Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

UDP yaahidi kusogeza huduma za maji safi kwa wananchi

Mgombea urais kupitia Chama cha UDP, Saum Rashid (kulia, mwenye miwani) akizungumza na wakazi wa mji wa Maswa katika mkutano wa kampeni uliofanyika Septemba 6, 2025 wilayani Maswa, mkoani Simiyu. Picha na Samwel Mwanga.

Muktasari:

  • Simiyu ni miongoni mwa maeneo yenye upungufu mkubwa wa maji safi.

Simiyu. Mgombea urais wa Tanzania kupitia Chama cha UDP, Saum Hussein Rashid, ameahidi kusogeza huduma ya maji safi na salama kwa kila mwananchi endapo atachaguliwa kuunda Serikali katika uchaguzi mkuu unaotarajiwa kufanyika Oktoba 29, 2025.

Akihutubia jana Jumamosi, Septemba 6, 2025, wananchi waliojitokeza katika mkutano wa kampeni uliofanyika viwanja vya Madeco mjini Maswa, Hussein amesema tatizo la maji bado ni changamoto kubwa nchini, hususan vijijini, jambo linalowafanya wananchi wengi kuishi kwa tabu.

“Huduma ya maji ipo, lakini si toshelevu. Serikali ya UDP tutakapopewa ridhaa, tutaweka kipaumbele kuhakikisha kila mwananchi anapata maji safi na salama karibu na makazi yake. Maji ni uhai, bila maji hakuna maendeleo,” amesema.

Amesema Mkoa wa Simiyu ni miongoni mwa maeneo yenye upungufu mkubwa wa maji safi. Kwa mujibu wa takwimu za Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS), zaidi ya asilimia 40 ya kaya vijijini hutegemea visima vya asili na mito, ambavyo hukaushwa na ukame.

Mgombea urais kupitia Chama cha UDP, Saum Rashid akihutubia wakazi wa mji wa Maswa katika mkutano wa kampeni uliofanyika Septemba 6, 2025 wilayani Maswa, mkoani Simiyu. Picha na Samwel Mwanga.

Hali hiyo imekuwa kikwazo kwa shughuli za kilimo, ufugaji na ustawi wa familia. Wanawake na watoto hutumia muda mrefu kutafuta maji badala ya kushiriki kwenye shughuli za uzalishaji.


Wananchi wanasemaje?

Suzana Jilingisila, mkazi wa Mwamanimba, amesema familia nyingi bado zinalazimika kutembea zaidi ya kilomita tatu kufuata maji.

“Kila siku tunaamka alfajiri, wakati mwingine maji yanakauka kabisa. Tunahitaji suluhisho la kudumu. Tunaamini wanasiasa wanapotuahidi lazima waweke vitendo,” amesema.

Naye John Mwalimu, mkazi wa kijiji cha Ntuzu, amelalamikia athari za kiafya zinazotokana na uhaba wa maji safi.

“Mara nyingi tunalazimika kutumia maji yasiyo salama kwa sababu tunakosa ya bomba. Magonjwa ya tumbo na kuhara yamekuwa ya kawaida, hasa kwa watoto,” amesema.

Kwa upande wake, Asha Ramadhani, mkulima wa Nyabubinza, amesema maji yakipatikana karibu kutawaokoa wanawake muda na nguvu.

“Kwa sasa muda mwingi tunapoteza barabarani kufuata maji. Tungekuwa tunautumia kufanya shughuli za kilimo na biashara ndogo ndogo,” amesema.


Kauli ya UDP

Rashid amesema Serikali ya UDP itapanga bajeti ya kutosha kwenye sekta ya maji, kuboresha miundombinu na kusogeza huduma vijijini kwa usawa.

“Tunahitaji mabadiliko ya kweli. Serikali itakayojali wananchi wake lazima ihakikishe maji yanapatikana bila usumbufu,” amesisitiza.

Wakati UDP ikiahidi kusogeza huduma hiyo, vyama vingine vya upinzani na chama tawala (CCM) pia vimekuwa vikitoa ahadi za kuboresha huduma za maji.

Hata hivyo, wananchi wamesema tatizo limekuwa likiendelea kwa miaka mingi bila suluhisho la kudumu.