Jokate: UWT ndiyo askari wa kumrejesha Samia Ikulu

Muktasari:
- Katibu Mkuu wa UWT Jokate Mwegelo amekabidhiwa barua ya uteuzi wa nafasi hiyo, aomba ushirikiano kwa wanajumuiya hiyo, awaambia wao ndio mainjinia wa kuhakikisha Rais Samia Suluhu Hassan anaibuka kidedea 2025.
Dar es Salaam. Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Umoja wa Wanawake wa Chama cha Mapinduzi (UWT), Jokate Mwegelo amewaambia wanawake wa umoja kuwa wao ndio mainjinia wa kuhakikisha Rais Samia Suluhu Hassan anaibuka kidedea katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2025.
Jokate aliteuliwa Oktoba Mosi, 2023 kushika wadhifa huo na Kamati Kuu ya Halmashauri Kuu ya CCM akichukua nafasi ya Dk Phillis Nyimbi ameeleza hayo leo Jumatano Oktoba 4, 2023 wakati akizungumza na wana UWT kutoka mikoa ya Dar es Salaam na Pwani.
Katibu mkuu huyo wa UWT, aliyewahi kuwa Mkuu wa Wilaya za Kisarawe, Temeke na Korogwe mkoani Pwani, amewataka pia wanawake wa UWT kuwa mstari wa mbele kuhakikisha wanajitokeza katika ushiriki wa chaguzi za Serikali za Mitaa, vitongoji na vijiji.
"Hakuna mwingine wa kufanya kazi hii ni sisi jeshi la Mama (Rais Samia). Jeshi la Mama mpo? akiitikiwa na kina mama wa UWT tupo..." amesema Jokate muda mfupi baada ya kuchukua barua ya uteuzi wa nafasi hiyo katika ofisi ndogo za CCM Lumumba jijini hapa.
Katika hatua nyingine, Jokate ameomba ushirikiano kwa wana UWT katika utekelezaji wa majukumu yake mapya huku akiwashurukuru viongozi wa CCM wakiongozwa na mwenyekiti wao Rais Samia kwa kumchagua katika nafasi hiyo.
"Unaweza kuwa kiongozi mzuri lakini ukikosa ushirikiano ni kazi bure, lakini sina shaka kwa sababu nimepata bahati ya kuingia kwenye UWT ikiwa na viongozi wake shupavu na wachapakazi. Kuanzia mwenyekiti ( Mary Chatanda) na makamu wake Zainabu Shomary wanachanja mbuga.
"Kazi yangu itakuwa nyepesi... naingia kwenye jumuiya iliyojipambanua, iliyojipanga na kujidhatiti katika utekelezaji wa majukumu yake. UWT ndio askari tutakaokuwa mstari wa mbele katika chaguzi zijazo tutakazo mheshimisha Rais Samia," amesema Jokate.
Naibu Katibu Mkuu Taifa wa UWT, Riziki Kingwande amewashukuru wote waliojitokeza kuja kumpokea Jokate katika hafla fupi iliyofanyika katika ofisi za CCM za Mkoa wa Dar es Salaam.
Mjumbe wa Kamati ya Utekelezaji Taifa wa UWT, Mariam Ulega amesema kwa niaba ya wenzake wanaishukuru Kamati Kuu ya CCM kwa uteuzi wa Jokate. Amesema wanawake wamefarijika na uteuzi wa Jokate kuwa Katibu Mkuu wa UWT.
"Karibu wiki moja sasa umekuwa ukisambaa kwenye makundi ya mitandao ya kijamii kuhusu uteuzi wako watu wa rika zote wamefurahia uteuzi wako. Tuna imani kubwa sana na wewe kutokana na utendaji kazi wako katika nafasi mbalimbali ulizohudumu," amesema Mariamu.
Mjumbe wa Baraza Kuu la UWT, Neema Lugangira amesema, " tuna imani kubwa na ubunifu wako na namna utakavyoipeleka mbele UWT .
"Tunakuahidi tutakupa ushirikiano mkubwa kama wajumbe wa baraza na wabunge wanawake, tutakuwa na wewe bega kwa bega," amesema Lugangira ambaye ni Mbunge wa Viti Maalumu Mkoa wa Kagera.