CCM ijipime nguvu kwa wanaoikimbiza

Mwenyekiti wa CCM, Rais Samia Suluhu Hassan akipokea mfano wa kadi ya uanachama wa chama hicho kutoka kwa Katibu Mkuu, Daniel Chongolo wakati wa uzinduzi wa kadi hizouliokwenda sambamba na maadhimisho ya miaka 45 ya CCM yaliyofanyika mkoani Mara. Picha na maktaba

Muktasari:

Mwaka 1995 katika Mkutano Mkuu wa CCM, Baba wa Taifa Julius Nyerere alisema bila CCM, imara nchi itayumba kwa kuwa Watanzania wanataka mabadiliko na wasipoyaona au kuyapata ndani ya CCM watayatafuta nje ya chama hicho.


Mwanza. Mwaka 1995 katika Mkutano Mkuu wa CCM, Baba wa Taifa Julius Nyerere alisema bila CCM, imara nchi itayumba kwa kuwa Watanzania wanataka mabadiliko na wasipoyaona au kuyapata ndani ya CCM watayatafuta nje ya chama hicho.

Wakati huo Mwalimu Nyerere akitoa kauli hiyo vyama vya upinzani vilikuwa na miaka mitatu tangu vianzishwe. tangu wakati huo mpaka sasa vyama hivyo vimechagiza ukuaji wa demokrasia na kutoa upinzani mkali kwa CCM ambao kwa namna moja au nyingine umekimarisha chama hicho kikongwe.

Usijisifu kwa kuwa na mbio bali msifu pia anayekukimbiza! ndivyo unavyoweza kusema baada ya Chama cha Mapinduzi (CCM), kutambulisha kadi za kieletroniki wakiingia kwenye uendeshaji wa chama kwa njia za kisasa.

CCM kimetimiza miaka 45 kikiwa madarakani, si miaka michache lakini kinapojisifia kwa uimara wake ni lazima kiangalie na wanaokikimbiza mpaka kikapata mafanikio iliyonayo hivi sasa.

Mfumo wa vyama vingi vya siasa uliorejea nchini mwaka 1992 na mwaka 1995 kushuhudiwa uchaguzi mkuu wa kwanza uliohusisha vyama vingi umechangia kuimarika kwa chama tawala.

CCM haiwezi kuwa imara kama vyama vya upinzani si imra kwakuwa vyenyewe ndivyo huonyesha udhaifu wa chama tawala kwa wananchi ili navyo vipate uungwaji mkono

Tayari baadhi ya vyama vya upinzani viliaanza kuingia katika matumizi ya teknolojia ya kisasa kwenye uendeshaji wake. Ni zama za kidijitali hivyo vyama vya siasa hapa nchini haviwezi kukwepa matumizi ya mifumo ya kisasa ambayo si tu inaboresha shughuli zao lakini pia inawapa fursa ya kutambulika zaidi nje ya mipaka ya Tanzania.

Vyama hivyo hivi sasa vinaona fursa ya kusajili wanachama, kupokea michango ya wanachama, kutunza kumbukumbu, kutoa kadi za kieletroniki na kutoa taarifa mbalimbali kuhusu maendeleo, programu na mikutano ya chama husika.

Kimsingi vyama vya siasa zinaweza kutumia mifumo ya kisasa kujiendesha kupitia ada na michango mbalimbali inayotolewa na wanachama, marafiki, wafadhili na wahisani.

Mifumo ya kieletroniki ni njia mojawapo wa kudhibiti ubadhirifu, ukosefu wa taarifa sahihi za wanachama na uhifadhi hafifu wa nyaraka za chama.


Chama cha Mapinduzi

Chama Cha Mapinduzi (CCM) kimezindua kadi mpya za wananchama za kielektroniki ambazo siyo tu zitakuwa na taarifa zote muhimu za mwanachama, bali pia zitawawezesha kutambukilika na kupata huduma za kifedha.

Uzindizi huo umefanyika mjini Musoma Februari 5 ikiwa ni sehemu ya maadhimisho ya miaka 45 ya kuzaliwa kwa chama hicho tawala zilizofanyika kitaifa mkoani Mara.

CCM imezindua kadi hizo ikiwa imepita miaka 45 tangu chama hicho tawala kiundwa Februari 5, 1977 baada ya kuungana kwa vyama vya ukombozi vya Tanu (Tanganyika) na Afro Shirazi kwa upande wa Zanzibar.

Mwenyekiti wa Taifa wa CCM ambaye pia Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan andiye aliyezindua kadi hizo huku akikabidhiwa kadi ya kwanza na Katibu Mkuu wake, Daniel Chongolo.

Kwa mujibu wa Chongolo, hadi kufikia siku hiyo ya uzinduzi, zaidi ya wanachama 2.07 milioni wa CCM walikuwa wamesajiliwa kielektroniki.


Wanachama wote kielektroniki 2027

Akizungumzia mikakati ya chama hicho ya kufanya shughuli zake kidijitali, Chongolo ameujulisha umma kuwa ifikapo Februari 5, 2027, wanachama wote wa CCM aliosema wanafikia zaidi ya 12 milioni watakuwa wamesajiliwa kielektroniki.

Chongolo anasema uamuzi huo ni utekelezaji wa kifungu cha 181 (c) cha mwelekeo wa Sera za CCM katika kipindi cha miaka 10 kuanzia mwaka 2020 hadi 2030.

