Kamati Kuu NLD yaja na maazimio manane
Katibu Mkuu wa Chama cha National League for Democracy (NLD), Doyo Hassan Doyo (katikati) akiongoza kikao cha Kamati Kuu ya chama hicho leo Jumatano Jalai 1, 2026, Buguruni jijini Dar es Salaam.
Muktasari:
- Kamati Kuu ya Chama cha National League for Democracy (NLD) ilifanya kikao chake cha kawaida cha siku mbili kuanzia Julai 1 hadi 2, 2026 jijini Dar es Salaam, ambacho kimepitisha maazimio manane yanayolenga kuimarisha chama, uongozi na uchumi wake.
Dar es Salaam. Kamati Kuu ya Chama cha National League for Democracy (NLD) imehitimisha kikao chake cha siku mbili, Julai 1 hadi 2, 2026 jijini Dar es Salaam na kupitisha maazimio manane yanayogusa mustakabali wa chama hicho kisiasa, kiutawala na kiuchumi.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Katibu Mkuu wa NLD, Doyo Hassan Doyo, kikao hicho kimejadili hali ya kisiasa nchini, tathmini ya uchaguzi mkuu wa 2025 pamoja na mikakati ya muda mfupi na muda mrefu ya kukijenga chama.
Katika Azimio la kwanza, Kamati Kuu imeamua kuunda timu ya tathmini ya uchaguzi ndani ya siku 14 ili kuchambua matokeo ya uchaguzi wa Rais, wabunge na madiwani, pamoja na kuboresha mikakati ya kampeni.
Pia, viongozi wakuu watafanya ziara nchi nzima kuwashukuru wananchi na kusikiliza maoni yao katika kuboresha sera na mwelekeo wa chama.
"Chama kimeazimia kuimarisha umoja na nidhamu ya ndani, kufanya semina za itikadi na kuteua Kamati ya Maridhiano ya watu watano kushughulikia migogoro ya ndani," imesema taarifa hiyo katika azimio la pili.
Aidha, NLD imesisitiza kupinga vitendo vinavyohatarisha amani ya taifa na kinachokiita uchochezi wa uvunjifu wa utulivu kupitia mitandao ya kijamii.
Azimio la tatu limeelekeza kuteuliwa kwa walezi wa mikoa kutoka Kamati Kuu ili kusimamia uhai wa chama na kuratibu utekelezaji wa maamuzi katika ngazi zote.
Katika Azimio la nne, NLD imeaazimia kuanzisha programu endelevu ya mafunzo kwa viongozi kuhusu uongozi, itikadi, sheria za uchaguzi na maadili ya uongozi.
Hatua hiyo inalenga kuandaa viongozi na kuimarisha ushiriki wa chama katika ushindani wa kisiasa kwenye uchaguzi na kupata viongozi wenye sifa.
"Azimio la tano limeidhinisha Mpango Mkakati wa Chama 2026–2030, unaolenga kuongeza wanachama hadi milioni mbili ifikapo 2028 na kuongeza ushiriki wa vijana na wanawake," imeeleza sehemu ya taarifa hiyo.
Katika Azimio la sita, chama hicho, kimeelekeza kuimarisha uchumi wake kupitia mfumo wa kidigitali wa michango, miradi ya kiuchumi na harambee ya “mtetezi wa umma.”
Azimio la saba limeweka msisitizo kwenye kuanzisha miradi ya kilimo ya chama kama mazao ya chakula na biashara ili kujenga vyanzo endelevu vya mapato.
Katika azimio la nane, NLD imeazimia kuunda tume ya wataalamu wa kilimo, uchumi na mazingira itakayofanya tafiti za kitaalamu kuhusu mazao na maeneo bora ya uzalishaji, na kuwasilisha ripoti ndani ya miezi minne.
"Lengo ni kuhakikisha chama kinakuwa na vyanzo imara vya mapato ili kiweze kujitegemea katika shughuli zake," imeandika taarifa hiyo.
Aidha, wajumbe wa kamati hiyo wameazimia kubakikisha maazimio yote yanatekelezwa mara moja, huku sekretarieti ikitakiwa kuandaa mpango wa utekelezaji na ufuatiliaji wa karibu.
Akifafanua msimamo wa chama hicho, Doyo amesisitiza NLD imekusudia kuanzisha miradi ya uchumi ili kukifanya chama kujitegemea na kuongeza ushiriki wake katika ushindani wa kisiasa nchini.
"Kamati Kuu imesisitiza uwajibikaji, umoja na uzalendo katika utekelezaji wa maamuzi hayo ili kuimarisha NLD kuwa chama imara na chenye kujitegemea," amesema.