Mfahamu Bassirou Faye, mfungwa huru aliyeshinda urais Senegal

Bassirou Diomaye Faye 

Muktasari:

  • Faye anakuwa Rais wa tano wa Senegal akitanguliwa na marais wanne ambao ni Leopold Sedar Senghor (1960—1980), Abdou Diouf (1981—2000), Abdoulaye Wade (2000—2012) na Macky Sall aliyeingia madarakani mwaka 2012 hadi sasa.

Jumapili iliyopita, wananchi wa Senegal wamemchagua Bassirou Diomaye Faye kuwa Rais mpya wa nchi hiyo akiwa ni kijana mwenye umri wa miaka 44.

Matokeo rasmi yanatarajiwa kutangazwa mwishoni mwa wiki hii, hata hivyo, tayari Rais anayemaliza muda wake, Macky Sall amempongeza kwa ushindi huo, huku mshindani wake wa karibu, Waziri Mkuu wa zamani, Amadou Ba akikubali kushindwa kwenye duru ya kwanza ya uchaguzi huo

Faye anakuwa Rais wa tano wa Senegal akitanguliwa na marais wanne ambao ni Leopold Sedar Senghor (1960—1980), Abdou Diouf (1981—2000), Abdoulaye Wade (2000—2012) na Macky Sall aliyeingia madarakani mwaka 2012 hadi sasa.

Senghor alipoingia madarakani Septemba 6, 1960, alikuwa na umri wa miaka 54, Diouf alikuwa na miaka 46, Wade alikuwa na miaka 74 na Sall aliingia akiwa na miaka 51. Hii inamfanya Faye kuwa Rais wa Senegal mwenye umri mdogo zaidi kuchaguliwa katika historia ya taifa hilo.

Wachache walisikia habari zake mwaka mmoja uliopita, na sasa ni Rais mteule. Kipindi chake cha kukaa jela kwa miezi kadhaa yeye na mwenzake Ousmane Sonko kiliisha ghafla baada ya kuachiwa huru siku 10 kabla ya uchaguzi mkuu wa nchi hiyo.

Sasa “Bwana Msafi”, kama anavyojulikana kwa jina la utani, ambaye Machi 25 alikuwa akisherehekea siku yake ya kuzaliwa, atalazimika kufanyia kazi mageuzi makubwa aliyoahidi wakati wa kampeni. Wengine wanamwita “mtoza ushuru” kwa sababu aliwahi kufanya kazi katika idara ya kodi nchini humo.

Faye anayakumbuka kwa furaha maisha yake ya kijijini huko Ndiaganiao, ambapo anasema huwa anarudi kila Jumapili kufanya kazi shambani.

“Hajawahi kuwa waziri na hakuwa kiongozi wa serikali, hivyo wakosoaji wanahoji uzoefu wake katika uongozi,” mchambuzi Alioune Tine aliliambia Shirika la Utangazaji la Uingereza (BBC).

“Lakini, kwa mtazamo wa Faye, watu wanaodhaniwa wana uzoefu mkubwa ambao wameendesha nchi tangu mwaka 1960, wameshindwa kwa kiasi kikubwa.”

Kupambana na umaskini, dhuluma na ufisadi ilikuwa ni ajenda kuu ya Faye wakati wote wa kampeni zake. Walipokuwa wakifanya kazi Hazina, yeye na Sonko waliunda jopo lao la kukabiliana na ufisadi.

Sehemu ya ufisadi ambao wao walidai kuwa waliuona ni kwenye nishati. Katika kampeni zake alisema mikataba ya gesi, mafuta, uvuvi na ulinzi lazima yote ijadiliwe ili kuwahudumia vema watu wa Senegal.

Aliahidi kuanzisha kile alichokiita “enzi ya uhuru”. Kuimarisha uhuru wa mahakama na kutengeneza ajira kwa vijana wengi wa Senegal, pia, ni vipaumbele vyake muhimu.

