Kinana aeleza dhamira ya CCM, Serikali katika chaguzi zijazo

Makamu Mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi (CCM) Bara, Abdulrahman Kinana akizungumza katika Mkutano Mkuu wa ACT- Wazalendo jijini Dar es Salaam leo Machi 5, 2024. Picha na Michael Matemanga


Muktasari:

 Kinana pia, amempongeza Zitto Kabwe anayemaliza muda wake kwa uongozi mzuri na madhubuti wenye busara


Dar es Salaam. Makamu Mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi (CCM-Bara), Abdulrahman Kinana amewahakikisha Watanzania kwamba uchaguzi wa Serikali za mitaa na Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2025 utakuwa huru na haki.

Amesema pia, Rais Samia Suluhu Hassan na Serikali wana dhamira ya dhati ya kuhakikisha mchakato huo unakuwa huru na haki ili watu wapate fursa ya kuwachagua viongozi wanaotaka.

Kinana ameeleza  hayo leo Jumanne Machi 5, 2024 akimwakilisha Rais Samia katika Mkutano Mkuu wa nne wa ACT- Wazalendo, uliofanyika Mlimani City Dar es Salaam.

"Kuna sheria na dhamira, unaweza kuwa na sheria nzuri, lakini kama huna dhamira nzuri unaweza kuikanyaga hiyo sheria kama unavyotaka. Unaweza kuwa na dhamira nzuri na sheria mbaya lakini dhamira ikitawala mambo yatakuwa mazuri.

"Niwahakikishie, Rais Samia ameamua uchaguzi wa mwaka huu na ujao unakuwa huru na haki, ninazungumza hili nina uhakika wapo wenye shaka na kauli hii, lakini wanazo sababu zinatokana na mwaka 2019 na mwaka 2020," amesema Kinana huku akipigiwa makofi na wanachama wa ACT.

Katika uchaguzi wa Serikali za mitaa, vitongoji na vijiji mwaka 2019 wagombea wengi wa CCM walipita bila kupingwa kama ilivyokuwa katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2020 ambao chama tawala kilinyakua viti vingi vya udiwani, uwakilishi, ubunge na urais.

Mchakato huo ulilalamikiwa na vyama vya upinzani waliodai haukuwa wa haki huku wagombea wao wakienguliwa pasipo sababu za msingi.

Kitendo hicho kilifanya baadhi ya vyama vya upinzani kususia shughuli zinazoandaliwa na Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa.

Katika maelezo yake, Kinana amesema sheria ya awali iliwezesha wabunge na madiwani wa upinzani kuingia kwenye vikao vya uamuzi.

"Lazima tuseme ukweli hofu viongozi wenzangu wa vyama vya siasa, na asasi za kiraia na viongozi wa dini msingi wa hofu yao ni yale yaliyojitokeza mwaka 2019/20, naomba nikiri Rais Samia ameamua uchaguzi wa mwaka huu na mwaka 2025 utaachwa ili wapigakura wafanye uamuzi wao," amesema Kinana.

Amesema kwa namna Bunge lilivyofanya marekebisho ya sheria tatu ikiwamo ya uchaguzi ni kutokana na dhamira ya Rais Samia, ndio maana miswada hiyo ilipewa muda mrefu ili kusikiliza na kuchukua maoni ya wabunge.


Kuhusu ACT-Wazalendo

Katika hatua nyingine, Kinana ambaye amewahi kuwa katibu mkuu wa CCM, amekipongeza chama hicho ambacho kwa miaka michache kimekua na kusambaa katika maeneo mbalimbali.

"Tumekuwa tukiwafuatilia sisi kama CCM hatuwachukulii kirahisi," amesema huku akiendelea kupigiwa makofi.

Mbali na hilo, mwanasiasa huyo mkongwe amesema kila inapotokea nafasi ya kuunga Serikali ya Umoja wa Kitaifa Zanzibar (SUK), ACT - Wazalendo imekuwa ikiweka mbele masilahi ya wananchi na kushiriki mchakato huo.


"CCM inatambua ushirika wenu wa Umoja wa Kitaifa, tupo tayari kukaa nanyi na kusikilizana kutafuta haki, uhuru na maendeleo ya wananchi wa Zanzibar, nawapongeza kwa namna mnavyoendelea kukiimarisha chama.

"Mmepitia kwenye mambo mawili kwanza ni shusha tanga na pandisha tanga, mmefanya bila mfarakano na kazi ikaendelea haikuwa jambo rahisi," amesema Kinana.

Amesema jambo jingine ni kuondokewa na mwenyekiti wao marehemu Maalim Seif Sharif Hamad aliyekuwa nguzo ndani ya ACT- Wazalendo.

Lakini walivuka salama kwa sabubu Maalim Seif alijenga taasisi hakujenga mtu na ACT- Wazalendo imeendele kuwa imara.


Ampongeza Zitto

Katika hotuba yake, Kinana amempongeza Zitto Kabwe (Kiongozi wa ACT) anayemaliza muda wake kwa uongozi mzuri na madhubuti wenye busara na kukiwezesha chama hicho kuwa na hali ya utulivu.

"Sio hilo tu, umekubali kuzingatia matakwa ya katiba ya mihula miwili umeamua kukaa pembeni sio kustaafu Zitto hastaafu, anakaa pembeni, atakuwa mshauri mzuri wa chama chenu.

Kiongozi wa ACT- Wazalendo Zitto Kabwe akizungumza katika Mkutano Mkuu wa chama hicho, jijini Dar es Salaam leo Machi 5, 2024. Picha na Michael Matemanga

"Lazima nikiri nimefanya kazi kwa ukaribu na Zitto kupitia Kituo cha Demokrasia Tanzania (TCD) kwa ajili ya kujenga demokrasia, namshukuru sana nitachota ushauri wako wa mara kwa mara," amesema Kinana.

Pia, amempongeza mwenyekiti anayemaliza muda wake Juma Duni Haji akisema uamuzi wake wa kujiondoa kwenye mchakato wa kuwania uenyekiti unaonyesha anajalia masilahi ya Taifa kuliko yeye mwenyewe.