Jokate azungumzumzia uteuzi wake, awataja vijana

Mkuu wa Wilaya ya Korogwe, Jokate Mwegelo akizungumza wakati wa mahojiano maalumu na waandishi wa kampuni ya Mwananchi Communications Limited (MCL) ofisini kwake. Picha na Elizabeth Edward
Muktasari:
- Jokate azungumzia uteuzi wake na hamasa iliyotengenezwa kwa vijana, aeleza alivyojipanga kushirikiana na wadau bila kujali tofauti za kiitikadi.
Dar es Salaam. Siku moja baada ya kuteuliwa kuwa Katibu Mkuu wa Umoja wa Wanawake (UWT), Jokate Mwegelo ametumia ukurasa wake wa Instagram kueleza namna uteuzi huo ulivyoamsha chachu ya mabinti kupambania ndoto zao kwenye siasa.
Jokate ambaye kabla ya uteuzi huo alikuwa Mkuu wa Wilaya ya Korogwe amesema vijana sasa wanaamini kwamba upo uwezekano wa wao kuaminiwa katika nafasi kubwa.
Kupitia ujumbe wake alioweka kwenye mtandao huo asubuhi ya leo ameandika, “Ni heshima kubwa kwa chama changu kikiendelea kutuamini vijana na kutupa majukumu makubwa ya kukitumikia chama na Taifa.
“Naamini uteuzi huu utakuwa chachu kuona mabinti wadogo chipukizi wa chama kupambania ndoto zao wakiamini chama kinawajali na kuwaamini watu wote wenye uwezo na dhamira ya kweli ya kuleta mageuzi ya kweli na maendeleo ya chama na Taifa letu.”
Pamoja na hayo ameeleza namna ambavyo binafsi ameguswa na uteuzi huo ambao unamuweka katika ngazi ya juu kisiasa.
Amesema uteuzi huo unampa nafasi ya kujiweka tayari kushirikiana na viongozi na wanachama wa UWT nchini kwa uadilifu, ueledi, ubunifu, ustadi, uzalendo na umakini kwa kutanguliza masilahi ya chama na Taifa.
Sambamba na hilo ameahidi kushirikiana na wadau wote wanaopigania maendeleo na ustawi wanawake bila kujali tofauti za itikadi za vyama, dini, utaifa na ukabila.