Wadau wachambua safu mpya ACT-Wazalendo, mustakabali wake

Viongozi wapya wa Chama cha ACT Wazalendo wakiwa kwenye picha ya pamoja kutoka kushoto ni Makamu Mwenyekiti (Bara), Isihaka Machinjita, Kiongozi wa chama, Dorothy Semu, Mwenyekiti wa chama, Othman Masoud Othman na Makamu Mwenyekiti (Zanzibar), Ismail Jussa, jijini Dar es Salaam, leo Machi 6, 2024. Picha na ACT-Wazalendo

Muktasari:

  • Siku mbili za mkutano mkuu wa chama cha upinzani nchini Tanzania ACT-Wazalendo zimemalizika kwa kupata viongozi wapya, akiwemo Dorothy Semu anayekuwa Kiongozi wa Chama (KC).

Dar es Salaam. Chama cha ACT-Wazalendo kimekamilisha uchaguzi na kupata safu mpya ya viongozi wa juu watakaokiongoza chama hicho hadi mwaka 2029, huku mtihani wao wa kwanza ukitajwa kuwa ni kukipa mafanikio katika uchaguzi wa mwaka huu na ule wa mwakani.

 Safu hiyo imepatikana kupitia mkutano mkuu wa nne uliofanyika kwa siku mbili  katika ukumbi wa Mlimani City, Dar es Salaam jana na leo Jumatano, Machi 6, 2024 na washindi kwenda kutangaziwa katika mkutano wa hadhara uliofanyikia Uwanja wa Las Vegas, Mabibo.

Safu hiyo ya juu ya uongozi ambayo yote ni mpya, inaongozwa na Dorothy Semu akiwa Kiongozi wa Chama (KC), akichukua nafasi ya Zitto Kabwe aliyemaliza muda wake wa uongozi wa vipindi viwili vya miaka mitano mitano.

Semu aliyekuwa Makamu Mwenyekiti Bara kabla ya kuikwaa nafasi hiyo, atakuwa pamoja na Othman Masoud Othman, Mwenyekiti na makamu wenyeviti, Jussa Ismail (Zanzibar) na Isihaka Mchinjita (Bara).

Hatua ya Semu, Othman, Jussa na Mchinjita kuibuka kidedea inaonyesha ACT-Wazalendo, imepata safu mpya ya viongozi wa juu, huku leo ikitarajiwa kutangazwa sekretarieti mpya itakayokuwa na katibu mkuu, manaibu, makatibu wa ngome zote tatu za vijana, wanawake, wazee na wakuu wa idara.

Kwa sasa sekretarieti hiyo inaongozwa na Ado Shaibu ambaye ni Katibu Mkuu. Swali linalobaki ni je, ataendelea na wadhifa huo au atapatikana mwingine? Kwa manaibu, Joran Bashange (Bara) na Nassor Ahmed Mazrui inaelezwa wanastaafu nafasi hizo.

Nafasi nyingine inayosubiri kujua ni nani anaikwaa ni Naibu Katibu Mwenezi, Habari na Mahusiano na Umma wa ACT-Wazalendo kwa sababu aliyekuwa akiiongoza, Janeth Rithe amechaguliwa kuwa Mwenyekiti wa Ngome ya Wanawake.

Kwa mabadiliko ya katiba ya chama hicho, katibu mkuu, naibu katibu wakuu na makatibu wa ngome za chama hicho (Vijana, Wanawake na Wazee) wanateuliwa. Kwa maana hiyo kesho Alhamisi, itafahamika nafasi hizi zote ni kina nani watateuliwa na kikao cha Halmashauri Kuu kitakachoongozwa na Mwenyekiti, Othman.

Mchambuzi wa siasa wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Dk Richard Mbunda amesema safu mpya ya viongozi hao, itasaidia na itakibeba ACT-Wazalendo kwa sababu ni watu wenye uwezo kueleza hoja hatua itakayokijenga na kukikuza kisiasa chama hicho.

Mtazamo wa Mbunda juu ya safu hiyo ya uongozi inawiana na ile ya mchambuzi wa siasa, Said Msonga ambaye amesema hatua ya ACT-Wazalendo kukakimilisha mchakato wa uchaguzi, imedhihirisha ni chama ambacho kinajipanga na kuonyesha kwa vitendo namna demokrasia inavyotakiwa kuwa ndani ya vyama.

