Rais Mwinyi kuzindua Kamati ya Maridhiano

Unguja. Rais wa Zanzibar Dk Hussein Mwinyi anatarajia kuzindua vikao vya pamoja vya Kamati ya Maridhiano kati ya Chama cha ACT-Wazalendo na Chama Cha Mapinduzi (CCM) Zanzibar.

 Uzinduzi huo unatarajiwa kufanyika leo Mei 31, 2023 Ikulu Zanzibar. Hii ni hatua muhimu ya kuendeleza mazungumzo na ushirikiano wa vyama hivyo vinavyounda Serikali ya Umoja wa Kitaifa (GNU), kwa maslahi ya wananchi na taifa hilo kwa ujumla.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais Ikulu, Charles Hilary, uzinduzi huo utafanyika leo saa 7:30 mchana.

"Katika uzinduzi huo, Rais Dk Mwinyi atatoa hadidu rejea ambayo itaeleza mpango wa vyama hivi na hatua zijazo za Serikali," amesema


Mei 18, 2023 Dk Mwinyi alikutana na kufanya  mazungumzo na viongozi wakuu Chama cha ACT Wazalendo wakiongozwa na Mwenyekiti wa chama hicho, Juma Haji Duni, makamu wake ambaye pia ni Makamu wa Kwanza wa Rais Othman Masoud na Kiongozi Mkuu wa chama hicho, Zitto Kabwe.

Kamati hiyo pamoja na mambo mengine itakuwa na jukumu la kujadiliana na kutoa mapendekezo ya utekelezaji wa ripoti ya kikosi kazi kilichoundwa kufuatia mkutano wa Baraza la vyama vya siasa uliojadili maeneo mahususi yanayohusu Zanzibar Oktoba mwaka jana.

Katika ripoti ya kamati iliyotokana na  kikosi kazi hicho, ikiongozwa na Mwenyekiti wake, Dk Ali Ahmed Uki ilipendekeza matokeo ya Rais yahojiwe mahakamani na kuangalia muundo mzuri wa Serikali ya Umoja wa Kitaifa na kuwa na Tume huru ya Uchaguzi.