Katibu Kiongozi Apiyo afariki dunia A.Kusini

Picha ya Maktaba ikimuonyesha Katibu Mkuu Mstaafu Ofisi ya Rais, Timothy Apiyo (katikati), akipongezwa na mfanyabiashara maarufu nchini, Mustafa Sabodo (kushoto) na Balozi Paul Rupia alipoadhimisha miaka 81 ya kuzaliwa mwaka 2011.

Muktasari:

  • Mtoto wa marehemu, Clay Apiyo alisema alikuwa anasumbuliwa na mapafu kujaa maji na kwamba, alipelekwa Afrika Kusini wiki mbili zilizopita kwa matibabu. 

Dar/Mwanza. Aliyekuwa Katibu Mkuu Ofisi ya Rais enzi za Utawala wa Hayati Julius Nyerere, Timothy Apiyo (83), alifariki dunia juzi jioni Hospitali ya Milpark Johannesburg, Afrika Kusini.

Katibu Mkuu Kiongozi, Ombeni Sefue alizungumza kwa simu jana kuwa, mipango inafanyika kuurudisha mwili wa marehemu nyumbani.

“Ni kweli Mzee Apiyo amefariki na hivi sasa ubalozi wetu nchini Afrika Kusini,  ulikuwa unashughulikia mipango ya kuleta mwili wake,” alisema Sefue.

Mtoto wa marehemu, Clay Apiyo alisema alikuwa anasumbuliwa na mapafu kujaa maji na kwamba, alipelekwa Afrika Kusini wiki mbili zilizopita kwa matibabu.   

Alisema mwili wa marehemu unatarajiwa kuwasili nchini kesho mchana, Ijumaa utaagwa nyumbani kwake Ukonga Stakishari na Jumamosi utasafirishwa kwenda Kijiji cha Marasibora, Rorya kwa ajili ya mazishi.

Mzee Apiyo atakumbukwa kwa kuwa mmoja wa viongozi nchini, ambaye amefanya kazi wakati wa Utawala wa Rais wa Kwanza, Mwalimu  Nyerere, hasa kipindi cha vita ya kupambana na wahujumu uchumi miaka ya 1980.

Pia, atakumbukwa kwa mengi hususan alipokuwa Katibu Mkuu Wizara ya Viwanda na Biashara, ulipotokea uhaba mkubwa wa bidhaa nchini baada ya kuanzishwa Azimio la Arusha na Serikali kushika njia kuu za uchumi, jambo ambalo lilimlazimu kuanzisha Shirika la Biashara la Taifa. 

 Mzee Apiyo alikuwa Katibu Mkuu Kiongozi wa nne Juni 22,1974 hadi Juni 30, 1986 akipokea kijiti kutoka kwa mtangulizi wake, Dickson Ntembo aliyeshika wadhifa huo Mei 8, 1967 hadi Juni 21, 1974.

Katibu Mkuu Kiongozi wa kwanza alikuwa ni Dunstan Omar (Februari 28,1962-Julai 29,1964), alifuatiwa na Joseph Namata (Julai 30,1964-Mei 3,1967). 

Alizaliwa mwaka 1930 Wilaya ya Rorya zamani Tarime, alipata elimu yake ya msingi na sekondari wilayani hapo na mwaka 1959 alijiunga na Chuo Kikuu cha Makerere Uganda ambako alitunukiwa Shahada ya Kilimo, baadaye alishika nyadhifa mbalimbali nchini kabla ya kushika ukatibu mkuu kiongozi.