Mrithi wa Chongolo asiogope ‘chawa’

Watanzania na wadau wa siasa wanasubiri matokeo ya ujio wa Katibu Mkuu wa Chama cha Mapinduzi (CCM), Dk Emmanuel Nchimbi. Tofauti na viongozi wengi kwenye medani za siasa, Dk Nchimbi anaonekana kama mtu aliye tayari kufanya mageuzi ndani ya chama na kwa umma wa Watanzania bila woga. Ni mmoja kati ya watu wasioogopa matokeo baada ya uamuzi mgumu.

Kiti hiki cha moto kimewahi kuketiwa na zaidi ya wanachama 10 tangu kilipoanzishwa mwaka 1977. Katika orodha yao, ni Pius Msekwa na Rashid Kawawa pekee ndio walioondoka kitini kwa amani.

Wengine akina Horace Kolimba, Lawrence Gama, Philip Mangula, Yusuf Makamba, Wilson Mukama, Abdulrahman Kinana, Bashiru Ally na Daniel Chongolo waliondoka kila mmoja na staili yake.

Katika kuonyesha ugumu wa nafasi ya Katibu Mkuu katika chama tawala, karibu kila Katibu Mkuu alikutana na mbilinge za aina yake zilizosababisha kuhojiwa na Kamati ya Maadili, kusimamishwa kazi au kuandika barua ya kujiuzulu. Lakini hakuna mmoja wao aliyeuzungumza kinagaubaga moto uliowafanya waondokane na kikombe hicho.

Pengine hii ni ishara ya ukomavu wa kisiasa na wasingeweza kwenda kupiga kelele mitaani.

Nafasi ya Katibu Mkuu ni ya tatu kwa ukubwa katika mtiririko wa kiuongozi wa chama hicho chini ya Mwenyekiti na Makamu wawili. Kwa mujibu wa Katiba ya CCM, kazi na majukumu ya Katibu Mkuu ni pamoja na kuratibu kazi zote za chama, kusimamia kazi za utawala na uendeshaji katika chama, kuratibu na kufuatilia masuala ya usalama na maadili katika chama na kusimamia udhibiti wa fedha na mali za chama.

Chama hiki kina watu tofauti kama taasisi nyingine yoyote. Wapo waadilifu na wenye utayari wa kuwatumikia wenzao, lakini wapo wanafiki wenye kujifikiria wenyewe binafsi.

Kwa bahati mbaya wale waadilifu hawaishi kurushiwa mawe kama miti yenye matunda. Na wanafiki daima hujiegemeza kwenye nguzo imara ili wanaporusha mawe kwa waadilifu, wakuu wasiyaone hayo.

Ni wazi kila mwanachama wa CCM anaweza kuwa na mawazo yanayotofautiana na uongozi. Kwa sababu hii hawakosekani wanaodhani kuwa wangelifanya vizuri zaidi kama wangelipewa nafasi hiyo.

Kila mmoja anaweza kuota ndoto za Alinacha na kusema; “Ningelikuwa mimi nisingefanya vile, ningelifanya hivi”.

Sababu hii japo kwa udogo, inaweza kuwa chanzo cha ukosefu wa imani kwa viongozi.

Lakini mbaya zaidi Katibu Mkuu ni nafasi inayowagusa wanachama wote, iwe kimaadili, kimaslahi au namna yoyote inayohusu maisha yao ndani ya chama.

Wa kale walisema penye maslahi ndipo majungu huzaliwa, ndipo tunapoona makundi yanayotofautiana yakianzishwa na watu walioamua kwa hiari yao kuishi kwenye chama kimoja. Kuna ukweli kwamba kwenye vyama vya siasa wapo viongozi na wanachama wasio wabunifu, na wasiotaka kujishughulisha na lolote zaidi ya kutafuta mkate wao wa kila siku kupitia chama.

Hawa ndio sumu kali kwa viongozi mahiri, na hufurahi sana wanapoletewa kiongozi asiye na umakini. Hii ni kwa sababu viongozi makini hutaka kazi na si porojo, wakati wao wanategemea blabla kupata ugali.

Waganga njaa wa aina hii ndio hujipachika kama chawa kwa watendaji wakuu. Lakini kwa kiongozi huyu, wana CCM waliojipachika “u-chawa” wategemee tofauti kubwa na matarajio yao.

Kulingana na misimamo yake, wanachama na wajumbe wa Kamati Kuu hawakutegemea kama ungependekeza jina lake kwenye nafasi nyeti kama hiyo. Lakini pia alipoanza kuongea na umma aliwaonya viongozi wa chama kutowakejeli viongozi wa Serikali, tabia iliyokwisha kuanza kuota mizizi ndani ya chama.

Hakihitajiki cheti kwa mtu yeyote kuelewa kwamba nchi yetu inaendeshwa na Katiba na Sheria za Jamhuri za Muungano.
Kwa mantiki hiyo, Serikali inajipambanua kuwa baba wa vyama vyote vya siasa kwa sababu ndiyo iliyovisajili, kama wewe Mheshimiwa ulivyo Rais wa Watanzania wote bila kujali itikadi zao za vyama.

Kwa ukweli huo, viongozi wa vyama vyote vya siasa wanapaswa kuwaheshimu wateule wako Serikalini.

Lakini hawakosekani viongozi wa vyama wanaojizima data makusudi na kujifanya kutoutambua ukweli huu.

Wanadiriki kutoa amri na maagizo kwa Waziri Mkuu na wakuu wa mikoa kwa madai ya chama kushika hatamu za uongozi!
Hawa sidhani kama wanajua maana ya demokrasia na pengine hawajui kwamba Serikali, Bunge na Mahakama ndio mihimili mitatu inayoshikilia dola.

Kwa kipindi kirefu, viongozi wa vyama (tawala na upinzani) wameendelea kuichukulia poa Serikali kama vile wapo nayo kwenye kiwango kimoja au wameizidi nguvu.

Kwa kujua au kutokujua, wanaupotosha umma na kuuonyesha kuwa wao wanaweza kufanya lolote juu ya mhimili huu muhimu. Watu hawa wanatumia uvivu wa Watanzania kujisomea na kujua mipaka ya uongozi wa chama na Serikali kama fursa ya kutafuta kiki.

Ukweli unapodhihirika, uongo hutokomea. Naamini tukiwa na viongozi wa aina ya Nchimbi, upotoshaji na uchawa utaanza kupotea kuanzia kwenye chama tawala na hatimaye vyama vya upinzani.

Ule mzimu unaowaondoa Makatibu Wakuu, tena wengine kwa muda mfupi sana unaweza usionekane tena. Inawezekana kuwa kipele kimempata mkunaji. Mungu amlinde Nchimbi.