. Mtanzania yeyote anayechaguliwa au kuteuliwa katika uongozi ni lazima awe na akili timamu.

Ameamua kuutumikia umma, na anajua miiko ya uongozi. Moja ya vitu vigumu sana ni kuzima data wakati wa kuapa mbele ya Mwenyezi Mungu na mbele ya Katiba kwamba atatenda haki sawa kwa kila mtu. Kama vile haitoshi, anapaswa kuapa kutotumia mali ya umma kwa manufaa yake binafsi.

La kushangaza hapa kwetu viongozi wanaapa huku wakijua kuwa watakwenda kinyume na kiapo. Wana uhakika kwamba pindi wakishtukiwa watachukuliwa hatua ya kuhamishwa vituo vya kazi, kushushwa vyeo au kufukuzwa kwenye uongozi. Hilo ndilo linalowafanya wawekeze zaidi kwenye biashara na kujiwekea uhakika wa kutotetereka kimaisha linapotokea la kutokea.

Kumbe ndio maana viongozi wetu wamekuwa wakatili dhidi yetu. Wanakula rushwa bila soni wala huruma kiasi cha kusigina haki za wajane na mayatima, kusababisha wagonjwa wafe kwa ukosefu wa dawa, wajawazito kupoteza maisha yao na ya vichanga kwa ukosefu wa huduma, na wala hawaumii kwa watoto masikini kukosa shule na madarasa. Na wala hawaioni dhambi kubwa wanayoitenda mbele za Mungu na wanadamu.

Viongozi wetu huwa tunamalizana mara tu wanapotangazwa kushinda kwenye chaguzi. Sisi tuliowachagua hatuna thamani tena kutoka siku hiyo.

Kibaya zaidi, japo tuliwachagua wenyewe hatuna uwezo wa kuwaonya wala kuwaadabisha tena. Wanaacha kututumikia na wanaanza kututumikisha na kutuumiza kwa rushwa katika mahitaji na haki zetu za msingi.

Rushwa ni adui wa haki. Yeyote anayeweza kupitia hatua ya kiapo halafu akaja kufanya mauzauza kama hayo anapoteza sifa ya kuwa mwanadamu.

Mtu anayeweza kumwongopea Mungu aliyemuumba hadharani anaweza kuliangamiza Taifa zima apatapo nafasi hiyo.

Haishangazi kwa Rais Kiduku wa Korea kuamua kumnyonga mjomba wake baada ya kupatikana na tuhuma za rushwa. Lakini pia adhabu ya mla rushwa katika baadhi ya mataifa ni kifo.