VIDEO: Zitto awaaga ACT-Wazalendo akitaja yanayomsikitisha

Kiongozi wa ACT- Wazalendo Zitto Kabwe akizungumza katika Mkutano Mkuu wa chama hicho, jijini Dar es Salaam leo Machi 5, 2024. Picha na Michael Matemanga

Muktasari:

  • Machi 29, 2015, wajumbe wa Mkutano Mkuu wa ACT-Wazalendo walimchagua Zitto Kabwe kuwa Kiongozi wa Chama (KC). Wakafanya hivyo miaka mitano baadaye yaani 2020. Miaka tisa ametangaza kung’atuka na kuwaachia ujumbe viongozi watakaompokea.

Dar es Salaam. Safari ya miaka tisa ya Zitto Kabwe kuwa Kiongozi wa Chama (KC) wa ACT-Wazalendo inatamatika kesho Jumatano, Machi 6, 2024 kwa wajumbe wa mkutano mkuu kumchagua mrithi wake.

Kikiwa na mwaka mmoja tangu kuanzishwa Kwake 2014, Zitto akachaguliwa na wajumbe wa mkutano mkuu kuwa KC wa kwanza. Ametangaza kung’atuka kwa mujibu wa katiba ya chama hicho.

Leo Jumanne, Machi 5, 2024 katika siku ya kwanza ya mkutano mkuu, uliofanyika ukumbi wa mikutano ya Mlimani City, jijini Dar es Salaam, Zitto ametoa hotuba ya kuwaaga wajumbe hao na kuwashukuru jinsi walivyompa ushirikiano.


Hotuba yote ya Zitto aliyoitoa hii hapa-:

Nianze kwa kusema, uwingi wetu hapa leo, kukusanyika kwetu hapa leo, kwa mara ya kwanza, mkutano wetu mkuu kuwa na wajumbe kutoka kila Mkoa na kila jimbo la Tanzania, mikoa 39 ya Kichama na Majimbo 264 ya Uchaguzi kunatimiza ndoto yetu ya kuwa na chama kikubwa nchini Tanzania.

Chama chenye uwakilishi mpana Tanganyika na Zanzibar. Chama cha Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, kwa hakika.

Kiongozi wa Wapigania Haki wa Kimarekani Martin Luther King katika hotuba yake maarufu alisema “Ana ndoto” I have a Dream! Ndoto ya kuwa na Taifa la Wamarekani lisilo na Ubaguzi. Kukua kwa chama chetu ilikuwa ni ndoto na leo imetimia.

Lakini sio tu imetimia bali inadhihirisha kuwa suala sio kuwa na ndoto tu bali je ndoto yako ni kubwa kuweza kuwanufaisha wengine?

Je, ndoto yako shirikishi yaani inawahusisha watu wengine au ni ndoto binafsi isiyo na faida kwa wengine? Je unaiishi na kutekeleza ndoto yako? Haya ndio maswali muhimu katika kutimiza ndoto yako. Labda niwape hadithi ya chanzo cha ndoto hii!

Ndugu zangu, asubuhi hii naomba niwarudishe nyuma tarehe 23 Novemba 2013, katika Ukumbi wa Hoteli ya Blue Pearl pale Ubungo, walikukusanyika watu katika kikao halali kabisa na kutishwa na ndoto ya kijana mmoja kutoka Mwandiga, na wakatishika kwa sababu ndoto ya kijana huyu ni kubwa kiasi cha kuwatisha watu wazima wenye uwezo wa kifedha, elimu na mamlaka makubwa. Suluhisho la kutishwa na ndoto hiyo ni nini? Tumfukuze uanachama!

Mkutano mkuu wa ACT-Wazalendo

Ndoto ya kijana huyu aliyezaliwa kutoka katika mkoa masikini kabisa! Mtoto aliyezaliwa katika familia fukara! Mtoto aliyelelewa na mama mwenye ulemavu inataka kuzimwa na kundi la watu waoga waliotishwa na ukubwa wa ndoto.

Jitihada na kazi kubwa aliyoifanya kijana huyu kuishi na kuitekeleza ndoto yake toka akiwa na umri wa miaka 16 tu, inataka kukatizwa ikiwa bado haijatimia.