Msonga amesema ACT-Wazalendo imepata viongozi wapya katika uongozi, lakini sio wapya katika chama, kwa sababu walishahudumu nyadhifa mbalimbali na wamekuwa katika siasa kwa muda mrefu.
Wakati wachambuzi hao wa medani za kisiasa wakieleza hayo, Semu akiwahutubia mamia ya wananchi kwenye mkutano wa hadhara wa kutangazwa kwao, amesema uchaguzi wa chama umemalizika, kinachotakiwa sasa ni kufanya kazi kwa pamoja.

"Baada ya joto kubwa la miezi minane ya uchaguzi, sasa tunakwenda kufanya kazi ya kuwasemea Watanzania na matatizo yao,” amesema.

Katika hotuba yake fupi, Semu amesema chama hicho kimejiandaa kushiriki na kushinda uchaguzi wa serikali za mitaa mwaka huu pamoja na uchaguzi mkuu mwakani, huku akiwataka viongozi wenzake kwenda kuhamasisha wanachama wajitokeze kushiriki.

Viongozi wa chama cha ACT Wazalendo wakiwa kwenye matembezi kutoka Mlimani City hadi uwanja wa Las Vegas uliopo Mabibo jijini Dar es Salaam, leo Machi 6, 2024, ambapo matokeo ya uchaguzi wa ndani wa chama hicho yalitangazwa katika eneo hilo.

Kwa upande wake, Othman ambaye pia ni Makamu wa Kwanza wa Rais Zanzibar  amesema kazi yake kubwa itakuwa kusimamia yale ambayo chama hicho, kiliwaahidi Watanzania kupitia dira yao, akisema wana uwezo na nafasi hiyo na wana dhamira ya kuyatekeleza masuala hayo.

 “Kwa kushirikiana na viongozi wenzangu tunakwenda kujenga chama chetu, kujenga Tanzania ili wananchi watuamini na kutupa fursa katika uchaguzi wa serikali za mitaa na uchaguzi wa madiwani, ubunge, uwakilishi na urais ili waone namna ACT-Wazalendo itakayokwenda kuijenga nchi hii.

“Leo sio fursa ya kusema mengi, ila naombeni imani na ushirikiano, niwaahidi tutakwenda kusimamia chama hiki, ili kutekeleza ahadi yetu kwa wananchi wa Tanzania Bara na Zanzibar,” amesema.

Othman kwa mara nyingine amevaa viatu vya Maalim Seif Sharif Hamad  ambaye alifariki Februari 17, 2021.

Miongoni mwa watu ambao Maalim Seif inaelezwa aliwapendekeza enzi za uhai wake kuwa wanaoweza kurithi nafasi ya Umakamu wa Kwanza wa Rais ni Othman. Alipofariki dunia, ACT-Wazalendo waliishi wosia huo na kumpendekeza kuwa Makamu wa Kwanza wa Rais. Rais Hussein Mwinyi akamteua na kumwapisha.


…wanaweza kuimudu

Wakiichambua safu hiyo, Dk Mbunda amesema Semu anaweza kuimudu nafasi ya KC, kwa sababu atakuwa anapata ushauri kutoka kwa Zitto na Babu Duni ambao ni wazoefu katika masuala ya siasa. Amesema anamuona akiimudu majukumu ya KC.

Kuhusu Othman, Dk Mbunda amesema ilikuwa lazima kiongozi huyo awe na mamlaka ndani ya ACT-Wazalendo, ili kutekeleza majukumu yake vema, ndio maana baada ya mashauriano Babu Duni aliamua kujitoa na kumuachia agombee peke yake nafasi hiyo.

“Tuna uhakika ACT-Wazalendo itaendelea kujiimarisha kuwa chama kikuu cha upinzani Zanzibar, hatua hii itamsaidia Othman kushawishi ndani ya chama kutumika mara mbili Serikali na ACT,” amesema Dk Mbunda.

Kiongozi wa chama cha ACT Wazalendo aliyemaliza muda wake, Zitto Kabwe akimpongeza kiongozi mpya wa chama hicho, Dorothy Semu kabla ya kumpisha kwenye kiti chake, wakati wa mkutano maalumu wa kutangaza matokeo ya uchaguzi wa ndani wa chama yaliyofanyika katika uwanja wa Las Vegas uliopo Mabibo jijini Dar es Salaam leo Machi 6, 2024.

