Prime
Uteuzi wa Jokate waibua damu changa UWT

Dar es Salaam. Uteuzi wa Jokate Mwegelo kuwa Katibu Mkuu wa Umoja wa Wanawake Tanzania (UWT), umetajwa kuibua damu changa ndani ya jumuiya hiyo.
Hilo linatokana na ukweli kwamba, Jokate ndiye anayeonekana kuwa Katibu Mkuu kijana zaidi kuteuliwa katika wadhifa huo alioukwaa akiwa na miaka 36.
Kauli kuhusu ingizo hilo la vijana, imeibuliwa na wasomi, kutokana na Kamati Kuu ya Halmashauri Kuu ya CCM kumteua Jokate Mwegelo kuwa Katibu Mkuu wa UWT.
Kulingana na taarifa iliyotiwa saini na Katibu wa NEC ya CCM, Itikadi na Uenezi, Sophia Mjema, pamoja na Jokate mwingine aliyeteuliwa ni Raphael Lulandala kuwa Katibu Mkuu wa Umoja wa Vijana wa CCM (UVCCM).
Damu changa
Akizungumzia uteuzi huo jana, Mhadhiri wa Sayansi ya Siasa kutoka Chuo Kikuu Huria cha Tanzania (OUT), Dk Revocatus Kabobe alisema kiongozi huyo umeibua damu changa ndani ya jumuiya hiyo.
Hata hivyo, alisema kilichofanyika ni ishara ya umakini wa chama husika kwa kuwa chama makini lazima kitumie vijana wenye uwezo wa kukijenga.
Ingizo hilo la vijana alilitafsiri kama kete muhimu kwa CCM kutumia jumuiya yake ya UWT kujipanga vizuri zaidi kwenye chaguzi zijazo.
"Kumbuka takwimu za uchaguzi zimeonyesha kuwa wanawake ndiyo kundi kubwa hapa nchini na wanaongoza kupiga kura ukilinganisha na makundi mengine. Kwa ufupi naweza kusema ukifanikiwa kushawishi wanawake kisiasa tayari unakuwa umeweka mtaji mkubwa sana.
"Jokate ni kijana mwenye uwezo ana anaushawishi kwa vijana achilia mbali wanawake ambako nako pia anaweza," alisema.
Kuhusu uwezo wake, alisema ni chaguo sahihi kwa Jumuiya hiyo na CCM kwa ujumla.
"Kwa kipindi ambacho amekuwa Mkuu wa Wilaya ameonyesha ukaribu wake na jamii hasa ya wanawake na jamii hiyo imemkubali sana," alisema.
Alisema anachopaswa kufanya ni kujipanga kukabiliana na wapinzani wake kutoka vyama vingine.
"Kwa mtazamo wangu haitakuwa rahisi maana najua vyama pinzani navyo mara nyingi vimekuwa vikiteua kujibu mapigo kitu ambacho kisiasa ni kizuri," alisema.
Wadau washauri
Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Mtakatifu Agustino (Saut), Dk Kanaeli Kaale alisema uteuzi na kupanda ngazi kwa Jokate katika nafasi mbalimbali ni ujumbe kwa vijana wasomi na makada wa vyama vya siasa kuwa utendaji, uwajibikaji, kujituma, kujifunza na nidhamu kazini ni siri kufikia malengo na mafanikio katika nyanja zote.
"Baadhi ya vijana wasomi na makada wanajibweteka walidhani usomi na ukada unatosha.....hapana! Pamoja na vyote, watu hupimwa kwa utendaji na nidhamu yao kazini," alisema Kaale ambaye pia ni mwandishi wa habari kitaaluma.
Alisema akiwa Kisarawe, Jokate alidhihirisha uwezo wake katika kusimamia masuala ya msingi ikiwemo la elimu kwa watoto wa kike na hata alivyohamishiwa Korogwe alionyesha njia kwa kuhamasisha maendeleo, hasa kupitia vikundi vya ujasiriamali vya wanawake na vijana.
Edwin Soko, mchambuzi wa masuala ya kisiasa aliunga mkono hoja hiyo huku akionya kuwa safari hii, Jokate anakabiliwa na mtihani mgumu wa kuonyesha uwezo wake kiutendaji na kiuongozi kutokana na siasa za ndani na nje ya Jumuiya za vyama vya siasa.
"Jumuiya za UWT na UVCCM ni injini za CCM katika harakati za siasa kutokana na wingi wa wanachama wake....macho siyo tu ya CCM kama taasisi, bali pia hata makada wenye nia ya kuwania nafasi za uongozi yako kwa UWT na UVCCM," alisema Soko
Alisema ugumu wa jukumu linalomkabili Jokate na mwezake unaongezwa na chaguzi zijazo za Serikali ya Mitaa mwaka 2014 na uchaguzi mkuu wa mwaka 2025.
Kauli ya Lulandala
Akizungumza na Mwananchi, baada ya kuteuliwa Lulandala, alisema yupo tayari kwa weledi na nguvu zote kuitumikia nafasi hiyo kwa manufaa ya wananchi.
Aliishukuru Kamati Kuu kwa kumteua akibainisha kuwa Chama cha Mapinduzi (CCM) kinao watu wengi wenye uwezo, weledi ndani na nje ya Tanzania, hivyo anaenda kufanya kile wanachotarajia chini ya mwenyekiti, Rais Samia Suluhu Hassan.