Uchaguzi wa mwisho wa Rais nchini Senegal ulifanyika Februari 24, 2019 na uchaguzi mwingine ulipangwa kufanyika Februari 25, mwaka huu lakini uliahirishwa hadi Jumapili iliyopita, Machi 24.


Historia yake

Faye alizaliwa Jumanne ya Machi 25, huko Ndiaganiao, Senegal. Mwaka 2000 alipata shahada ya uzamili katika sheria na baadaye alijiunga na Chuo cha Taifa cha Utawala (ENA) na kuhitimu mwaka 2004.

Alianza kufanya kazi kama mkaguzi wa kodi katika Idara ya Kodi na Majengo. Akiwa huko alikutana na Sonko na kuwa marafiki. Mwaka 2014, uhusiano wa Faye na Sonko ulikuwa karibu zaidi katika chama cha Muungano wa Kodi na Mashamba kilichoundwa na Sonko ambaye alikuwa kiongozi wa chama cha siasa cha alichokiita Wazalendo wa Kiafrika wa Senegali kwa Kazi, Maadili na Udugu” (PASTEF).

Wakati chama hicho kinaanzishwa, Faye alikuwa kama mgeni rasmi siku ya uzinduzi. Lakini baadaye alipanda haraka sana na kuwa mmoja wa watu mashuhuri sana ndani ya chama hicho, na baadaye akawa mmoja wa watu muhimu waliopanga mikakati ya ushindi kwa Sonko katika uchaguzi mkuu wa mwaka 2019.

Kupitia chama chake cha PASTEF, Sonko alipata karibu asilimia moja ya kura zote zilizopigwa na akashika nafasi ya tatu akitanguliwa na Macky Sall wa chama cha APR, Idrissa Seck wa Rewmi.

Februari 2021, Faye alichaguliwa kuwa katibu mkuu wa PASTEF baada ya Sonko kukamatwa, akituhumiwa kwa ubakaji aliodaiwa kuwa alikuwa akiufanya mara kwa mara.

Kama sehemu ya mkakati wake wa kuishinda serikali, Faye alijaribu kuunganisha upinzani katika uchaguzi wa mwaka 2022, na upinzani huo ulishinda viti 56 chini ya muungano wa Liberate the People.


Kampeni za urais

Baada ya kutokuwa na uhakika juu ya uwezekano wa Sonko kuwa mgombea katika uchaguzi wa urais katika uchaguzi mkuu wa Februari 2024, PASTEF ilimwidhinisha Faye Novemba 2023 kuwa mgombea wake wa kiti cha urais katika uchaguzi huo, licha ya yeye kukamatwa na serikali na kutupwa jela.

Hata hivyo, PASTEF nayo ilikuwa imepigwa marufuku miezi kadhaa iliyokuwa imepita, na hivyo ilimaanisha kuwa iwapo Faye angegombea, basi angefanya hivyo kama mgombea binafsi.

Januari 20, 2024, Baraza la Katiba la Senegal lilichapisha orodha ya mwisho ya wagombea kiti cha urais. Katika orodha hiyo, jina la Sonko halikuonekana pamoja na kwamba kulikuwa na malumbano makali ya kisheria kuhusu suala hilo.

Ugombea wa Faye ulithibitishwa kwa sababu, pamoja na kwamba alikuwa jela, hakuwahi kuhukumiwa na mahakama. Kutokana na sababu hizo na nyingine, Sonko alitangaza haraka kumuunga mkono Faye katika uchaguzi huo.

Machi 15, 2024, ikiwa ni siku moja baada ya Faye kuachiwa huru kutoka jela, alifanya mkutano wa hadhara uliokusanya mamia ya wafuasi wake. Hiyo ilikuwa ndiyo siku alionekana kwa mara ya kwanza tangu atoke jela.

Rais wa zamani wa nchi hiyo, Abdoulaye Wade na chama cha Senegalese Democratic Party (PDS), walimpitisha Faye siku hiyo hiyo kugombea kiti cha Rais, na hivyo kuongeza nafasi yake ya kushinda uchaguzi.

