Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Migogoro ya ardhi ilivyotikisa ziara ya Kihongosi

Katibu wa NEC, Itikadi Uenezi na Mafunzo wa CCM, Kenani Kihongosi, akizungumza  Jumatatu Juni mosi 2026, katika Shina namba moja tawi la Masakta, wilayani Hanang' mkoa wa Manyara alipokuwa katika mwendelezo wa ziara zake katika mikoa ya Kanda ya Kaskazini.

Muktasari:

  • Katibu wa NEC, Itikadi, Uenezi na Mafunzo wa CCM, Kenani Kihongosi amehitimisha ziara ya siku tisa katika mikoa ya Kilimanjaro, Manyara na Arusha ambako migogoro ya ardhi imeibuka kuwa kero kubwa iliyotawala mikutano yake ya hadhara.

Arusha. Migogoro ya ardhi imeendelea kuwa moja ya changamoto kubwa zinazowakabili wananchi, hali iliyodhihirika pia katika ziara ya siku tisa ya Katibu wa NEC, Itikadi, Uenezi na Mafunzo wa CCM, Kenani Kihongosi, katika mikoa ya Kilimanjaro, Manyara na Arusha.

Kama ilivyotokea wakati wa ziara ya Waziri Mkuu, Dk Mwigulu Nchemba hivi karibuni, malalamiko kuhusu ardhi yalitawala mikutano mingi ya hadhara iliyotumiwa na Kenani kusikiliza kero za wananchi.

Katika mikutano hiyo, malalamiko mengi yaliyojitokeza yalihusu migogoro ya ardhi, madai ya uuzaji holela wa maeneo ya wananchi na ucheleweshaji wa utatuzi wa migogoro hiyo.

Ziara hiyo ilianza Mei 29 na kuhitimishwa Juni 6, 2026 katika wilaya za Siha, Hai na Moshi (Kilimanjaro) Hanang', Babati na Simanjiro (Manyara) pamoja na Karatu, Arumeru na Arusha (Arusha)

Mbali na kukagua uhai wa chama na kutembelea miradi ya maendeleo, Kihongosi alitumia mikutano hiyo kusikiliza kero za wananchi na kuelekeza hatua za kuzitatua.

Akiwa wilayani Siha, miongoni mwa changamoto zilizowasilishwa ni za ardhi, maji na miundombinu ya barabara. Moja ya malalamiko yaliyovuta hisia ni ya Mariam Issa, mkazi wa Sanya Juu (80), aliyedai kupoteza shamba lake la ekari tatu kutokana na mgogoro wa ardhi uliochukua muda mrefu bila kupatiwa ufumbuzi.

Akizungumzia suala hilo, Kihongosi alionyesha kutoridhishwa na namna mgogoro huo ulivyoshughulikiwa na kuwataka watendaji wa sekta ya ardhi kuongeza uwajibikaji, akiwemo ofisa ardhi aliyefanya kazi wilayani humo kwa miaka 12.

"Katika masuala ya ardhi wapo wananchi wengi wanyonge wanaoonewa na wenye nguvu. Hatuwezi kama chama kuvumilia hali hiyo. Baadhi ya watumishi wanapaswa kujitathmini kwa sababu kutowajibika kwao kunasababisha Serikali na viongozi wake kulaumiwa bila sababu," alisema.

Katika Wilaya ya Simanjiro, suala la ardhi lilijitokeza kwa uzito zaidi baada ya Mbunge wa Simanjiro, James Ole Millya kueleza kuwa bado kuna malalamiko makubwa kuhusu uuzaji wa ardhi unaofanywa na baadhi ya viongozi.

Ole Millya alisema ardhi ni rasilimali muhimu kwa wananchi wa Simanjiro wanaotegemea ufugaji na kilimo, hivyo ni lazima haki zao zilindwe.

"Bado kuna changamoto kubwa ya ardhi katika Simanjiro. Malalamiko mengi ninayopokea kutoka kwa wananchi yanahusu ardhi. Hatuwezi kuruhusu haki zao zipotee kwa manufaa ya watu wachache," alisema Millya ambaye pia ni Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki.

Alisema hatakuwa tayari kuona haki za wananchi zinapotea kutokana na watu wachache wanaojinufaisha kwa kuuza au kujimilikisha ardhi bila kuzingatia sheria za nchi.

"Nitasimamia ukweli siku zote kwa sababu kazi yangu ni kusimamia masilahi ya wananchi walionichagua. Watu wa Simanjiro wanahitaji ardhi kwa ajili ya ufugaji na kilimo.Tunapogawa ardhi kwa wengine ni lazima sheria zifuatwe na haki za wananchi zilindwe ," amesema.

Kwa upande wake, Kihongosi aliwaonya viongozi wa vijiji, vitongoji na kata wanaotumia nafasi zao vibaya kwa kuuza ardhi au kushiriki vitendo vinavyoibua migogoro.

Alisisitiza kuwa CCM haitavumilia viongozi wanaokiuka sheria au kufumbia macho vitendo vinavyowaumiza wananchi.

"Ni marufuku kwa kiongozi yeyote kuuza ardhi bila kufuata utaratibu wa kisheria. Taifa hili lina sheria zake na kila mtu anapaswa kuziheshimu. Chama hakitasita kuwachukulia hatua watakaobainika kufanya kinyume chake," alisema.

