Ushauri wangu kwa Doktari Nchembuz

 Nkwazi Mhango

Doktari Lameki Mkumbo Madilu Nchembuz, kwa vile unapenda kuitwa doktari hata kama udoktari wenyewe ngwengwe, acha nikuite ili tuelewene. Naomba usome hii kitu kimyakimya. Usimuonyeshe fyatu yeyote.

Pia, kama kweli maza anamaanisha serious business, omba asiisome akakutumbua, japo najua hawezi kwa vile mnahitajiana, hasa usawa huu wa kuelekea uchakachuaji ujao. Hayo tuyaache nitayadurusu siku zijazo.

Juzi nilikusikia mwenyewe ukisema eti siri kali ianze kununua gold ili kupata njuluku za uhakika. Kwani, shida yetu ni kukosa njuluku za uhakika au kukosa uaminifu na uwajibikaji kwa mafyatu? Hivi unataka kumfyatua nani au unadhani mafyatu ni maskini wa kumbukumbu.

Unakumbuka siri kali ikifanya hiyo biashara kichaa na kuishia kuuziwa kakumba baada ya mafyatu fulani siri kalini kushirikiana na wauza dhahabu na kufyatua ulaji? Ulikuwa wapi au ndo ulikuwa unanyonya?

Aaaah!, sorry, doktari unadhani hakuna njia nyingine ya siri kali kufyatua njuluku? Basi nitakuonyesha njia rahisi ya siri kali kufyatua njuluku tena kihalali.

Mosi, kusanyeni kodi kikamilifu badala ya kuacha mafyatu mafisi na mafisadi kukusanya kodi na kujilimbikizia. Mnakumbuka visa vya mafyatu kuua mashine za kielektroniki na kupiga njuluku huko wilayani vilivyofichuliwa hivi karibuni?

Je, hili li siri kali limefanya nini zaidi ya kueneza ubangaizaji na sanaa? Mnajali nini wakati nyie ndiyo wanufaika nambari wani? Anayebisha aniambie mbona hatusikii kwenye mahekalu yenu wakija mafyatu na kujiibia wakati mkiangalia na wasifanywe lolote au kutoa ngonjera, longolongo na sanaa kama mfanyavyo tukifyatuliwa? Hii misiri kali ya kisanii taabu tupu. Anyways, hayo tuyaache.

Pili, kupata njuluku za heri na uhakika, jenga uaminifu, ubunifu, uwajibikaji, na mazingira ya uzalishaji badala ya kukazania mitozo na usanii huu wa siri kali kutaka kujiingiza kwenye biashara ili kupiga.

Mmeshindwa hata ubinafsishaji mdogo tu, mtaweza biashara ya madini yenye kila aina ya utapeli kama dhahabu na madini mengine? Mnashindwa hata kukusanya kodi, mtaweza hii biashara?

Badala ya kutaka kuwaongezea mafyatu hasara, maumivu, presha, na umaskini, jenga mazingira mazuri ya uzalishaji. Mkifanya hivyo, mafyatu watatengeneza njuluku na kulipa kodi.

Tatu, ziba mianya ya utoroshaji njuluku zetu na madini. Hapa maana yake ni kuweka uchumi mikononi mwa mafyatu wa kaya hii badala ya kuacha kwenye mikono ya kunguru toka nonihino kwa akina dugu yangu.

Nne, pambana na ufisadi, ubabaishaji, uvivu, usanii na matumizi mabaya ya rasilimali na njuluku za mafyatu kiukweli bila ya usanii. Jiulize. Je, CAG anapotoa ripoti ya mwaka ambazo siku zote ni msiba kwa mafyatu na sherehe kwenu, pamoja na madudu yote hayo, huwa li siri kali linafanya nini zaidi ya kutoa matamko na kufyatua mafyatu ambao huishia kuufyata na kuliwa kiulaini?

Huwezi kutegemea upate njuluku wakati kila jambo linafanyika kibabaishaji, kifisadi, kisanii, mbali, na uvivu na uzembe vinavyovumiliwa kutokana na kujuana. Hebu mfano, jikumbushe kashfa ya hivi karibuni ya Mkurugenzi wa mkoa wa Mwendazake aliyepatikana kashfa akahamishiwa Moro.

Je, wapo wangapi na washapiga njuluku ngapi za mafyatu?
Tano, tueleze hii dhahabu itakavyonusurika iwapo mmeshindwa hata kuilinda hiyo iliyoko ardhini? Yako wapi makinikia mliyotufyatua changa la macho nayo? Kama mnashindwa hata kulinda tanzanite Mirirani mtaweza dhahabu safi au mtakusanya kakumba na kuiweka na kuondoka na dhahabu safi kama ilivyotokea wakati ule wa wizi wa ruxa?
Mmetupotezea njuluku kujenga na kuzungushia ukuta Mirirani wakati akina nanihii bado wanapiga njuluku na kampuni zao mizimu. Kwani, Mirirani Tanzanite hazivushiwi kupitia hayo mageti? Kaulize akina hao.

Sita, je, hiyo dhahabu mtanunua toka kwa kampuni hizi ambazo zimekuwa zikitupiga tangu ziingie? Jikumbushe bilioni 30 zilizozamishwa na kampuni ya kuchimba dhahabu ya Buhembe wakati wa Ben Makapi? Je, wajanja waliozifyatua mliwafanya nini zaidi ya Muumbaji kuwafyatua baada ya kugundua mafyatu hamuwezi kufanya lolote japo mnaliwa kila uchao?

Jikumbushe akina Mgonjwa na Chwenge mbali na akina Kadamage. Ibra M7ha, Kagoda ambaye siku hizi amezaliwa upya, Meremetuka, Richmonduli, Absa, kuunguzwa kwa benki kubwa, juzijuzi Mirirani na wengine wengi walioifyatua kaya hii.
Jikumbushe kashfa kama Mwanakaya gold na nyingine nyingi zilizamisha njuluku kibao za mafyatu kama mna kumbukumbu au utaratibu wa kutunza kumbukumbu.
Kwa ushauri wangu, hii unayopendekeza ni biashara kichaa, tena ifanywayo na vichaa. Kama tulivyopigwa wakati wa ruxa, mtatupiga halafu mnakuja na longolongo bila kujali mnakuwa mmeishafyatua mafyatu. Hapa ni usiamini. Mnataka kuwaliza mafyatu.

Kwa nini sasa, au ni kwa vile kuna uchakachuaji ujao twenty twenty-five? Kwa nini miaka yote mmekuwa mnapokea madafu wakati wenzenu wanahomola na kwenda kuuza kwa njuluku kali badala ya kupokea kodi na mirahaba kwa dhahabu badala ya madafu yenu? Halafu eti mnajidai ni madoktari. Anza kutoza kodi na mirabaha kwa dhahabu muache uvivu wa kufikiri.

Hivi leo nimekunywa bia ngapi? Hata kama nimelewa, mafyatu msikubali kuwa kichwa cha mwendawazimu akina Madilu kujifunzia kunyoa.