Uzalendo ni silaha ya ujenzi wa Taifa

Zamani rafiki zangu wengi wa shuleni walijua mimi ningekuja kuwa kiongozi au mwanasiasa. Nilikuwa nikiwahamasisha kushiriki matukio ya kisiasa kama vile nimeyaandaa mimi. Kwa mfano tulipokuwa na mapokezi ya viongozi wa nje, wenzangu waliiona hiyo kama fursa ya ‘kula chocho’, wangetoroka kwenda kufanya yao bila kujulikana. Lakini mimi niliwakazia kwamba hiyo ndiyo fursa ya kuona kilichomo kwao.

Nikideklea interest zangu, nilikuwa kiongozi kwenye masomo ya Lugha, Siasa na Historia. Yote hayo yalitokana na jinsi nilivyowatafsiri viongozi kutokana na sura zao, matamshi na lugha walizotumia hapa kwetu. Ni ukweli kwamba sikuielewa lugha ya mmojawao, lakini kwa jinsi alivyokuwa akiongea na Watanzania sikukosa cha kuhadithia.

Ni kama kijana yeyote wa wakati huo alivyoweza kuhadithia picha la Kihindi lililokwenda kwa masaa matatu, kwa sababu tu anamfuatilia Amitabh Bachchan au Dharmendra.

Nilihisi kwamba ningelienda mbali zaidi ningelikuwa mwanasaikolojia mzuri. Niliisikiliza hotuba ya Mwalimu wakati wa mchakato wa kumteua Mzee Benjamin Mkapa kuipeperusha bendera ya CCM, nikagundua kumbe nilikuwa najua mengi kuliko nilivyojijua. Alisema kiongozi wa kweli atajulikana machoni pake.

Hata mtu atie huruma, au avae sura ya mbuzi, lakini mwangalie kwa umakini ili ugundue iwapo anakwambia la moyoni au anakupiga changa la macho.

Wanasiasa wengi hutembelea huruma (passion) za wapiga kura. Wachache wanatembea kwenye njia zao ambazo ndizo wanaziona za kuleta mabadiliko kwa wananchi wao. Tusishangae kuona Trump anatawazwa kuwa Rais wa Marekani kwa mara nyingine, wala tusijiulize Wamarekani wameleweshwa mvinyo gani; bali tuangalie wakisemacho wapinzani wake na kile alichoshikilia yeye.

Yeye amebakia kwenye upendeleo wa Wamarekani. Mpaka sasa ni marais wengi wanaondoa uhusiano na Marekani. Hivyo ni muhimu kutambua kuwa kiongozi anayebeba machungu ya Watanzania ndiye wanayemhitaji Watanzania.

Na Watanzania watameng’enyua kati ya mwenye uso wa mbuzi na yule atakayetaka huruma za wapigakura.

Nasema hivi kwa kuwa hizi panga pangua za safu za uongozi hazijakuwa na tafsiri ya moja kwa moja huku uswazi. Wengine washaanza kunong’ona kwamba huu ni mchakato mpya kuelekea uchaguzi ujao. Kama kuna ukweli kuhusu hilo, nina wasiwasi kwamba tutaendelea kusimama au kutambaa katika safari yetu ya kimaendeleo. Kukijenga chama hakuna maana kubwa kuliko kuijenga Serikali.

Tanzania imekuwa na mchango mkubwa sana katika ukombozi wa Afrika. Nadhani mpaka leo inaamini kwamba haitakuwa huru mpaka nchi zote za Afrika ziwe huru.

Hii ina maana kubwa sana kwenye maendeleo ya Bara letu kwa sababu hakuna uhuru bila maendeleo. Inatisha sana kuona nchi tulizozisimamia kupata uhuru zinakuwa kimbilio la watoto wetu. Sina maana kuwa watoto wetu wasiende nchi jirani kutafuta maisha, ila isiwe kwa sababu tumechoka kivileeeee...

Napenda kukumbusha kuwa Tanzania siyo ya kitoto kwenye maendeleo ya dunia yetu. Kama itakumbukwa vizuri mwaka 2013 wakati dunia nzima ikiwa inafuatilia matangazo ya moja kwa moja ya kumbukumbu ya kifo cha Rais Nelson Mandela, jambo la kihistoria lilifanyika: Rais Barack Obama wa Marekani alishikana mkono na Rais Raul Castro wa Cuba. Tukio hilo lilionyesha taswira mbili za Tanzania duniani:

Ya kwanza ni uhusika wa Tanzania katika mapigano ya kuusaka uhuru wa Afrika ya Kusini. Bila kujali makundi ya Waafrika yaliyokuwa yakipingana yenyewe kwa yenyewe, Tanzania ilisaidia kwa nguvu kubwa, ikiwa ni kiongozi wa harakati za uhuru wa Afrika, hasa maeneo ya Kusini mwa bara la Afrika.

Lakini taswira ya pili ni uhusika wa Tanzania kwenye siasa ya Ujamaa na Kujitegemea. Kwenye tukio la Obama na Castro dunia ilijifunza kwamba ubepari hauwezi kuwepo pasipo ujamaa. Mabepari hawakuisha kuishutumu Serikali ya Cuba ya tangu enzi za Fidel Castro kuhusiana na siasa zake. Cuba, licha ya kuwa jirani wa Marekani, ni hasimu mkubwa wa nchi hiyo tangu enzi na enzi. Lakini zaidi ni kwamba Cuba ilizisaidia nchi za Kusini mwa Afrika kujikomboa.

Katika wakati huu ni lazima tujihadhari vikubwa na kujenga vyama badala ya nchi. Uchaguzi upo, na chama chochote kitakachofanikiwa kuongoza nchi ni lazima kihangaike na Taifa. Tusije kuwajenga viongozi watakaojali vyama badala ya wananchi, kwani kiongozi yeyote atakuwa ni wa vyama vyote. Ndiyo maana hata leo sisi tunaamini kwamba uzalendo ni kitu cha kwanza katika maendeleo yetu.