Naye Msonga amesema: “Katika mazingira ya kawaida sio jambo jepesi kufanya mabadiliko ya kiuongozi kama ambavyo ACT-wamefanya katika hali ya utulivu.

Tumekuwa tukisikia rabsha za hapa na pale kwa baadhi ya vyama hasa nyakati za uchaguzi ikitokea watu wakionyesha nia ya kuwania nafasi zinazoshikiliwa na viongozi wanaonekana ni waasisi au wenye maoni kunakuwa na msuguano.”

Msonga amesema Semu ni mwanamama jasiri ndani ya ACT-Wazalendo, kwa sababu alianza kwa kushika nyadhifa mbalimbali hadi sasa yupo katika nafasi ya KC.

“Ni dhahiri ana uzoefu wa kutosha wa kuendesha siasa, kuelewa falsafa na itikadi ya ACT-Wazalendo. Anaweza kurithi vizuri mikoba ya Zitto ingawa si kwa asilimia 100, kwa sababu kila mwanasiasa ana haiba yake, lakini kwa uzoefu wake ataweza kubeba majukumu haya,” amesema.

“Othman amekuwa katika siasa kwa muda mrefu, uenyekiti wa chama utampa mawanda mapana ya kusukuma ajenda na falsafa ya chama chake na ameshawahi kushika nafasi za juu huko nyuma, ni mtu anayeelewa  masuala ya uongozi,” amesema.

Msonga alisema Jussa na Mchinjita ni wanasiasa wazoefu waliokuwa CUF kabla ya kuhamia ACT-Wazalendo, kwa hiyo wana uelewa mpana namna ya kuendesha siasa za chama hicho.

“Kwa uongozi huu mpya kutakuwa na mwendelezo mzuri wa kupokea mawazo kutoka kwa watangulizi wao ili kuendelea kukitangaza, kukiimarisha na kukijengea ushawishi kwa Watanzania,” amesema Msonga.

 

Walivyotangazwa washindi

Awali, katika mkutano huo wa hadhara ulioanza kwa maandamano kutoka Mliman City, Katibu Mkuu wa ACT-Wazalendo, Ado Shaibu amesema ilizoeleka matokeo ya uchaguzi kutangazwa ukumbini mara tu baada ya uichaguzi kumalizika.

Amesema chama hicho kimeona kitumie utaratibu mpya na kuichagua Dar es Salaam hususan eneo la Mabibo kuwatangaza viongozi hao wapya.

Akitangaza matokeo, mwenyekiti wa kamati maalumu ya uchaguzi ya ACT-Wazalendo, Joran Bashange amesema mkutano mkuu wa nne wa chama hicho, uliokuwa ajenda ya uchaguzi ambapo Semu alichaguliwa kuwa KC kwa kura 354 (65.7) dhidi ya mpinzani wake, Mbarala Maharagande kura 184 (34.3). Idadi ya wajumbe walikuwa 538.

Bashange alisema kati ya wajumbe 538 waliopiga kura kumchagua Mwenyekiti, mbili ziliharibika huku kura 536 sawa na asilimia 99.6 zilikwenda kwa Othman.

Othman ambaye kitaaluma ni mwanasheria alikuwa akiwania nafasi hiyo pekee yake baada ya Juma Duni Haji maarufu Babu Duni aliyekuwa akitetea nafasi hiyo, kujitoa katika mchakato huo, siku moja kabla mdahalo ulioandaliwa baina yao.

Bashange amesema katika nafasi ya umakamu uenyekiti, Zanzibar Ismail Jussa aliibuka kidedea kwa kupata kura za  ndio 480 sawa na asilimia 94.2. Kama ilivyokuwa kwa Babu Duni, mpinzani wa Jussa,  Hijja  Hassan Hijja naye alijitoa.

Kwa upande wa Tanzania Bara, Bashange amesema wajumbe waliohudhuria  walikuwa 538, kura halali ni 517 na zilizoharibika ni 21 hivyo sawa asilimia 99.09 na Mchinjita alishinda nafasi hiyo.

