Kihongosi akemea fitina na majungu kazini
Katibu wa NEC, Itikadi, Uenezi na Mafunzo wa CCM, Kenani Kihongosi akipokea maelekezo katika Hospitali ya Wilaya ya Kaloleni, leo Jumamosi Juni 6, 2026, alipofanya ukaguzi wa hospitali hiyo.
Muktasari:
- Katibu wa NEC, Itikadi, Uenezi na Mafunzo wa CCM , Kenani Kihongosi, amewataka watumishi nchini kuimarisha mshikamano mahali pa kazi na kuepuka fitina, majungu na uchonganishi vinavyosababisha migogoro isiyo ya lazima. Huku akisisitiza umuhimu wa kulinda amani na kuachana na siasa za chuki ili kuendeleza utoaji wa huduma bora kwa wananchi.
Arusha. Katibu wa NEC, Itikadi, Uenezi na Mafunzo wa CCM, Kenani Kihongosi, amesisitiza umuhimu wa mshikamano mahali pa kazi, akisema migogoro mingi inayojitokeza katika taasisi mbalimbali husababishwa na fitina, majungu, maneno ya uongo na uchonganishi miongoni mwa watumishi.
Aidha amekemea siasa za migogoro,chuki na maneno yanayowagawa watu na badala yake akihimiza kuhubiriwa siasa za maendeleo ambazo zinamgusa mwananchi moja kwa moja.
Kihongosi ametoa kauli hiyo leo Jumamosi Juni 6, 2026 wakati wa ziara yake katika Hospitali ya Wilaya ya Kaloleni jijini Arusha.
Amewataka watumishi wa afya kujenga utamaduni wa kuheshimiana, kushirikiana na kufanya kazi kwa upendo ili kuongeza ufanisi wa utoaji wa huduma kwa wananchi.
"Nimekuwa nikisema mara nyingi kwamba kazi za walimu na watumishi wa afya ni kazi maalum sana si kila mtu anaweza kufanya kazi hizi, zinahitaji moyo wa huruma, uvumilivu na kujitoa.
""Naomba kusisitiza suala la mshikamano mahali pa kazi,mara nyingi migogoro mingi kazini husababishwa na fitina,majunhu,maneno ya uongo na uchonganishi,tuache tabia hizo tuwe mfano wa watu wanaifanya kazi kwa upendo,kuheshimiana na kushirikiana na tukifanya hivyo tutaongeza tija katika utoaji huduma kwa wananchi,"amesema
Aidha, aliwataka wanasiasa kuachana na siasa za migogoro, chuki na maneno yanayogawa watu, akisisitiza kuwa siasa za maendeleo ndizo zenye manufaa kwa wananchi kwa kuwa zinachochea utekelezaji wa miradi na utoaji wa huduma muhimu za kijamii.
“Tuachane na siasa za migogoro,chuki na maneno yanayogawa watu, tuendelee kuhubiri siasa za maendeleo ambazo zinamgusa mwananchi moja kwa moja. Mwananchi anapokuja hospitalini na kupata matibabu, huo ndiyo ushahidi wa maendeleo halisi,” amesema.
Aidha Kihongosi alipongeza maendeleo makubwa yaliyofanyika katika Hospitali ya Wilaya ya Kaloleni, akisema uwekezaji wa Serikali umeboresha kwa kiasi kikubwa huduma za afya zinazotolewa kwa wananchi.
Amesema hospitali hiyo imepatiwa vifaa tiba vya kisasa vya hali ya juu vinavyorahisisha utoaji wa huduma na kupunguza ulazima wa wagonjwa kusafiri umbali mrefu kutafuta matibabu.
“Nimeitembelea hospitali hii mara nyingi nikiwa Mkuu wa Wilaya na baadaye Mkuu wa Mkoa, lakini leo nimefurahi kuona mafanikio makubwa yaliyofikiwa. Kuna vifaa vya kisasa ambavyo baadhi yake hata katika Hospitali ya Mount Meru havikuwepo hapo awali,” amesema
Kihongosi alibainisha kuwa Serikali imetoa zaidi ya Sh2.2 bilioni kwaajili ya ununuzi wa vifaa tiba katika hospitali hiyo.
Amesema uwekezaji huo umechangia kupatikana kwa huduma nyingi za kibingwa katika hospitali hiyo, jambo lililopunguza gharama za matibabu kwa wananchi ambao hapo awali walilazimika kwenda Hospitali ya KCMC mkoani Kilimanjaro.
Mganga Mkuu wa Wilaya (DMO) ya Arusha, Dk Maduhu Nindwa, amesema Hospitali hiyo imepiga hatua kubwa tangu ilipopandishwa hadhi kutoka kituo cha afya na kuwa Hospitali ya Wilaya Aprili mwaka huu
Amesema hatua hiyo imewezesha wananchi kupata huduma za afya za ngazi ya hospitali karibu na maeneo yao na kupunguza msongamano katika hospitali za rufaa.
Dk Nindwa amesema katika kipindi cha mwaka wa fedha 2025/2026 hospitali hiyo imehudumia wagonjwa zaidi ya 150,000 ikilinganishwa na wagonjwa 50,000 waliopatiwa huduma mwaka 2020, huku wastani wa wagonjwa wanaohudumiwa kwa siku ukiongezeka kutoka kati ya 151 na 252 hadi kufikia wagonjwa 450 hadi 501 kwa siku kutokana na maboresho makubwa ya huduma na miundombinu.
Ameeleza kuwa serikali imeendelea kuimarisha upatikanaji wa dawa, vifaa tiba na vitendanishi kwa zaidi ya asilimia 95, huku zaidi ya Sh758 milioni zikitumika kununua dawa na vifaa tiba kati ya Julai 2025 na Aprili 2026.
Aidha, hospitali imepokea watumishi wapya 26 wa kada mbalimbali za afya, hatua iliyoongeza uwezo wa utoaji huduma kwa wananchi.
Bima ya afya
Awali akifungua shina la wakereketwa Sekei,aliwataka wananchi kuchangamkia suala la bima ya afya kwa wote litakapowafikia waachane na propaganda za wanasiasa na badala yake wakajiunge kwenye mfumo ili iwasaidie kupunguza gharama za matibabu.
"Na jambo lingine ndugu zangu ambao napenda kulisema kwenu kwenye shina hili wametoa ombi la bima za wazee. Hili ni jambo la ksera na serikali imeainisha na itaanza bima kwa watu wote. Na mpango huu utaanza mara moja na baada ya mikoa wameishaanza,"amesema
"Kwa hiyo utakapolelewa kwetu, muachane na propaganda za wanasiasa, twendeni tukajiunge kwenye mfumo wa bima itasaidia kupunguza gharama za matibabu yetu,hili ni kipaumbele cha Serikali kuhakikisha afya inakuwa ni kipaumbele cha kudumu kwetu sote.
"Kwani ni jambo ambalo tumelipokea na tunazidi kutoa elimu na kusisitiza kwamba tujiunge katika mfumo wa bima.
Akiwasilisha ombi hilo,Katibu wa shina Elinipa John,aliwasilisha ombi la bima ya afya kwa wazee kwani ni changamoto inayowakabili.