Kadi za kielekroniki za CCM kutumika kama ATM

Muktasari:

  • Chama Cha Mapinduzi (CCM) kimesema kadi za kielekroniki za chama hicho zitaweza kutumika kama kadi ya kufanyia miamala ya fedha (ATM).

Iringa. Katibu wa Oganaizesheni wa CCM, Issa Haji Gavi amesema kadi za uanachama za chama hicho zitaweza kutumika kwa huduma nyingine ikiwamo kufanya miamala ya kifedha.

 Amesema mbali na miamala ya fedha, kwa wanaotumia huduma za Bima ya Afya wataweza kuitumia kadi hiyo pamoja na wanachama wa Mfuko wa Hifadhi ya Jamii (NSSF).

Akizungumza katika kikao cha balozi shina namba saba, katika Kijiji cha Ilambilole, Jimbo la Isimani, Gavi amesema huduma hizo ndizo zilizosababisha kuchelewa kwa kadi hizo.

"Mabadiliko ya kimfumo ndiyo yamesababisha zichelewe, tulikuwa tunafanya mabadiliko ya kimfumo ili tupate kadi zenye sifa. Kuanzia mwezi wa nane kila mtu atakuwa na kadi," amesema Gavu.

Amewataka wanachama wa chama hicho kuendelea kuiunga mkono CCM kwa kuhakikisha inashinda chaguzi zote zijazo.

Awali baadhi ya wanachama walilalamika kukosa kazi za kielektroniki licha ya kujisajili.

"Kati ya wanachama wote wa shina letu 42,  ni nane tu ndio wanazo kadi," amesema Helena Kiliwa, ambaye ni mkazi wa Kihorogota.

Awali, Katibu wa Siasa, Itikadi na Uenezi, Sophia Mjema alisema wanaendelea kusimamia na kuhakikisha yale yaliyoahidiwa yanatekelezwa.