Mwenyekiti mpya wa ACT-Wazalendo, Othman Masoud Othman akizungumza jambo na kiongozi wa chama hicho, Zitto Kabwe aliyemaliza muda wake.

Kibarua safu mpya

Viongozi wapya wa  ACT-Wazalendo, wanakabiliwa na majukumu mbalimbali mbele yao, ikiwemo kuhakikisha maridhiano baina yao na CCM yanakwenda kwa ufanisi, Zanzibar, kushinda uchaguzi wa serikali za mitaa, vijiji na vitongoji na uchaguzi mkuu wa mwaka 2025.

Pia, kufanya ziara katika maeneo mbalimbali kwa ajili ya kukiimarisha chama hicho, sambamba ya kuitangaza dira ya chao ya ‘Ahadi Yetu’ yenye lengo la kujenga Taifa la wote kwa maslahi ya wote.

Kabla ya kufanya mkutano huo, viongozi hao walifanya maandamano yaliyodumu umbali wa kilomita sita yakipita maeneo mbalimbali ikiwemo Ubungo, Urafiki Daraja la Kijazi, hatua iliyosababisha baadhi ya watumiaji wa barabara hizo kusubiri kwa muda ili kupisha msafara huo.

Maandamano hayo yalipita barabara za Sam Nujoma na Morogoro na kuhitimishwa Las Vegas Mabibo ambako kulifanyika mkutano kwa lengo la kutangaza matokeo uchaguzi na safu mpya ya viongozi waliochaguliwa.


Ifahamu safu mpya,

Dorothy Semu

Dorothy alizaliwa Julai 13, 1975 na kufanikiwa kupata elimu katika ngazi mbalimbali ikiwemo elimu ya sekondari katika Shule ya Weruweru na baadaye alijiunga na masomo ya kidato cha tano na sita shule ya Lutheran Junior Seminary kati ya mwaka 1993 – 1995.

Baada ya elimu ya sekondari, alijiunga na Chuo cha KCMC kwa masomo ya stashahada ya tiba mazoezi (physiotherapy) kati ya mwaka 1995 – 1998. Baadaye mwaka 2001 – 2002, alisoma shahada ya tiba mazoezi (Bsc.Physiotherapy) katika Chuo Kikuu cha Western Cape kilichopo Afrika Kusini.

Baada ya kumaliza masomo yake alifanya kazi katika Wizara ya Afya kama ofisa kwenye kampeni ya kutokomeza magonjwa ya ukoma na kifua kikuu. Hata hivyo, aliamua kuacha kazi mwaka 2015 ili awe huru kufanya siasa.

Baada ya kuingia kwenye siasa, aliamua kujiunga na chama cha ACT- Wazalendo ambacho wakati huo kilikuwa na mwaka mmoja tangu kilipopata usajili wa kudumu 2014 kama chama cha siasa Tanzania na huo ukawa ndiyo mwanzo wa safari yake kisiasa.

Ndani ya chama, Dorothy amekuwa Katibu Mkuu kuanzia mwaka 2017 – 2020, amekuwa makamu mwenyekiti kuanzia mwaka 2020 – 2024 na aliwahi kukaimu nafasi ya mwenyekiti kwa mwaka mmoja baada ya kifo cha Maalim Seif Sharif Hamad.

Vilevile, amekuwa akiongoza baraza kivuli lililoundwa na aliyekuwa Kiongozi wa Chama (KC), Zitto Kabwe, akiwa ni Waziri Mkuu kivuli tangu Februari 2022 - 2024. Sasa amechaguliwa kuiwa Kiongozi wa Chama akichukua nafasi ya Zitto. 


Othman Masoud Othman

Othman Masoud Othman alizaliwa Kijiji cha Pandani, wilaya ya Wete, mkoa wa Kaskazini Pemba, mwaka 1963, baba yake akiwa ni Sheikh Masoud Bin Othman.

Alipata elimu ya msingi katika shule ya Pandani na baadaye Sekondari ya Fidel Castro, Chake Chake, Kusini Pemba.

Baadaye alijiunga na Chuo Kikuu cha Dar es Salaam kwa Shahada ya Kwanza katika Sheria (LLB). Baada ya Chuo Kikuu alirejea Zanzibar na kuajiriwa na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar (SMZ) katika Wizara ya Katiba na Sheria kama Wakili.