Akikinukuu kifungu hicho, Katibu mkuu huyo anasema; “Katika kipindi cha kuelekea CCM kufikisha miaka 50; chama na jumuiya zake kitahakikisha wanachama wote wa CCM wanakuwa na kadi za kielektroniki na mfumo mzuri wa Tehama wa kuwatambua popote walipo,”

Ili kufikia lengo hilo, Chongolo amewataka watendaji wote wa CCM na Jumuiya zake kutimiza wajibu wao kufanikisha lengo hilo huku akifichua kwamba usajili wa wanachama kielektroniki utakuwa kati ya vipimo na vigezo vya kiutendaji kwa watendaji hao.

“Napenda kutoa wito kwa watendaji wote wa CCM na jumuiya zake wa ngazi zote, kufanya kazi kwa uwezo wao wote kufanikisha jambo hili na watambue mojawapo ya kipimo cha utendaji wetu, nikiwemo mimi mwenyewe ni kuhakikisham kazi hii inakamilika kwa asilimia 100 kwa kipindi ambacho kimewekwa na mwongozo na sera yetu ya miaka 10,” alisema Chongolo

Katibu Mkuu huyo amefichua kwamba kurejeshwa kwa utaratibu wa matembezi ya mshikamano miongoni mwa wana CCM utakaoambatana na kazi kusajili wanachama ni mkakati wa kufanikisha usajili wa wanachama wote kielektroniki ifikapo mwaka 2027.


Chadema na ACT

Wakati CCM ikizindua kadi za kielektroniki mwaka huu, Chama Cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) kilizindua operesheni ya kusajili wanachama wake kielektroniki tangu Mei, 2021.

Pamoja na kuwatambua wanachama wake, chama hicho kikuu cha upinzani kinalenga kutumia operesheni hiyo kujenga na kuongeza uwezo wa kujitegemea kiuchumi kupitia michango ya hiari ya wanachama.

Kwa mujibu wa Mwenyekiti wa Taifa wa chama hicho, Freeman Mbowe alisema kufanikiwa kwa mpango huo kutaiondolea chama hicho utegemezi wa ruzuku kutoka Serikali inayotolewa kupitia Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa kulingana na uwakilishi kwenye halmashauri na bungeni.

Akizungumza wakati wa uzinduzi wa opareshini hiyo uliofanyika katika makao makao makuu ya Chadema Kanda ya Kaskazini jijini Arusha, Mbowe alisema operesheni hiyo iliyopewa jina la “Operesheni Haki” unalenga kukirejesha chama hicho kwa wananchi.

Kutokana na zuio la mikutano ya hadhara ya kisiasa, Chadema kiantekeleza operesheni hiyo nchi nzima kupitia vikao na mikutano ya ndani.

Opareseheni hiyo ya Chadema ya kidijitali yenye kauli mbiu ya “Tunakwenda Kidijitali” itahusisha kuandikisha upya wanachama na kupewa kadi za kielekroniki, ambazo ziko katika makundi matano kulingana na kiwango cha pesa kitakachotolewa na wanachama.

Chama cha ACT-Wazalendo nacho tayari kimezindua kampeni ya kujiendesha kidijitali ikiwemo uandikishaji wa wanachama.

Kupitia taarifa yake kwa umma Januari 24, Katibu Mkuu wa chama hicho, Ado Shaibu anasema mfumo huo siyo tu utarahisisha uendeshaji, bali pia uwezo wa kiuchumi wa chama.

Siku chache zilizopita kiongozi wa ACT-Wazalendo, Zitto Kabwe aliwaambia wahariri na waandishi wa habari kuwa mfumo huo wa kidijitali utakwenda kuondoa utegemezi wa ruzuku ya Serikali hivyo chama kitakuwa na uwezo wa kujiendesha kupitia malipo ya ada na huduma mbalimbali

Wadau wasifu

Wakizungumzia vyama vya siasa kuanza kujiendesha kidijitali, wadau na wachambuzi wa masuala ya kisiasa Edwin Soko na Dk Onesmo Kyauke walisema mfumo wa kidijitali utakuwa na faida nyingi kwa vyama kisiasa na kiuchumi pia.

Soko ambaye pia ni Mwenyekiti wa Klabu ya Waandishi wa Habari Mkoa wa Mwanza, anasema vyama hivyo vitaweza kufahamu wanachama hai na wafu wakati wa maandalizi ya chaguzi mbalimbali.

“Tanzania tunaelekea kwenye chaguzi za kielektroniki, vyama kuingia kwenye mfumo huo ni maandalizi ya kutosha kufikia chaguzi za kisasa za kielektroniki katika kipindi hiki tunachoelekea uchaguzi mkuu wa mwaka 2025. Hata kama hatutakuwa na uchaguzi wa kidijitali 2025, haya ni maandalizi mazuri kwa vyama,” anasema Soko

Licha ya kupongeza vyama ambavyo tayari vimeanza kujiendesha kidijitali, Dk Kyauke anasema mfumo huo utakinufaisha zaidi CCM kutakana na urahisi wa kuwaandikisha wanachama wake kupitia mtandao wake ulioenea hadi ngazi ya vitongoji na vijiji.

“Itakuwa rahisi kwa vyama kujua idadi ya wanachama wake, wako wapi na wana uwezo gani kiuchumi; changamoto kubwa inaweza kuwa maeneo ya vijijini ambako wanachama wengi ni wazee au hawana simu za viganjani vinavyoruhusu mawasiliano ya mfumo wa kidijitali,” anasema Dk Kyauke

Anasema mfumo wa kidijitali katika shughuli za kisiasa utaleta mapinduzi makubwa katika harakati za kisiasa nchini