Ruto anavyonyooshewa kidole ziara za kimataifa, mwenyewe ajitetea
Nairobi. Ziara za nje ya nchi za Rais wa Kenya, William Ruto zimeibua gumzo nchini humo ambapo wananchi na wakosoaji wake wanaona ziara hizo zinaliongezea mzigo taifa hilo la Afrika Mashariki, hasa wakati huu ambao kuna mfumuko wa bei.
Ruto amefanya ziara kadhaa za kimataifa mfululizo kuanzia Mei hadi Juni 2026 ambapo wakosoaji wanazitazama ziara hizo kama mzigo kwa walipakodi ambao wanahangaika kujikwamua kimaisha.
Juni 6, 2026, saa chache baada ya kurejea kutoka ziara ya Afrika Kusini, ndege binafsi ya Rais Ruto, iliondoka tena kuelekea Ulaya kwa ratiba nyingine ya shughuli za kidiplomasia na kiuchumi.
Katika taarifa iliyotolewa Juni 7, 2026, Msemaji wa Ikulu ya Kenya, Hussein Mohamed alisema Rais Ruto ameanza ziara rasmi nchini Ubelgiji na Norway pamoja na ziara ya kiserikali nchini Finland.
“Leo mchana, Rais William Ruto ataondoka kwa ziara rasmi nchini Ubelgiji na Norway, na ziara ya kiserikali nchini Finland. Ziara hizi zinalenga kuvutia uwekezaji, kupanua upatikanaji wa masoko kwa bidhaa za Kenya na kuimarisha ushirikiano utakaoongeza mauzo ya nje, kuunda ajira na kukuza uchumi,” ilisema sehemu ya taarifa hiyo.
Ziara hiyo ilikuja muda mfupi baada ya Rais huyo kurejea kutoka Afrika Kusini, ambako alikuwa katika ziara ya kiserikali iliyoanza Juni 3, 2026.
Katikati ya Mei mwaka huu, Rais Ruto alikuwa Azerbaijan kushiriki Kikao cha 13 cha Jukwaa la Dunia la Masuala ya Miji (World Urban Forum - WUF13). Serikali ya Kenya ilisema alikuwa amealikwa na Shirika la Umoja wa Mataifa la Makazi (UN-Habitat) kuwasilisha mafanikio ya Mpango wa Makazi Nafuu wa Kenya pamoja na jitihada za maendeleo endelevu ya miji.
Baada ya kumaliza ziara hiyo nchini Azerbaijan, Rais Ruto alielekea moja kwa moja Kazakhstan kwa ziara rasmi ya kiserikali.
Wakati Rais huyo akiwa Azerbaijan na Kazakhstan, Kenya ilishuhudia maandamano ya kitaifa yaliyoandaliwa na wadau wa sekta ya usafiri wa mabasi madogo (matatu) wakipinga kupanda kwa gharama za mafuta.
Ziara nyingine atakayoifanya ni ya kwenda Evian, Ufaransa ambako unafanyika mkutano wa mataifa yenye uchumi mkubwa wa viwanda (G7), kuanzia Juni 15 – 17, 2026 ambapo Kenya ndiyo taifa pekee la Afrika lililoalikwa kuhudhuria mkutano huo mkubwa.
Baadhi ya viongozi wa muungano wa upinzani, akiwamo Makamu wa Rais wa zamani, Rigathi Gachagua, walimkosoa Rais Ruto kwa kufanya safari nyingi za nje kwa kutumia ndege za kukodi binafsi zinazogharimiwa na walipa kodi, wakati wananchi wengi wakikabiliwa na ugumu wa maisha kutokana na kupanda kwa gharama za maisha.
Hata hivyo, Ruto ametetea tena safari zake za mara kwa mara nje ya nchi, akisema ni muhimu katika kuendeleza maslahi ya kiuchumi ya Kenya na kuvutia uwekezaji, licha ya kukosolewa vikali na viongozi wa upinzani pamoja na baadhi ya wananchi wanaodai safari hizo zinawagharimu walipakodi fedha nyingi.