Pia alimtaka Mkuu wa Mkoa wa Manyara, Queen Sendiga, pamoja na viongozi wengine wa Serikali kusimamia kikamilifu utekelezaji wa sheria za ardhi ili kuzuia wananchi kupoteza maeneo yao kwa njia zisizo halali.

Katibu wa NEC, Itikadi, Uenezi na Mafunzo wa CCM, Kenani Kihongosi wakati akizungumza katika Hospitali ya Wilaya ya Kaloleni, Jumamosi Juni 6, 2026 alipokagua hospitali hiyo

"Ni lazima kuwe na usimamizi madhubuti. Bila kufanya hivyo, baadhi ya watu wanaweza kujimilikisha maeneo ya wengine na kusababisha migogoro isiyo ya lazima," alisema.

Aidha, aliwataka wananchi kutoa taarifa kwa mamlaka husika wanapobaini vitendo vya ubadhirifu wa ardhi au viongozi wanaotumia madaraka yao vibaya.

"Viongozi lazima wawe waadilifu na watangulize masilahi ya wananchi. Wananchi mkiona viongozi wanaoshiriki vitendo visivyo halali, toeni taarifa ili hatua zichukuliwe kwa mujibu wa sheria," alisema.

Baadhi ya wananchi waliohudhuria mikutano hiyo waliunga mkono kauli za viongozi hao na kuomba hatua za haraka zichukuliwe kumaliza migogoro ya ardhi.

Mkazi wa Naisinyai, Simanjiro, Moses Mollel, alisema migogoro hiyo imekuwa chanzo cha migongano kati ya wafugaji na wakulima na kuathiri shughuli za uzalishaji.

"Kinachohitajika sasa ni utekelezaji wa maelekezo yaliyotolewa ili wananchi walindwe na haki zao za umiliki wa ardhi ziheshimiwe," alisema

Naye Nasieku Ole Kasaine alisema wanawake wengi wamekuwa waathirika wa migogoro ya ardhi kutokana na changamoto za kufuatilia mashauri mbalimbali ya kisheria.

Mbali na ardhi, wananchi katika maeneo mbalimbali waliwasilisha kero zinazohusu huduma za maji, barabara na miundombinu mingine ya kijamii.

Katika mikutano yake yote kwenye wilaya hizo tisa Kihongosi alisisitiza masuala kadhaa ikiwemo kuwataka Watanzania kuendelea kulinda uhuru, amani na utulivu wa nchi kwa kupinga wanaohamasisha chokochoko na vitendo vinavyoweza kuhatarisha usalama.

Alisema Tanzania imejengwa kwa misingi ya umoja, msihakamano na amani iliyopatikana kwa juhudi za waasisi wa taifa, hivyo wananchi wanapaswa kuendelea kuithamini na kuilinda.

“Hakuna jambo baya kama kuwa mtumwa ndani ya mataifa ya watu, uhuru tulionao leo hapa, tuulinde na wale wanaohamasisha chokochoko tuwapinge hadharani,” amesema.

Wanachama wa CCM katika Shina namba moja tawi la Masakta, wilayani Hanang' Mkoa wa Manyara walipokuwa wakimsikiliza Katibu wa NEC, Itikadi Uenezi na Mafunzo wa CCM, Kenani Kihongosi


Migogoro kwingineko

Migogoro ya ardhi imeendelea kuwa mfupa mgumu, licha ya malalamiko dhidi yake kutawala pia ziaza za Dk Nchemba, katika mikoa mbalimbali nchini.

Pamoja na tangazo la Serikali la upimaji wa ardhi, utoaji hati za kimila hasa vijijini, bado havijatatua changamoto ya migogoro.

Februari mwaka huu, Dk Mwigulu alifanya ziara katika mikoa ya Tanga, Kilimanjaro, Arusha na Manyara, ambapo pamoja na masuala mengine alisikiliza kero za wananchi, wengi wao wakiwasilisha kilio cha migogoro ya ardhi.


Baada ya kuhitimisha ziara katika mikoa hiyo, aliendelea katika mikoa mingine.

Machi 10,2026 akizungumza katika mkutano wa hadhara uliofanyika Kasanga, Sumbawanga, Dk Mwigulu aliwaagiza Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi na Waziri wa nchi Ofisi ya Rais-Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi) kukaa kwa dharura na kuja na mapendekezo yatakayomalizia migogoro ya ardhi iliyodumu kwa miaka mingi.

Dk Nchemba alifikia hatua hiyo baada ya malalamiko ya muda mrefu kutoka kwa wananchi kuhusu migogoro yaa rdhi nchini, na kuwataka viongozi na mawaziri wa kisekta kutafakari na kupendekeza mbinu itakayoleta suluhu ya kudumu.


Kamati ya Bunge yatia mguu

Pia, hivi karibuni akiwa mkoani Arusha, Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Utawala, Katiba na Sheria, Dk Damas Ndumbaro, alisema migogoro ya ardhi imeendelea kuwa changamoto nchini na inaweza kuhatarisha amani ya Taifa endapo haitapatiwa ufumbuzi wa haraka.

Alisema takwimu za kampeni ya Samia Legal Aid zinaonyesha asilimia 36 ya migogoro yote iliyoripotiwa nchini inahusiana na ardhi.

Aliwataka wataalamu wa sheria kufanya tafiti na kuibua suluhu za kisheria na kimfumo ili kudhibiti migogoro hiyo kabla haijaendelea kuathiri utulivu wa nchi.