Prime
Huyu ndiye Bassirou Faye aliyeishangaza dunia kutokea Senegal
Kiongozi wa upinzani Senegal, mwenye nguvu zaidi, Ousmane Sonko, alitarajiwa kuwa mgombea urais mwenye nafasi kubwa ya kushinda katika uchaguzi mkuu 2024, hata hivyo alizuiwa kugombea.
Karima Wade, mtoto wa Rais wa tatu wa Senegal, Abdoulaye Wade, alikuwa mgombea urais mwingine mwenye nguvu, aliyetarajiwa kutoa ushindani mkubwa. Karim pia alizuiwa kugombea.
Sonko, baada ya kuzuiwa kugombea urais, aliwaangukia Wasenegali wamchague Bassirou Diomaye Faye. Karim, alijipanga kugombea urais kupitia Chama cha Senegalese Democratic (PDS), kilichoasisiwa na baba yake mwaka 1974.
Baada ya Karim kuondolewa kwenye kinyang’anyiro cha urais, yeye na chama chake, walifanya kampeni kuhakikisha Faye anashinda kiti cha urais. Hata Wade, Rais mstaafu na Katibu Mkuu wa PDS, alifanya kampeni kumwombea kura Faye.
Mgombea mwingine wa urais, Cheikh Tidiane Dieye, alijitoa kwenye mbio na kumuunga mkono Faye. Mshikamano ulikuwa na shabaha moja tu; kuondokana na Rais Macky Sall na masalia yake.
Sall, amekuwa madarakani tangu mwaka 2012. Katika uchaguzi wa Rais Senegal, uliofanyika Machi 24, 2024, Sall alimfanyia kampeni Amadou Ba, ambaye matokeo yameonesha ameshika nafasi ya pili.
Ba, Waziri Mkuu wa Senegal, Septemba 17, 2022 mpaka Machi 6, 2024, alipojiuzulu ili kuwania urais, alishiriki uchaguzi kwa tiketi ya chama cha Alliance for the Republic (APR), kilichoasisiwa mwaka 2008 na Sall.
Faye, aligombea urais kama mgombea binafsi (mgombea huru), baada ya chama chake, African Patriots of Senegal for Work, Ethics and Fraternity (Pastef), kuzuiwa kushiriki uchaguzi mwaka 2024.
Pastef, ni chama kilichoasisiwa Januari 2024 na Sonko. Faye, alishawishiwa na Sonko kujiunga na Pastef. Baada ya Faye kujiunga na Pastef, akiwa mwanasiasa mpya lakini sehemu ya waasisi, alipanda ngazi mpaka kuwa Katibu Mkuu wa chama hicho.
Kampeni siku 10
Faye, mtaalamu wa ukaguzi wa kodi, Aprili 2023, alikamatwa na kuwekwa mahabusu kwa makosa ya kusambaza habari za uongo, kudharau mahakama na kukashifu chombo cha kikatiba kupitia posti yake kwenye mtandao wa kijamii.
Julai 2023, Sonko alitiwa nguvuni kwa makosa ya kujihusisha na ugaidi, vilevile utovu wa maadili. Faye na Sonko, waliachiwa huru Machi 14, 2024. Kutoka Machi 14 mpaka Machi 24, ni siku 10 tu. Hizo ndizo Faye alizitumia kikamilifu kufanya kampeni ambazo zimemwezesha kushinda kiti.
Sonko, Kiongozi wa Pastef na Faye, Katibu Mkuu Pastef, wote walijaza fomu kuwania urais. Januari 20, 2024, Baraza la Kikatiba la Senegal, lilitoa orodha ya jumla ya wagombea urais 2024 waliopitishwa. Jina la Sonko halikujumuishwa. Faye alipitishwa.
Haraka sana baada ya taarifa ya Baraza la Kikatiba Senegal, Sonko bila kuchelewa alitangaza kumuunga mkono Faye. Halafu kwenye kampeni, Sonko aliwahubiriwa Wasenegali: “Bassirou ni mimi, na mimi ni Bassirou.”