Alikwenda kusoma Chuo Kikuu cha London ambako alipata shahada ya pili ya sheria (LL.M). Baada ya masomo aliteuliwa kuwa Katibu Mkuu katika Wizara ya Utawala Bora na Sheria chini ya Dk Salmin Amour, baadaye akawa Mkurugenzi wa Mashtaka Zanzibar chini ya Amani Karume na Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG) chini ya Dk Ali Mohamed Shein.
 

Kiongozi mpya wa ACT-Wazalendo, Dorothy Semu akifurahia na wanachama wengine baada ya kutangazwa kurithi nafasi iliyoachwa na mtangulizi wake Zitto Kabwe.

Wakati wa Bunge la Katiba, msimamo wake ulimfanya afukuzwe nafasi hiyo.

Agosti 2014 alijiunga na CUF hadi mwaka 2020 alipohamia ACT- Wazalendo. Hatimaye Machi 21, 2021 alitangazwa kuwa Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar akichukua nafasi ya Maalim Seif ambaye alifariki dunia Februari 17, 2021.

Januari 29, 2022, Othman alichaguliwa kuwa Makamu Mwenyekiti wa ACT Wazalendo (Zanzibar), nafasi anayoitumikia hadi Machi 6, 2024 kabla ya kuchaguliwa kuwa mwenyekiti wa chama hicho. Othman pia ni Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar.


Ismail Jussa

Jussa ni mmoja wa wanafunzi waaminifu wa aliyekuwa mwenyekiti wa ACT Wazalendo, Maalim Seif Sharif Hamad na alipohamia ACT- Wazalendo akitokea Chama cha Wananchi (Cuf), Jussa alihama naye.

Alizaliwa Agosti 18, 1971 huko Zanzibar na katika ujana wake alijikuta akiingia kwenye siasa za upinzani, wakati huo akiwa mwanachama wa CUF ambapo alifanikiwa kuwa mjumbe wa Baraza la Wawakilishi la Zanzibar.

Jussa alijitosa kugombea nafasi ya kiongozi wa chama dhidi ya Zitto kwenye uchaguzi wa Machi 2020, hata hivyo Zitto alichaguliwa kwa kipindi cha pili. Anaamini kwamba ana uwezo wa kukiongoza chama hicho.

Kabla ya Jussa kuchaguliwa kuwa Makamu Mwenyekiti-Zanzibar alikuwa mjumbe wa kamati kuu ya ACT Wazalendo. Amechukua nafasi ya Othman ambaye yeye amechaguliwa kuwa Mwenyekiti. Jussa ana uzoefu alioupata kutokana na nafasi mbalimbali alizokuwa nazo CUf.

Issihaka Mchinjita

Mchinjita alizaliwa January 9, 1983 huko Nyangao mkoani Lindi. Alifanikiwa kupata elimu ya msingi katika shule ya msingi Mahiwa kati ya mwaka 1992 – 1998 kabla ya kujiunga na shule ya sekondari Chidya Wavulana kati ya mwaka 1999 – 2002.

Baadaye mwaka 2003, kada huyo wa ACT Wazalendo alijiunga na sekondari ya Tosamaganga iliyopo mkoani Iringa kwa masomo ya kidato cha tano ambapo alihitimu mwaka 2005 kabla ya kujiunga na chuo cha ualimu cha Al Haramain na kufanikiwa kupata stashahada ya ualimu.

Kati ya mwaka 2017 – 2023, Mchinjita amesoma shahada ya sheria (LLB) katika Chuo Kikuu Huria cha Tanzania (OUT).

Kabla ya kuhamia ACT- Wazalendo mwaka 2019, Mchinjita alikuwa kada na kiongozi wa CUF ambapo amekitumikia chama hicho nafasi mbalimbali ikiwemo mwenyekiti wa Jumuiya ya Vijana wa CUF (Juvicuf) na mgombea ubunge wa CUF katika jimbo la Mtama katika uchaguzi wa mwaka 2015.

Vilevile, Mchinjita alikuwa mkurugenzi wa uchaguzi wa CUF katika wilaya ya Lindi kati yam waka 2014 – 2019 kabla ya kuhamia ACT- Wazalendo na kuchaguliwa kuwa mwenyekiti wa chama hicho mkoa wa Lindi, nafasi anayoitumikia hadi sasa.