Ndugu zangu, katika chumba kile hakukuwa na chama tawala, hakukuwa na usalama wa Taifa, hakukuwa na Polisi tunaowatuhumu kila siku. Walikuwepo watu wazima waliotishiwa na ndoto kubwa.

Rais mstaafu wa Liberia Mwanamama Ellen Johnson Sirleaf aliwahi kusema “Kama Ndoto yako haikutishi, basi sio kubwa vya kutosha” If your dreams do not scare you, they are not big enough.

Kijana huyu si kwamba alikuwa na ndoto kubwa iliyomtisha yeye binafsi bali ilikuwa kubwa kiasi cha kuwatisha wengine. Na badala ya kushirikiana kuishi ndoto hiyo waliamua kujitoa katika ndoto hiyo.

Kijana yule kwa vile aliamini katika ndoto yake, hakukatishwa tamaa. Aliwashirikisha wengine ndoto yake na kwa pamoja wakaanza kuifanyia kazi ndoto ile. Ndoto bila kuifanyia kazi hata iwe kubwa kiasi gani inabaki kuwa ndoto tu. Lazima kuifanyia kazi ndoto yako.

Ishi ndoto yako maana yake ifanyie kazi ndoto yako. Itekeleze ndoto yako. Vijana wale walianzisha chama chao ili kiwe chombo cha kutekeleza ndoto yao, ndoto kubwa, ndoto shirikishi, ndoto ya kuona nchi yao inapata maendeleo, na watu wake wanapata maendeleo na kuishi kwa utu ndani ya Taifa lao. Walianzisha chombo ili Watanzania wapate sehemu ya kutekeleza ndoto zao.

Ndugu zangu, Taifa letu halina upungufu wa watu waoga wa ndoto kubwa. Mwaka 2017 watu waoga walifanya jitihada ya kuzima ndoto za wenzetu wengine.

Nguvu za watawala kwa kutumia Polisi wao, usalama wa taifa wao na Mahakama zao walijaribu kuzima ndoto za malaki ya watu ambao kwa robo karne walikuwa wanapambana kutaka demokrasia katika nchi yao, hususan upande mmoja wa Jamhuri yetu ya Muungano.

Ulipofika mwaka 2019 wenzetu wakaamua kujumuika nasi katika chombo chetu kuendeleza ndoto yao. Hatua ya wenzetu hawa kuchagua chombo chetu kama sehemu ya kutekeleza ndoto yao ni ishara kubwa kuwa ndoto hii ni kubwa na shirikishi.

Mwangwi wa Shusha Tanga Pandisha Tanga ukasikika kila kona ya Jamhuri yetu na nchi zetu mbili. Ndoto mbili zikaungana kuwa lindoto limoja likubwa, lililotamalaki kutoka fukwe za Ziwa Tanganyika mpaka Fukwe za Bahari ya Hindi, kutoka savana ya Serengeti mpaka kando kando ya Mto Ruvuma na kutoka Juu ya Mlima Kilimanjaro mpaka chini ya Bonde la Ufa.

Ndugu wajumbe leo nina furaha kubwa sana kuona ndoto yetu inatimia. Tumepata funzo kubwa kuwa lazima tuwe na ndoto kubwa. Lazima tufanyie kazi ndoto zetu.

Wito wangu kwa vijana wa Tanzania, haijalishi umezaliwa wapi, haijalishi hali ya familia yako, haijalishi vikwazo na magumu unayopitia, haijalishi jinsia, rangi, dini, hali yako kimaumbile, wala  unakatizwa tamaa kiasi gani ni lazima uwe na ndoto, uishi na kuifanyia kazi ndoto yako.

Kama mtoto kutoka katika mkoa masikini, familia fukara, aliyelelewa na mama mlemavu amefanikiwa basi Jiamini utafanikiwa.

Tusisahau maneno murua ya rafiki yangu Hakainde Hichilema ambayo yamejaa kwenye ukuta wa chumba chetu za mikutano kwamba kizazi kijacho hakitakumbuka tulianguka mara ngapi, bali tuliweza kuinuka mara ngapi kila tulipoanguka na kuendelea na mapambano.

Ndugu wajumbe, kwa kipindi cha miaka 10 tumejenga chama chetu kwa jasho na damu.

