Gachagua akataa fidia ya Sh1 bilioni, kukata rufaa
Aliyekuwa Naibu Rais wa Kenya, Rigathi Gachagua. Picha na Mtandao
Muktasari:
- Amesema timu ya mawakili itawasilisha rufaa Mahakama ya Rufani, kubatilisha baadhi ya maamuzi muhimu yaliyotolewa na Mahakama Kuu.
Nairobi. Aliyekuwa Naibu Rais wa Kenya, Rigathi Gachagua, amekataa fidia ya Ksh50 milioni sawa na (Sh1 bilioni ) alizopewa na Mahakama Kuu kama fidia ya ukiukwaji wa haki zake za kikatiba, akisema kiasi hicho hakishughulikii masuala ya msingi aliyoyaibua kupitia kesi ya kupinga kuondolewa kwake madarakani.
Akizungumza na waandishi wa habari jana Juni 9, 2026 nchini Kenya, Gachagua alikosoa Mahakama Kuu kuthibitisha kuondolewa kwake ofisini, wakati huohuo ikikiri haki yake ya kusikilizwa ilikiukwa wakati wa mchakato wa seneti.
"Kiasi cha KSh50 milioni nilichopewa ni dharau kwa haki na uhuru wangu wa msingi, na ni kejeli kwa katiba," alisema.
Katika hukumu iliyotolewa Jumatatu Juni 8, 2026 na jopo la majaji watatu Eric Ogolla, Anthony Mrima na Freda Mugambi, Mahakama ilibaini kuwa wabunge na maseneta walikuwa na sababu za kutosha za kuanzisha na kuendeleza mchakato wa kumuondoa Gachagua madarakani Oktoba 2024.
Mahakama ilikataa ombi la kufuta uamuzi wa seneti, hatua inayomaanisha kuwa kuondolewa kwake madarakani kumeendelea kubaki halali kisheria.
Hata hivyo, majaji walibaini baadhi ya haki zake za kikatiba zilikiukwa wakati wa mchakato huo na kuamuru alipwe fidia ya Ksh50 milioni za Kenya, (sawa na Sh1 bilioni).
Hata hivyo, Gachagua alisisitiza kuwa shauri lake halikuwahi kulenga kupata fidia ya kifedha, bali lilikuwa na dhamira ya kutetea misingi ya katiba na kuhakikisha kuwa taratibu za haki zilifuatwa ipasavyo.
Alisema uamuzi huo unaibua maswali muhimu kuhusu namna haki za kikatiba zinavyolindwa na jinsi michakato ya kuwaondoa viongozi madarakani inavyotekelezwa nchini huo.
Kwa mujibu wa Gachagua, suala kuu lililokuwa mbele ya mahakama hiyo, ilikuwa kubaini iwapo kinga na taratibu za kikatiba ziliheshimiwa katika kila hatua ya mchakato wa kumng’atua madarakani.
Gachagua kukataa rufaa
Gachagua alisema uamuzi wa Mahakama unatuma ujumbe wa wasiwasi kuhusu ulinzi wa haki za kikatiba.
Alihoji jinsi mahakama inatambua kwamba haki za mtu zilikiukwa wakati wa mchakato fulani, lakini bado ikaruhusu matokeo ya mchakato huo kubaki halali.
Gachagua alisisitiza ulinzi unaotolewa na katiba haupaswi kuchukuliwa kama taratibu za kawaida zinazopuuzwa na baadaye kufidiwa kwa fedha.
Kwa miezi kadhaa, Gachagua amekuwa akidai kuwa kuondolewa kwake madarakani kulichochewa kisiasa na kulifanyika kwa namna iliyopuuzia kinga na haki zinazohakikishwa na katiba.
Katika ombi lake mahakamani, alipinga vipengele mbalimbali vya mchakato huo, ikiwa ni pamoja na mwenendo wa Bunge, namna ushahidi ulivyoshughulikiwa, na uamuzi wa seneti kuendelea na vikao vya kusikiliza shauri hilo licha ya kuwa alikuwa mgonjwa.
Hata hivyo, Mahakama Kuu ilitupilia mbali hoja zake nyingi na kuthibitisha uhalali wa kuondolewa kwake madarakani. Majaji pia walithibitisha uteuzi wa Kithure Kindiki kama Naibu Rais, jambo ambalo kwa kiasi kikubwa lilifunga njia ya kubatilisha mabadiliko ya uongozi kupitia Mahakama Kuu.
Pamoja na hayo, Gachagua alisema kuwa mapambano hayo bado hayajaisha, akielezea kuwa timu yake ya mawakili itawasilisha rufaa Mahakama ya Rufani kubatilisha baadhi ya maamuzi muhimu yaliyotolewa na Mahakama Kuu.
Rufaa hiyo inatarajiwa kujikita zaidi iwapo mchakato utakuwa halali baada ya mahakama kubaini haki za kikatiba zilikiukwa wakati wa utekelezaji wake.
Wataalamu wa sheria wanasema, kesi hiyo itakuwa na athari kubwa zaidi ya mustakabali wa kisiasa wa Gachagua.
Rufaa hiyo huenda ikawa kipimo muhimu cha viwango vinavyopaswa kufuatwa katika mchakato wa kumuondoa Ofisa wa umma madarakani, na kufafanua kiwango ambacho ukiukaji wa katiba unaathiri uamuzi unaofanywa na Bunge na Seneti.
Kadri suala hilo linavyoelekea katika hatua inayofuata ya kisheria, Gachagua anasisitiza lengo lake bado halijabadilika kutafuta majibu kuhusu kile anachokiona kama jambo muhimu la kikatiba, badala ya kufuatilia fidia ya kifedha.