Hatua hiyo ilichukuliwa baada ya mgombea wa PDS ambaye ni mtoto wa Wade, Karim Wade kuenguliwa kuwania kinyang'anyiro hicho kwa sababu alikuwa raia wa nchi mbili wakati alipowasilisha ombi lake la kugombea.

Cheikh Tidiane Dieye, mgombea mwingine katika uchaguzi huo, alijiondoa na kutangaza kumuunga mkono Faye.

Wakati wa kampeni za urais, Faye aliahidi kuwa akichaguliwa kuwa rais wa nchi hiyo atatengeneza ajira. Alifanya kampeni kali dhidi ya ufisadi na kuapa kuangalia upya kandarasi za nishati.


Kukamatwa na kuachiwa

Aprili 14, 2023, Faye alikamatwa alipokuwa akitoka ofisini kwake katika eneo la Rue de Thiong jijini Dakar. Baadaye, aliwekwa chini ya ulinzi wa polisi kwa mashtaka kadhaa yakiwamo ya “kueneza habari za uongo, kudharau mahakama, na kukashifu chombo kilichoundwa” kilichoundwa kihalali na serikali.

Hatua hiyo ilikuja kufuatia chapisho lake aliloandika katika mtandao wa kijamii.

Katika chapishi hilo, alilalamikia udhalimu aliosema umo ndani ya mfumo wa mahakama, akitabiri kwamba hukumu ambayo mahakama ingetoa dhidi ya Sonko ingekuwa ya kumkandamiza Sonko na PASTEF.

Wakati hali ikiendelea, mashtaka ya ziada ya “uchochezi na uasi” na “kutishia usalama wa serikali” yalifunguliwa dhidi yake, na hivyo ikajulikana kuwa angekuwa mahabusu kwa muda usiojulikana.

Baada ya jaribio la Rais anayemaliza muda wake, Macky Sall, Februari, mwaka huu la kuahirisha uchaguzi huo akitaja mizozo ambayo haijatatuliwa kuhusu nani anaweza kugombea, maandamano makubwa yalitokea na Baraza la Katiba likabatilisha uamuzi huo wa Rais Sall wa kuahirishwa kwa uchaguzi huo.

Baada ya maandamano na mashinikizo mengi, hatimaye Rasi Sall alisema kwamba ataachia ofisi Aprili 2, mwaka huu kama ilivyokuwa imepangwa, kisha akaitaja Machi 24 kuwa ndiyo siku ya uchaguzi mkuu wa nchi hiyo.

Maandamano na mashinikizo hayo pia yalimfanya aoneshe nia yake ya kuwaachia huru Faye, Sonko na wafuasi wao wote kama kitendo cha kuonyesha nia njema.

Mwishoni mwa Februari, Serikali ya Sall iliwasilisha muswada wa msamaha ili kutuliza hali ya kijamii na kisiasa ambayo ilikuwa imechafuka kutokana na maandamano na ghasia zilizokuwa zikiendelea.

Mamia kadhaa ya wafungwa wa kisiasa waliachiwa huru na serikali na Machi 14, mwaka huu zikiwa ni siku 10 pekee kabla ya uchaguzi kufanyika, Sonko na Faye waliachiwa huru kutoka gerezani.


Faye katika siasa

Faye anasema anaamini katika mabadiliko ya mfumo na mrengo wa kushoto wa umajumui wa Afrika ili kurudisha mamlaka ya Senegal kwa wananchi, matamshi ambayo baadhi ya wachambuzi wanaamini ni dokezo la nia ya kuitenga nchi hiyo kutoka kwa nchi za Magharibi, hususan mkoloni wao wa zamani, Ufaransa.

Kuhusu mabadiliko ya kikatiba, Faye ameahidi pia kupunguza mamlaka ya urais na kurejesha cheo cha Makamu wa Rais.

Kuhusu ufisadi, Faye ametanguliza vita dhidi ya ufisadi wa kisiasa, akisema: “Hakuna nchi inayoweza kuendelea wakati rushwa na ubadhirifu wa fedha za umma umekithiri.”