Katika kipindi hicho, pamoja na magumu yote tumekijenga chama chetu kutoka kuwa chama kidogo, mpaka kuwa chama cha kitaifa, kutoka chama cha mikoa michache mpaka chama chenye uongozi katika kila kijiji, kata, jimbo na mikoa yote ya Tanzania.

Naam tumejenga ACT kama chama pekee cha upinzani chenye uwakilishi mpana katika pande zote mbili za muungano. ACT Wazalendo inaweza tamba kuwa Chama cha Tanganyika na Zanzibar.

Siri ya mafanikio ya ujenzi huu, ni kutokuwa wabinafsi na wabaguzi. Narudia tumekijenga chama hiki kwa kutokuwa wabinafsi na wabaguzi. Viongozi na wanachama wote kwa pamoja hatukuwa wabinafsi na wabaguzi.

Tulijitolea muda wetu, baadhi yetu waliacha ajira zao. Vijana wengine kwa makumi hawakwenda kuajiriwa, ili kukitumikia chama bila kujifikiria wao binafsi wala familia zao na watoto wao.

Wengine wamejitolea fedha na mali bila kujitazama wao. Kuna waliojitolea uhai wao wakauwawa kwa kukipigania chama hiki.

Wapo walioteswa na kupewa vilema vya maisha, wapo walio fungwa jela kwa kuipigania ACT Wazalendo na kile Chama inachoamini. Hawa wote Hawakuwa wabinafsi.

Hawakujitazama wao, hawakuangalia malengo yao ya kiuchumi, kijamii au kisiasa. Walijitoa kwaajili ya chama.

Wanachama wa ACT-Wazalendo wakiburudika leo Machi 5, 2024 katika mkutanoo mkuu wa chama hicho uliofanyika katika ukumbi wa Mlimani City jijini Dar es Salaam. Picha na Michael Matemanga

Hakika majina yao yataandikwa, au niseme yameshaandikwa kwa wino wa dhahabu katika chama na katika mioyo yetu. Mimi kiongozi wenu nimewaandika kwa wino wa moto katika moyo wangu.

Katika siku 7 zilizopita chama chetu kimelidhihirishia Taifa kuwa ni chama chenye demokrasia kubwa nchini Tanzania. Taifa limeshuhudia demokrasia ikijengwa ndani ya chama.

Tumelionyesha taifa namna gani uchaguzi unafanyika ndani ya chama. Tumeonyesha kampeni za kistaarabu katika ngazi zote kuanzia uchaguzi wa ngome za chama.

Tumeona midahalo ya wagombea wakijinadi wao na chama chao. Hakuna chama Tanzania chenye uthubutu wa kufanya hivyo zaidi ya ACT Wazalendo.

Hakika tumelidhihirishia Taifa kuwa chama chetu kinafuata misingi ya demokrasia na kinaishi misingi ya kuanzishwa kwake.

Mimi kama kiongozi wenu ninayemaliza muda wangu nimejitahidi kuilinda demokrasia hiyo kwa vitendo. Kuagwa kwangu leo ni ushuhuda wa hilo. Baada ya kuongoza kwa muongo mmoja katiba inanitaka kuondoka na mimi mwenyewe nataka kuondoka ili niwaachie wengine watuongoze. Uongozi ni kama mbio za kupokezana vijiti ni lazima kupokezana.

Nimesema chama chetu ni cha kidemokrasia, hii haimaanishia katika kipindi chake hatujakutana na matatizo.

Lakini katika nyakati za mapito magumu tuliweka ubinafsi nyuma tukakataa ubaguzi, tukafuata misingi ya demokrasia na kuvuka salama. Hata pale mwenyekiti wetu Maalim Seif alipotutoka tulifaulu mtihani ule.

Lakini tunafahamu mitihani ni mingi mbele yetu na tunakazi ya kufanya. Na sote tunajua “We win where we work and work where we win.” Tutashinda!

Ndugu wajumbe wa mkutano mkuu, Mkutano huu ni mkutano wa uchaguzi. Watu waoga wa ndoto kubwa huwa wanatumia uchaguzi kufarakanisha watu na kuua ndoto zao.