Akizungumza katika hafla ya umma, mwishoni mwa wiki iliyopita, Rais Ruto alipuuzia madai kwamba safari zake za nje ni matumizi yasiyo na tija ya fedha za umma, akisisitiza kuwa kila safari inalenga kutafuta fursa za kukuza uchumi, kutengeneza ajira na kuimarisha nafasi ya Kenya katika jukwaa la kimataifa. “Shughuli tunazofanya nje ya nchi si safari za starehe binafsi. Hizi ni safari za kimkakati zinazolenga kuleta uwekezaji, masoko na ushirikiano wenye manufaa kwa wananchi wa Kenya,” alisema Rais Ruto.
Ratiba ya safari za nje za Ruto imekuwa mjadala wa mara kwa mara tangu alipoingia madarakani. Wanasiasa wa upinzani wamekuwa wakiilaumu Serikali yake kwa kutumia fedha nyingi katika safari za kimataifa wakati wananchi wengi wanakabiliwa na kupanda kwa gharama za maisha, ongezeko la kodi na changamoto za kiuchumi.
Wakosoaji wake wanahoji kuwa Serikali inapaswa kuelekeza nguvu zaidi katika kushughulikia matatizo ya ndani ya nchi, yakiwamo ukosefu wa ajira, mfumuko wa bei na deni la taifa, badala ya kutumia rasilimali nyingi katika safari za nje.
Wengine wamekuwa wakitilia shaka kama manufaa yanayoahidiwa kutokana na safari hizo yameleta maboresho yanayoonekana kwa wananchi wa kawaida.
Hata hivyo, Rais Ruto ameendelea kusisitiza kuwa ziara hizo zimeleta matokeo makubwa. Kwa mujibu wa Serikali, baadhi ya safari zake zimechangia kupata ahadi za uwekezaji katika sekta za viwanda, miundombinu, kilimo, teknolojia na nishati jadidifu.
Maofisa wa Serikali pia wameeleza kuwa safari hizo zimewezesha kusainiwa kwa makubaliano mapya ya biashara pamoja na ushirikiano wa maendeleo kati ya Kenya na washirika wake wa kimataifa.
Wafuasi wa Rais huyo wanadai kuwa diplomasia ya kimataifa yenye ushiriki mkubwa ni muhimu katika dunia ya sasa inayozidi kuunganishwa kiuchumi. Wanasema Kenya haiwezi kujitenga na mataifa mengine ikiwa inalenga kuvutia mitaji ya uwekezaji na kupanua masoko ya bidhaa zake nje ya nchi.
Mjadala huo unaibuka wakati ambao matumizi ya Serikali yanaendelea kuchunguzwa kwa karibu na wananchi. Asasi za kiraia pamoja na viongozi wa upinzani wameitaka Serikali kuwa wazi zaidi kuhusu gharama na matokeo ya safari za viongozi wa umma, wakitaka itoe taarifa za kina kuhusu makubaliano yaliyofikiwa na uwekezaji uliopatikana kupitia ziara hizo.
Wachambuzi wa siasa wanasema mjadala huo unaakisi wasiwasi mpana kuhusu usimamizi wa uchumi na uwajibikaji wa viongozi kwa umma.
Wanasema ingawa ushiriki wa kimataifa ni nyenzo muhimu ya diplomasia na maendeleo ya kiuchumi, Wakenya wengi wanataka ushahidi wa wazi unaoonyesha kuwa safari hizo zina manufaa yanayoweza kupimika.
Kiongozi wa chama cha People's Liberation Party (PLP) na Waziri wa zamani wa Sheria, Martha Karua, ni miongoni mwa waliomkosoa Rais Ruto kwa safari zake za mara kwa mara nje ya nchi.
Akizungumza katika mahojiano ya televisheni moja nchini humo, Juni 14, 2026, Karua alisema safari hizo zinaongeza mzigo wa kifedha kwa walipa kodi huku zikiwa na manufaa madogo kwa wananchi wa kawaida.
“Nadhani huyu ndiye rais ambaye amesafiri nje mara nyingi zaidi kuliko watangulizi wake wote,” alisema Karua.
“Hapendi kusafiri kwa ndege za Kenya Airways. Anatumia ndege za gharama kubwa ambazo hatuwezi kuzimudu kwa urahisi.”
Aliongeza kuwa: “Wakati watu wake wanaposema kwamba anasafiri kwenda kuleta manufaa kwa taifa, basi waweke wazi gharama za safari zake, gharama za msafara wake pamoja na thamani halisi ya hayo wanayodai kuwa ni manufaa aliyoyaleta.”