Makonda awapa kazi wenyeviti CCM

Muktasari:

  • Awataka kuwafuatilia wakurugenzi, wakuu wa wilaya wazembe.

Tanga. Katibu wa Itikadi, Uenezi na Mafunzo wa Chama cha Mapinduzi (CCM), Paul Makonda amewaagiza wenyeviti wa chama hicho, katika wilaya zote nchini kutoa ripoti za wakurugenzi na wakuu wa wilaya wazembe wasiotekeleza majukumu yako kwa ufanisi.

Ametoa maagizo hayo leo Januari 21, 2024 akizungumza katika mkutano wa hadhara na wananchi wa Muheza, mkoani Tanga aliposimama kuwasilimia akiwa ziarani kusikiliza na kutatua kero za wananchi.

Amesema kama kuna mkurugenzi au mkuu wa wilaya hatengi muda wa kusikiliza kero za wananchi ajiandae.

Makonda amesema jana Januari 20, 2024 alipotembelea Pangani alibaini kuna migogoro inayosababishwa na mkurugenzi wa wilaya hiyo, Isaya Mbenje aliyedai ameshindwa kutimiza majukumu yake ya kuwahudumia na kutatua kero za wananchi.

Kutokana na hali hiyo, Makonda amempigia simu Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais (Tamisemi), Mohamed Mchengerwa kumweleza kuwa mapendekezo ya CCM mkurugenzi huyo asimamishwe kazi na kuunda kamati ya kuchunguza malalamiko dhidi ya mkurugenzi huyo.

"Wapo wafanyabiashara wanaiuzia Halmashauri ya wilaya ya Pangani  malighafi kwa ajili ya ujenzi wa zahanati lakini hawalipwi fedha zao, wakienda kwa mkurugenzi ni Mungu mtu," amesema Makonda.

Katika hatua nyingine, amemuagiza mkuu wa Mkoa wa Tanga, Waziri Kindamba kutenga siku kwa kila wilaya kusikiliza kero za wananchi, kabla ya kufanya hivyo wahakikishe wanatoa matangazo kwa wananchi ili wafike katika ofisi hizo za umma.

"Siku hiyo iwe maalumu kwa ajili ya wananchi hakuna semina wala vikao bali kusikiliza kero zitakazowasilishwa na wananchi," amesema Makonda.

Katika mkutano baadhi ya wabunge mkoani Tanga ambao ni mawaziri wa maji na afya walimhakikishia Makonda wataendelea kuchapakazi kwa kuwasimamia watendaji ili kufikisha huduma kwa wananchi.

"Serikali imetoa fedha nyingi katika sekta ya afya ikiwemo kuboresha miundombinu, deni lililobaki ni sisi viongozi na watumishi kusimamia vema. Nikuhakikishie tutaendelea kusimamia vizuri," amesema Waziri wa Afya, Ummy Mwalimu ambaye ni mbunge wa Tanga Mjini.

Mbunge wa Pangani, Jumaa Aweso, ambaye ni Waziri wa Maji  aliwahakikishia wananchi wa Muheza, Korogwe na Handeni kuwa Serikali  inatatua kero mbalimbali za maji katika maeneo hayo.