Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Mama, tafadhali piga chini hawa ‘chawa’

Mama usishtuke na salamu yangu kuwa fupi, maana naogopa nisije kufanana na watu nitakaowasanua leo. Humo mjengoni kwako kuna watu wanatufanya sisi mazumbukuku ulimwengu uko huku.

Wanatuchukulia kama kuku wa chipsi ambao mwenzao anachinjwa bandani wakati wao wamejiachia kando yake wakipumulia midomo. Tofauti na kuku wa Kizaramo ambaye akiona wageni wanapokelewa kwa shangwe nyumbani anakula kona uchochoroni.

Hawa ninaokwambia leo ni wale ambao midomoni wana salamu za kizalendo, lakini mioyoni mwao kumejaa unafiki. Nakubali kuwa sisi tulikosea pale walipokuja mikono nyuma wakiomba tuwape ridhaa ya kuja huko.

Nakiri kuwa tulidanganyika na unadhifu pamoja na ukarimu wao bila kujua kuwa wachafu ndio wanaopenda nguo safi. Tukadhani ni kondoo kama sisi, kumbe walishawala wenzetu wakajivika sufu zao.

Binafsi nilianza kushtuka nilipoona wakichimbia dosho mapendekezo na matatizo yetu tuliyowatuma wakuletee. Tulipokuwa tukiwauliza walitujibu kuwa uko bize kiasi cha kukosa muda wa kutushughulikia.

Tulichoshangaa ni kuwaona walivyokuwa wakinywa bia kwa fujo ati kupoza makoo yao yaliyokauka. Kwa nini? Ati kwa sababu wamekuwa bize kupiga mayowe ya kukushangilia. Wanafiki wakubwa hawa!

Mama, hawa ni ndumilakuwili wenye meno kichwani na mkiani. Kelele zote wanazokupigia ni kukuziba masikio usisikie vilio vyetu. Wanakupaka mafuta (kwa mgongo wa chupa) ili usiwasahau kwa kuwa walishamalizana na sisi.

Wanashoboka ili usiwaache katika msimu unaofuata. Kifupi hawa ni mbweha wanaomdanganya mama kondoo kwamba wanakwenda kucheza na watoto wake kumbe ni manunda hatari.

Hapo nje kuna msururu wa wanyonge waliokuja kuwashtaki hawa wahuni kwako. Lakini kwa sababu wanasubiri ruhusa za wahuni haohao, sitegemei kama watakuona. Hilo ndilo lililonifanya mimi kupita “za mnyenje” (njia za panya). Hata hivyo malalamiko yao utayasikia kwenye nong’ono zangu, maana sote ni wahanga wa tufani la aina moja.
Kwanza unaweza kushangaa kuona wakati Taasisi za Serikali na za watu binafsi zikipunguza wafanyakazi, vijiwe vya wahuni hawa vinaongezeka.

Mwanzoni sikuelewa wanafaidika vipi, maana hao si wachaguliwa wala wateuliwa. Lakini sasa naanza kuelewa maana kumbe tuliowachagua wamejigeuza chawa wa wakubwa, halafu nao wanajenga maskani za chawa wao; yaani chawa wa chawa.

Kumbe ndio maana sisi tumesahaulika kabisa, maana wawakilishi wetu wamekuwa chawa wanaojenga mtandao wao. Hii ndiyo sababu ya kuzaliwa kwa magenge ya wahuni kila leo huku mtaani. Kumbe yanafugwa na hao washikadau wa mjengoni kwa faida yao wakiwa na lengo la kuonekana kwa picha ya Taifa zima.

Magenge haya hayana kazi nyingine zaidi ya kucheza kama karagosi. Yakiambiwa “cheka” yatakenua meno, lakini yakiamrishwa kulia basi yatafanya hivyo ilimradi tuonekane wananchi ndo tumelia. Hawa ndio unaowaona wakikushangilia hata pale unapowakemea. Hamna kitu humo.

Viongozi “chawa” ndio waliozorotesha maendeleo yetu. Badala ya kujenga na kusimamia misingi bora ya kutetea masilahi ya nchi, wao wanawekeza kwenye maslahi yao binafsi na wapambe wao. Wanajenga vidato ambapo ili mwananchi ale keki ya Taifa ni lazima aanzie kwa mpambe wa chawa”, kisha akapewe baraka na “chawa”.

Kwa mtindo huu ni vigumu kwa Mtanzania yeyote muadilifu kutoboa nchini mwake. Kiongozi akiwa chawa anapoteza uwezo wa kushughulika na maslahi ya Taifa. Hawezi kumsaidia mwananchi kabla hajahakikishiwa maslahi yake.

Mbaya zaidi atashindwa kukushauri kuhusu maendeleo zaidi ya kukusifia kwa unafiki katika kila jambo, hata lile analoliona linahitaji marekebisho.

Unafiki wa aina hii unaweza kudhoofisha demokrasia na mchakato wa uwajibikaji kwa kukufanya uamini kwamba kila mtu anakubaliana nawe, hata kama wananchi wana mawazo tofauti.

Matokeo yake ni kupungua kwa kasi ya uwajibikaji na mambo kuharibika. Hapo ndipo chawa anapokimbilia kwa wananchi na kukuangushia jumba bovu. Hivyo ndivyo watakavyoiua dhana ya uwajibikaji wa pamoja katika kulijenga Taifa letu.

Duniani kote wanatambua jitihada zako za kufungua mipaka ya kiuchumi ili kuleta hali bora kwa wote. Hili linadhihirika kwa Tanzania kuwa nchi ya kwanza barani Afrika kuwa wenyeji wa mkutano wa rasilimali watu.

Inaeleweka kuwa nchi yetu ina idadi kubwa ya vijana ambao ndio nguvukazi. Hivyo jitihada zako za kumuinua kijana wa Kitanzania zimeshaanza kuelekea kuzaa tija.
Hakika huu ndio wakati muafaka wa kuwazingua wote wanaozingua. Liokoe Taifa lako liondokane na uzoroto, jitihada zako za kuwashirikisha vijana kama mtaji wa kukuza uchumi zichanue mbele ya mapambazuko mapya.

Hatuwezi kuipata Tanzania tunayoiota bila kuwakataa hawa wachumia tumbo. Wakiachia hao ndipo waadilifu watakapoonekana waziwazi, maana “mlango mmoja ukifunga mingine itafunguka”.

Nasema hivi kwa sababu wahuni hawatofautiani na wachawi. Kazi kubwa ya mchawi ni kuwaharibia wenzake hata kama hapati faida yoyote.

Sasa kwa vile wale wahuni walibweteka kizembe na wakajiapiza kula kwa unafiki wao, hawatakubali kuona vijana wako wakisonga mbele katika kukuza uchumi wetu. Watawaharibia kwa dhana ya “tukose wote”.

Mama, usiwaachie kamwe wafike huko. Pamoja na kwamba nakufahamu mama yangu kama mama mwenye upendo na huruma, kwa hili nakuomba usimhurumie mtu. Wamezingua, wazingue!