Nawaasa wagombea wote katika uchaguzi huu katika nafasi zote, waogope na kujiepusha na kauli zenye kuchochea ubaguzi. Kila mmoja ndani yake awe na hofu ya kumaliza uchaguzi huu akiwa adui wa mgombea mwenzake. Kutofautiana kimawazo na maoni ni msingi wa demokrasia.

Lakini kutofautiana huko kimawazo na maoni kunakojikita katika ubaguzi na ubinafsi kutakibomoa chama. Lazima tuishi kwa kupendana, kuheshimiana na kuheshimu mawazo ya wengine. Dr King alisema “we must learn to live together as brothers, or we will perish as fools.”

Ndani ya masaa 24 toka sasa, chama chetu kitapata kiongozi mpya wa chama, mimi binafsi naahidi kufanya kazi naye na kumpa ushirikiano wote. Niwaase nanyi kumpa ushirikiano. Mimi naondoka katika nafasi yangu kama kiongozi wa chama.

Imekuwa ni fahari na heshima kubwa kwangu kufanya kazi kama Kiongozi wenu. Nimekuwa na wakati mzuri na wakati mgumu katika kazi yangu. Kuna wakati nimekuwa na furaha na wakati nimekuwa na huzuni.

Lakini katika nyakati zote hizo nimetiwa moyo na dhima kubwa inayobebwa na chama chetu. Wakati wote nimekuwa nimefarijiwa na mapenzi makubwa na upendo wa wanachama.

Mapenzi yenu na upendo kwa chama umeniinua katika nyakati ngumu za kiuongozi. Najiona mwenye baraka kuwa kiongozi wa chama hiki ninachokipenda. Ni fahari kubwa kuwa kiongozi wa kwanza wa chama. Siku zote nitakuwa mwenye shukrani kupewa nafasi hii.  

Ndugu wajumbe, ninamaliza muda wangu wa uongozi kukiwa na changamoto nyingi mbele yetu.

Bado hatujapiga hatua vya kutosha katika kujenga maridhiano Zanzibar na kuondokana na utamaduni wa watu kupoteza maisha kila mwaka wa uchaguzi.

Nikiwa kiongozi nimejitahidi kwa hali na mali kwa kushirikiana na viongozi wenzangu kupata ufumbuzi wa mageuzi ya msingi Zanzibar.

Nasononeka sana kuwa juhudi zetu hazileti matunda. Nilikiongoza chama chetu kufanya maamuzi magumu sana ya kukubali kushiriki katika Serikali ya Umoja wa Kitaifa Zanzibar ili kushirikiana na wenzetu kupata jawabu la kudumu la hali ya Zanzibar. Naondoka kwenye uongozi nikiwa sijafanikiwa. Wenzangu wanaochukua jukumu hili nawaachia mzigo ambao nilipaswa kuwa nimeumaliza.

Naomba niwasihi viongozi wa Serikali zote mbili, Serikali ya Muungano na Serikali ya Zanzibar tumalize huu mzunguko wa mauaji kila miaka mitano. Uchaguzi ujao Wazanzibari waende kupiga kura zao bila kupoteza maisha yao. Inatosha, inatosha inatosha.

Ndugu wajumbe wa Mkutano Mkuu, najua kuwa mna hamu ya kupiga kura na kuchagua viongozi wengine watakaotuvusha katika hatua tunayokwenda sasa. Huu ni mwaka wa uchaguzi kwa upande wa Tanzania Bara, Uchaguzi wa Serikali za mitaa, vijiji na vitongoji.

Sasa hatuna sababu tena ya kutokuwa na wagombea katika kila eneo linalogombewa uchaguzi. Chama chetu kimetumia vizuri miaka miwili ya utulivu wa kisiasa nchini kujenga muundo wake kuanzia chini.

Hatukutaka kupoteza muda bali tulitumia vizuri fursa ya kufunguliwa kwa siasa kujenga chama chetu tangu mwaka 2022. Nendeni mkahakikishe tunashinda vijiji, mitaa na vitongoji ili tuweze kujipanga vizuri kwa uchaguzi mkuu wa mwaka 2025.

Kwa wanachama wote wa ACT Wazalendo kwa mara ya mwisho kama kiongozi wa chama nasema ahsanteni sana.

Mungu awabariki. Ahsanteni kwa kunisikiliza.