Kama Pau Gekule, fyatua na wenzake chapchap

Kufyatuliwa kwa Madame Gekule kuna somo kubwa. Kwanza, ni mara ya kwanza maza kufyatua mnene chapchap. Huu ni utaratibu mpya wa kifyatu, japo wa kuchanganya kidogo, kama utakuwa endelevu, unaweza kuwaonya mafyatu mibaka na mijizi wa njuluku za mafyatu wanaoendelea kusikinishwa na mafyatu wanene.

Pili, kama siyo gea, sitaki niseme kanyabwoya, hata kama ni hivyo, ya kuonyesha mafyatu kuwa wanene sasa wanajali ili wawafyatue kwenye uchafuzi, sorry, uchakachuaji, sorry, uchaguaji ujao, basi kuna namna.

Sitaki niamini hizi ni kamba na maigizo hasa usawa huu maza anapotaka kunyaka kula ya kura kulhali hata kwa kutumia mishite kuondoa dhana kuwa kama siyo mkono wa God, asingekuwa mnene wa kaya. Haya kila la heri japo kuna shari.

Tatu, je, huu ni utamaduni mpya wa uwajibikaji na uwajibishaji wa mafyatu watumiao ulaji kimiungu ilhali ni mafyatu tena wengine vihiyo/vilaza au kuna namna tunafyatuliwa?

Nne, kama kweli. Kama amefyatua, lazima afyatuliwe. Je, alimfyatua yule fyatu au la? Mandata watatueleza. Je, huu ndiyo mwisho au mwanzo wa sekeseke hili? Inakuwaje Gekule afyatuliwe kisiasa na aendelee kusepa bila kunyakwa kisharia na kusweka lupango kama watuhumiwa wengine tena wa makosa makubwa kama haya ambao si wanene?

Je, sheria zetu zinagwaya au kuwapendelea wanene huku zikiwaumiza na kuwakandamiza wadogo? Sitaki kwenda huko wala kufikia hitimisho hili mbali na kuamini. Hivyo, nategemea kumuona bibie mbele ya pilato aidha akipozwa lupango au kupewa dhamana.

Tano, kwenye mahakama ya kisiasa, hakuna mwenendo wa mashtaka (procedure) bali kufyatua au kutofyatua kulingana na masilahi ya wahusika. Pia, kunaweza kuwapo kulindana hata kuoneana kwani ni vurugu mechi.

Sita, kama kuna utashi wa kisiasa, kunaweza kuwa uwanja mzuri wa kutenda au kutotenda haki. Sijui kilichotokea kwa madame Gekule ni kipi kati ya viwili hivi. Siwezi kusema ni kutenda au kutotenda haki. Kwa sababu hatujajua ukweli wote mbali na kuanza kushuku kwa nini Gekule pekee wakati watuhumiwa wa makosa tena makubwa tu wapo na hawashughulikiwi.

Saba, swali kubwa, muhimu lisilokwepeka, kwa nini fyatu mmoja aliyetuhumiwa kumfyatua mwenzake tena kwa ugomvi wa biashara na mambo binafsi ashughulikiwe haraka kuliko watuhumiwa wanaofyatua jamii nzima ya mafyatu? Hapa tatizo ni mfyatuzi au mfyatuliwa au nijengavyo ufyatuaji huu wa kinamna?

Nane, katika sheshe hili, najawa na maswali kibao ya kifyatuaji ninayoelekeza kwa maza mwenyewe yanayotaka majibu sahihi bila kuzungusha wala kupoteza muda. Imekuwaje kumfyatua Gekule kabla uchunguzi ukamilike?

Inakuwaje siyo watuhumiwa wa mishiko mikubwa, Mwehujuu Michembe, Januwari son of Ma-rope mgoshi, Mahame Kinyaa Mbawala n.k. aliowatuhumu Luhanga Mpini? Je, kuna wateule kayani wanaopaswa kufyatuliwa chapchap huku wengine wakifumbiwa macho?

Tisa, inakuwaje fyatu aliyemfyatua fyatu binafsi, tena kwa imani za kifyatu, afyatuliwe wanguwangu wakati wanaotuhumiwa kufyatua matrilioni yanayosababisha matatizo kwa mafyatu wengi waachwe wakiendelea kufyatua huku wengine wakibadilishwa mawizara? Ala!


Kumi, imekuwaje maza amemfyatua Gekule anayetuhumiwa kumfyatua fyatu mmoja wakati hajawafyatua mafyatua wanene waliotuhumiwa kuiba matrilioni, jambo ambalo linaumiza na linadhalilisha mafyatu kibao? Je, ni yale ya kuwafyatua vibaka huku mibaka ikiengwaengwa na kuendelea kufyatua na kusababisha umaskini kwa mafyatu walio wengi?

Kumi, ngoja tujiulize maswali mengi ya kifyatuzi huenda wahusika wakatupa majibu tena yenye mashiko au kuchukua hatua mujarabu kwa haki na usawa bila ubaguzi wala upendeleo. Ni wagonjwa wangapi wanakosa huduma, wanafunzi wangapi wanakosa elimu, makapuku wangapi wanatengenezwa kutokana na ufyatuaji huu?

Kumi na mosi, je, maza ametumia vigezo na usongo gani kumfyatua Gekule na kuwakumbatia hawa mafyatu wanaotuhumiwa kuuibia umma wa mafyatu?

Kumi na bee, kwa vile ngoma na sheshe bado vibichi, naomba leo, niulize maswali haya madogo na kidogo nikiacha makubwa na mengi waulize mafyatu wenyewe huku nikingoja kuona wahusika watenda haki vipi na kwa kasi ipi kwa watuhumiwa wote, hasa niliowataja hapa ambao, hata hivyo, walitajwa na mafyatu wenzao wanene tena kwenye chata lao la ulaji.

Kumbe namuota maza!