Katika kampeni zake, aligusia pia sarafu ya nchi hiyo. Anataka kutekeleza mageuzi ya fedha ili kuimarisha uchumi wa Senegal, kuondoa faranga ya CFA (inayotumika katika nchi nane za Afrika Magharibi).

Katika mpango wake huo, anasema: “Tutafanya mageuzi ya fedha ambayo yataruhusu nchi yetu kuwa na sarafu yake.”

Katika mkutano na waandishi wa habari, aliongeza: “Hakuna uhuru ikiwa hakuna uhuru wa kifedha.”

Baada ya wasiwasi kutoka kwa wawekezaji wa kigeni, aliwatia moyo kwa kauli yake aliyoitoa Machi 2023, akisema “Senegal itatekeleza mageuzi ya faranga ya CFA katika ngazi ya kanda kwanza na kama hilo litashindikana, itazingatia kuanzisha sarafu ya Taifa.”

Nishati ni eneo jingine alilolipa umuhumi. Anaamini katika kuanzisha upya mjadala kuhusu mikataba kati ya serikali na mashirika katika sekta kuanzia nishati na madini hadi uvuvi.

Analenga kuimarisha sifa na uadilifu katika vikosi vya ulinzi na usalama kupitia juhudi za pamoja za kupambana na ufisadi na uzembe.

Mpango huu unalenga kuhakikisha matumizi bora ya rasilimali kwa kutekeleza programu zinazolenga kuongeza ari, motisha, na uangalizi wa maafisa.

Vilevile, aliahidi kuongeza mishahara ya wafanyakazi wa ngazi za chini. Mpango wake unaahidi kudumisha msingi wa vikosi vya wanajeshi wa Senegal kwa kuhimiza kurejea kwenye kanuni za kijeshi na kuwazuia kushiriki katika kisiasa.

Mahakama ambayo amekuwa akiinyooshea kidole wakati wa kampeni zake, Faye anaamini kusiwe na uhusiano kati ya watendaji wa serikali na mahakama, kila mhimili ujitegemee.

Mpango wake unahusisha kuhama kutoka Baraza la Kikatiba hadi Mahakama ya Kikatiba na kuiweka kama kilele cha muundo wa mahakama.

Faye na kiongozi mwenzake wa upinzani, Ousmane Sonko waliachiwa kutoka gerezani huko Dakar siku 10 kabla ya uchaguzi wa nchi hiyo.

Kuachiwa kwao kulifuatia wiki za mzozo baada ya Rais Macky Sall kuahirisha uchaguzi wa urais uliokuwa ufanyike Februari 25 na kwa kiasi kikubwa kulibadilisha kampeni ya urais, huku matamshi yenye nguvu ya Sonko yakiwavutia wapiga kura vijana.

Sonko alikuwa kiini cha mzozo mkali wa miaka miwili na serikali na amekuwa gerezani tangu Julai mwaka jana. Mashtaka dhidi yake na matatizo ya kiuchumi na kijamii, yalisababisha machafuko mabaya kati ya mwaka 2021 na 2023.

Sonko alishika nafasi ya tatu katika uchaguzi wa urais wa mwaka 2019, lakini katika uchaguzi wa mwaka 2024, Sonko alimuidhinisha Faye ambaye pia alikuwa gerezani tangu Aprili 2023, achukue nafasi yake kama mgombea.


Nini mustakabali wa Senegal

Katika bara ambalo limekumbwa na mapinduzi ya kijeshi ya mara kwa mara, Senegal inasimama kama mojawapo ya nchi za Afrika ambazo hazikuwahi kukumbwa na tatizo hili tangu ilipojipatia uhuru wake mwaka 1960.

Hata hivyo, ni muhimu kutambua kwamba utekelezaji wa ahadi zote alizotoa wakati wa kampeni utategemea mazingira ya kisiasa na kiuchumi ya Senegal katika siku zijazo. Kwa hivyo, ingawa Faye ana matumaini makubwa, bado kuna changamoto nyingi zinazomkabili.