Wakati wa kampeni zake, Faye aliahidi kutengeneza ajira nyingi mpya. Vijana wengi Senegal kutokuwa na ajira ni bomu ambalo limemlipukia Sall. Faye aliona upenyo kupitia ukosefu wa ajira kwa vijana, hivyo alichanga karata zake katika eneo hilo.
Faye, kupitia kampeni zake za urais, alijielekeza kwenye mapambano dhidi ya rushwa, vilevile alikula yamini kuwa atahakikisha mikataba ya nishati inapitiwa upya kwa masilahi ya Wasenegali. Faye anaamini kuwa nchi hiyo inanyonywa sana kupitia mikataba ambayo imesainiwa pasipo kuzingatia masilahi ya nchi.
Faye ni nani?
Machi 25 ni tarehe yenye maana kubwa kwa Faye. Alizaliwa Machi 25, 1980. Miaka 44 baadaye, tarehe hiyohiyo inampa maajabu. Matokeo ya ushindi wa Faye kwenye kiti cha urais, yalidhihirika Machi 25, 2024.
Eneo la Ndiaganiao, Jiji la M’Bour, ndipo mahali Faye alizaliwa. Ni Muislam mwenye wake wawili. Kipindi cha kampeni, Faye alikuwa akipanda jukwaani na wake zake wote wawili. Wanawake hao pia walisimama imara kumwombea kura mume wao.
Dhahiri, kama Sonko asingezuiwa kugombea, maana yake Faye asingegombea, badala yake angesimama kumfanyia kampeni kiongozi wake (Sonko). Yupo mtu atatafsiri ushindi wa Faye kuwa sawa na hadithi ya mvua, kwamba haizuiliki. Ikitaka kunyesha inanyesha.
Sonko alizuiwa kugombea ili kupunguza makali ya upinzani wa kisiasa kwenye uchaguzi. Pamoja na jitihada au hila hizo, imeshindikana kutetea kiti, kwa Faye, mbadala wa Sonko, ndiye ametwaa urais. Ni vigumu mno kuzuia mvua.
Yupo mtu yeye atatafsiri ushindi wa Faye kupinga msemo “Mungu akitaka kukupa hakuandikii barua.” Ni namna tu ya kuisoma barua yenyewe. Jinsi Sonko alivyoondolewa katika mbio za urais, ndivyo Mungu alikuwa kwenye uandishi wa barua tajwa.
Huyo ndiye Mungu, unaweza kupambana kumdhibiti mwingine, kumbe ambaye anamtaka ni mwingine. Serikali ya Sall, ilijikita zaidi kumbana Sonko. Kumbe ndivyo walipaswa kutumika ili hatimaye Faye awe rais.
Uchaguzi wa Rais Marekani mwaka 1972, Richard Nixon na mgombea mwenza wake, Spiro Agnew, walicheza faulo mbaya. Walishinda uchaguzi, lakini baadaye kashfa ziliwaandama, wakang’oka. Kumbe walitumika ili Gerald Ford, ambaye hakutaka kugombea urais, awe Rais.
Oktoba 10, 1973, Makamu wa Rais, Spiro Agnew, alijiuzulu kwa kashfa ya rushwa. Rais aliyekuwa madarakani, Richard Nixon, alikuwa Republican, Bunge (Congress) lilitawaliwa na Democrats. Nixon ikabidi afanye mazungumzo na viongozi wa Congress kuhusu uteuzi wa Makamu wa Rais. Congress wakamwambia hakuna mwingine zaidi ya Ford.
Mwaka 1974, Congress walimkuta Nixon na hatia ya kufanya faulo kwenye uchaguzi wa mwaka 1972 uliomrejesha madarakani kwa muhula wa pili. Ni kashfa ya Watergate. Nixon akang'oka madarakani. Makamu wa Rais, Ford akawa Rais.
Lazima kukubali, ipo namna Mungu huamua kujidhihirisha na kufanya mambo yatokee hata kama yalikuwa hayatarajiwi. Ushahidi ni Faye alivyopenya baada ya Sonko kuzibiwa njia.
Vilevile Ford kutoka mjumbe wa Baraza la Wawakilishi, asiye na ndoto ya urais, lakini akawa Makamu wa Rais, kisha Rais.