Uchaguzi wa viongozi CUF wasogezwa mbele, sababu zatajwa
Muktasari:
- Awali, dirisha la uchukuaji na urejeshaji wa fomu lilifunguliwa Agosti mosi, 2024 likihusisha nafasi tatu za juu na lilipaswa kufungwa Agosti 25, 2024 lakini changamoto za maandalizi zimewalazimu kuongeza muda.
Dar es Salaam. Uchaguzi wa viongozi wa Chama cha Wananchi (CUF) uliotarajiwa kufanyika Septemba 15, 2024, umesogezwa mbele hadi Desemba 13, 2024 kwa kile kilichoelezwa kuwa ni changamoto za maandalizi.
Kinyang’anyiro hicho kitahusisha nafasi za mwenyekiti, makamu mwenyekiti (Tanzania Bara na Zanzibar) na wajumbe wa Baraza Kuu la chama hicho lililopo kwa mujibu wa katiba yao.
Akizungumza na Mwananchi leo Jumatatu Septemba 9, 2024 kuhusu uchaguzi huo, Naibu Mkurugenzi wa Uchaguzi wa CUF, Yusuf Mbungiro amesema dirisha la kuchua na kurejesha fomu za kuwania nafasi hizo pia limesogezwa mbele hadi Oktoba 30, 2024.
Awali, dirisha la uchukuaji na urejeshaji wa fomu lilifunguliwa Agosti mosi, 2024 likihusisha nafasi tatu za juu na lilitakiwa kufungwa Agosti 25, 2024, lakini changamoto za maandalizi zimewalazimu kuongeza muda.
“Tumesogeza muda mbele na mkutano wetu mkuu wa kuchagua viongozi utafanyika Desemba 13 hadi 15, 2024. Kwa hiyo, dirisha la kuchukua na kurejesha fomu bado liko wazi pamoja na kuendelea na chaguzi kwa baadhi ya wilaya za kichama ambazo hazikufanya,” amesema Mbungiro.
Amesema sababu nyingine ya kupeleka mbele uchaguzi huo ni kutoa uhuru kwa wilaya 27 za kichama ambazo hazikufanya uchaguzi watekeleze jukumu hilo.
“Wilaya nyingi za kichama zilikuwa zimefanya uchaguzi, lakini zilizobakia ni 27 zinatakiwa zifanye, lakini kama hawatafanya kwa muda huo kwa sababu mbalimbali, basi tutaendelea na uchaguzi mkuu,” amesema.
Katika maelezo yake, Mbungiro amedai idadi ya waliochukua na kurejesha ni kazi aliyowaachia maofisa wake wachakate na ndani ya siku tatu watakuwa wamemkabidhi orodha kamili ya waliojitokeza.
Alipotafutwa kuzungumzia mchakato huo, Mkurugenzi wa Uhusiano wa CUF, Mohamed Ngulangwa amesema idadi ya waliochukua fomu hadi sasa katika nafasi ya mwenyekiti Taifa ni saba, akiwemo mwenyekiti wa sasa, Profesa Ibrahim Lipumba.
“Lipumba amechukuliwa fomu na wanachama wa CUF, baada ya kumuomba na kumbembeleza ndipo alikubali achukuliwe. Wanaamini anaweza kuwafikisha mbali kwa kuwa wametoka naye mbali na amekuwa akizunguka wilaya zote kuwatembelea,” amesema Ngulangwa.
Ngulangwa amesema kwa nafasi ya Makamu Mwenyekiti Tanzania Bara na Zanzibar, pande zote za muungano, watu sita wamejitokeza kila upande.
“Katika idadi hiyo, ni wachache wamerejesha fomu hadi sasa, lakini kwa kuwa muda bado, ngoja tusubiri watakuja kwa kuwa muda bado wanao,” amesema Ngulangwa.
Ushauri wa Lwakatare
Mmoja wa wagombea wa nafasi ya uenyekiti, Wilfred Lwakatare ameonyesha wasiwasi wa kusogezwa mbele kwa uchaguzi huo kwa kile alichoambiwa kuwa ni changamoto ya fedha za kuitisha mkutano mkuu.
Lwakatare amesema amewashauri viongozi kwamba wagombea wa nafasi za juu washirikishwe kuhusiana na changamoto hiyo, ili wachangie mawazo kuhusu namna ya kupata fedha za kuitisha mkutano mkuu
“Hiki chama wakati tunakianzisha hatukuwa na hata senti tano, lakini tuliendelea hadi chama kilipofika, tulifika mahali tukapata ruzuku ya Sh160 milioni kwa mwezi, lakini tumeshuka hadi kuwa na Sh25,000 kwenye akaunti, chama chenye usajili namba mbili.
“Hiki chama kina watu, inategemea na ushirikishaji pale unapokwama, ukiwashirikisha vizuri, hakuna mahali unapoweza kukwama. Nakumbuka kuna wakati tulihitaji Sh1 bilioni za kufanya mkutano mkuu. Hiyo hela hatukuwa nayo, lakini ilipatikana kutoka kwa wanachama,” amesema Lwakatare.
Amesisitiza kwamba wakutane kushauriana, ili mkutano mkuu ufanyike Septemba hii, ili washiriki uchaguzi wa serikali za mitaa utakaofanyika Novemba 27, 2024 wakiwa na safu ya viongozi wapya.