“Sijaongea na chombo chochote cha habari zaidi ya Mwananchi, hii ni furaha kubwa kwangu kuteuliwa nafasi hii kubwa na ya juu, nimshukuru Rais Samia na nimeipokea uteuzi huu kwa unyenyekevu, heshima na nidhamu,”
“Naishukuru kamati kuu kuridhia mapendekezo kuniona nafaa na kustahili kuwa katika nafasi hii kwani CCM inao watu wengi sana ndani na nje, matarajio yangu ni kufikia kile wanachotarajia,” alisema
Akizungumzia uteuzi huo, mmoja wa wakazi wa Wilaya ya Momba, Atupaswile Mwaigomola alisema uteuzi wa Lulandala ni matokeo ya alichokifanya akiwa Mkuu wa Wilaya kwa kuwa muda mwingi aliutumia kusikiliza na kutatua matatizo ya wananchi.
“Zaidi namkumbuka kwenye masuala ya kilimo na miundombinu, lakini mfuatiliaji kwenye miradi ya maendeleo hakuwa mtu wa kukaa ofisini na aliwaunganisha wananchi ilipotokea migogoro,” alisema Atupaswile.
Naye Juma Ikolo, alisema Lulandala alikuwa kiongozi mchapakazi na kiungo kwa wananchi katika kusikiliza na kutatua kero mbalimbali na kwamba wanaamini nafasi aliyokabidhiwa ataimudu.
“Kwakuwa Momba ni wilaya ilipo maeneo ya vijijini na ameona changamoto zilizopo, haitampa wakati mgumu nafasi aliyopewa, alikuwa kiongozi ambaye alisikiliza kabla ya kuamua,” alisema Ikolo mkazi wa Momba.
Siasa za UWT, UVCCM
Jokate na wenzake wanakabidhiwa dhamana ya kuwa watendaji wakuu ndani ya Jumuiya za UWT na UVCCM wakati kukiwa kumesalia muda mfupi Taifa kuingia kwenye chaguzi muhimu kuanzia Serikali za Mitaa na Uchaguzi Mkuu wa 2025.
Ingawa haitarajiwi hali na nguvu ya Jumuiya hizo kurejea zilipokuwa kabla na miaka ya mwanzoni mwa tisini, bado macho ya viongozi wa CCM yapo kwa viongozi na wanachama wa Jumuiya hizo zinapowadia nyakati za uchunguzi.
Wakati vijana kupitia UVCCM wanategemewa kwenye harakati na shughuli za kisiasa ikiwemo kampeni zinazohitaji matumizi ya nguvu, wanawake kupitia UWT wanalengwa siyo tu kwa wingi wao bali pia utiifu wao kwa chama licha ya mawimbi ya kisiasa na kiuchumi wanayokumbana nayo.
Uimara wa UWT na UVCCM kipindi cha nyuma kiliwalazimisha makada wa CCM wenye nia ya kuwania nafasi za uongozi ndani na nje ya chama kutafuta uugwaji mkono kutoka kwa viongozi na wanachama wa Jumuiya hizo kabla na hata baada ya chaguzi.
Miongoni mwa viongozi waliovuma na kupata umaarufu wakati wakiongoza Jumuiya hizo ni pamoja na Dk Emmanuel Nchimbi aliyekuwa Mwenyekiti wa UVCCM, Anna Abdallah na Sophia Simba waliokuwa wenyeviti wa UWT kwa nyakati tofauti.
Harakati za Jokate, Lulandala
Safari za Jokate na Lulandala si za kubahatisha kwa kuwa zimeanza muda mrefu.
Wateule wote wawili hajawa na safari fupi katika harakati za kisiasa ambapo safari ya Jokate ndani ya CCM ilianza mwaka 2017 alipoteuliwa kuongoza Idara ya Uhamasishaji ya UVCCM akiwa na wadhifa wa katibu wa kamati.
Mwaka mmoja baadaye, nyota ya mlimbwende huyo iliendelea kung'aa kwa aliyekuwa Rais wa awamu ya tano Hayati John Magufuli kumteuwa kuwa Mkuu wa Wilaya ya Kisarawe mkoani Pwani alikosimamia kwa juhudi haki sawa ya elimu kwa watoto wa kike na kiume.
Baadaye alihamishwa kituo cha kazi kwa kuteuliwa kuwa Mkuu wa Mkoa Wilaya ya Temeke jijini Dar es Salaam, kabla ya kupelekwa Korogwe mkoani Tanga kwa wadhifa huo hadi alipoteuliwa Jana kuwa mtendaji mkuu wa UWT
Katika eneo la ulimbwende, Jokate alishiriki na kushika nafasi ya pili katika mashindano ya kumsaka mlimbwende wa Tanzania mwaka 2006.
Ushiriki wa mashindano ya ulimwende ulimfungulia njia katika shughuli mbalimbali ikiwemo a sanaa ya muziki na uigizaji.
Kwa upande wake, historia ya safari ya kisiasa ya Lulandala inahudisha harakati na siasa za vyama vya upinzani ikiwemo kuwa miongoni mwa makada na viongozi waandamizi wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) Mkoa wa Njombe.
Mwaka 2015, Lulandala alikuwa Mwenyekiti wa Chadema Mkoa wa Njombe ambako pia amewahi kuwania kiti cha ubunge jimbo la Njombe Kusini kupitia tiketi ya chama hicho kikuu cha upinzani.
Wakati wimbi la wanachama na viongozi wa vyama vya upinzani kuhamia CCM lililobatizwa jina la kuunga mkono juhudi za aliyekuwa Rais wa awamu ya tano, Hayati John Magufuli, Lulandala alikuwa miongoni mwa makada wa Chadema aliojiunga CCM kabla ya kukwaa uteuzi wa kuwa DC na sasa kupewa uongozi wa juu wa Jumuiya ya UVCCM