Rais Samia ajifunga kitanzi cha haki chaguzi zijazo

Muktasari:

  • Kwa mujibu Kinana,­­­ Serikali ya CCM inayoongozwa na Rais Samia,  ina dhamira ya dhati kwenye uchaguzi wa Serikali za mitaa mwaka huu na uchaguzi mkuu mwakani

Dar es Salaam. Wakati vyama vya siasa na wadau wa demokrasia nchini wakiendelea kujiandaa kwa uchaguzi wa Serikali za mitaa mwaka huu na Uchaguzi Mkuu mwakani, Makamu Mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi (CCM) Bara, Abdulrahman Kinana amesema Serikali itahakikisha chaguzi hizo zinakuwa huru na haki.

 Kinana amesema Rais Samia Suluhu Hassan ana dhamira ya dhati kuhakikisha uamuzi utakaofanywa na wananchi katika chaguzi hizo unaheshimika akisisitiza licha ya uwepo wa sheria, dhamira ya mkuu wa nchi ni kuona uhuru na haki unashamili.

Kinana ametoa hakikisho hilo mbele ya wajumbe wa mkutano mkuu wa nne wa ACT-Wazalendo leo Jumanne, Machi 5, 2024 katika mkutano wa Mlimani City, Dar es Salaam ambao unamalizika kesho Jumatano, Machi 6, 2024 kwa kufanyika kwa chaguzi wa viongozi ngazi ya juu.

Mbali na kauli hiyo ya Kinana aliyosema ni salamu za Rais Samia, Kiongozi wa chama hicho anayemaliza muda wake, Zitto Kabwe alitumia fursa hiyo kuwaaga wajumbe wa mkutano huo baada ya kuwaongoza kwa miaka tisa.

Katika salamu za Zitto aliwaeleza wajumbe masikitiko yake ya kung’atuka kwenye nafasi hiyo akiacha changamoto ikiwamo kujenga maridhiano Zanzibar na kuondokana na utamaduni watu kupoteza maisha kila mwaka wa uchaguzi.

Zitto amewataka viongozi watakaopata dhamana kupitia uchaguzi huo kuendeleza maridhiano hayo baina ya ACT-Wazalendo na CCM wanaounda Serikali ya Umoja wa Kitaifa (SUK).

Mkutano mkuu wa ACT-Wazalendo

Hakikisho la Rais Samia

Akitoa hotuba kwa niaba ya Rais Samia, katika mkutano huo, Kinana amesema mkuu huyo wa nchi amedhamiria kuhakikisha mchakato wa chaguzi zijazo unakuwa huru na haki.

“Serikali ya CCM inayoongozwa na Rais Samia ina dhamira ya dhati kwenye uchaguzi wa Serikali za mitaa mwaka huu na uchaguzi mkuu mwakani kuhakikisha tunakuwa na uchaguzi ulio huru na haki,” amesema Kinana huku akishangiliwa

 “Kuna sheria na kuna dhamira, unaweza kuwa na sheria nzuri, lakini kama huna dhamira nzuri unaweza kuikanyaga hiyo sheria ukafanya unavyotaka. Unaweza kuwa na dhamira nzuri na sheria mbaya lakini dhamira ikitawala mambo yatakuwa mazuri.”

Katika msisitizo wake huku akishangiliwa, Kinana amesema,"nataka niwahakikishie Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ameamua uchaguzi wa mwaku huu na mwaka ujao unakuwa huru na haki.”

Amesema wakati anazungumza hivyo ana uhakika wako ambao wana shaka na kauli hii, na hao wenye mashaka wanazo sababu na sababu zao zinatokana na 2019 na 2020 huo ndio ukweli.”

Amesema sheria tulizokuwa nazo za uchaguzi zilizotupeleka kwenye uchaguzi 2015 ziliwezesha wanachama kutoka wa upinzani 117 kuingia bungeni.

 Sheria hiyohiyo iliwezesha karibu madiwani asilimia 40 kuingia katika nafasi za halmashauri.

“Tulipokuja 2020 kusema kweli lazima tuseme ukweli hofu ya Watanzania, hofu ya wenzangu vyama vya siasa, asasi za kiraia, baadhi ya viongozi wa dini, msingi wa hofu yao ni yale yaliyotokea 2019.

Niwahakikishie Rais Samia Suluhu Hassan ameamua uchaguzi wa mwaka huu na ujao utaachwa ili wapiga kura uamuzi wao ndio utoe tafasiri kwenye uchaguzi ujao,” amesema Kinana.

Katika uchaguzi wa serikali za mitaa, vitongoji na vijiji mwaka 2019 wagombea wengi wa CCM walipita bila kupingwa kama ilivyokuwa katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2020 ambao chama hicho tawala kilinyakuwa viti vingi vya udiwani, uwakilishi, ubunge na urais.

Mchakato huo ulilalamikiwa na vyama vya upinzani na wadau wa demokrasia waliodai haukuwa wa haki huku wagombea wao wakienguliwa pasipo sababu za msingi.

Kitendo hicho kilifanya baadhi ya vyama vya upinzani kususia shughuli zinazoandaliwa na Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa kikiwemo Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema).


Kuhusu ACT-Wazalendo

Katika hatua nyingine, Kinana ambaye aliwahi kuwa katibu mkuu wa CCM, alikipongeza chama hicho kilichoanzishwa mwaka 2014 ambacho kwa miaka michache kimekua na kusambaa katika maeneo mbalimbali kimekuwa chama cha hoja sio vioja.

"Tumekuwa tukiwafuatilia sisi kama CCM hatuwachukulii kirahisi," amesema huku akiendelea kupigiwa makofi.

Mbali na hilo, mwanasiasa huyo mkongwe amesema kila inapotokea nafasi ya kuunga Serikali ya Umoja wa Kitaifa Zanzibar (SUK), ACT - Wazalendo imekuwa ikiweka mbele masilahi ya wananchi na kushiriki mchakato huo.

"CCM inatambua ushirika wenu wa Umoja wa Kitaifa, tupo tayari kukaa nanyi na kusikilizana kutafuta haki, uhuru na maendeleo ya wananchi wa Zanzibar, nawapongeza kwa namna mnavyoendelea kukiimarisha chama.

"Mmepitia kwenye mambo mawili kwanza ni shusha tanga na pandisha tanga, mmefanya bila mfarakano na kazi ikaendelea haikuwa jambo rahisi," amesema Kinana.

Wanachama wa ACT-Wazalendo wakiburudika leo Machi 5, 2024 katika mkutanoo mkuu wa chama hicho uliofanyika katika ukumbi wa Mlimani City jijini Dar es Salaam. Picha na Michael Matemanga

Amesema jambo jingine ni kuondokewa na mwenyekiti wao marehemu Maalim Seif Sharif Hamad aliyekuwa nguzo ndani ya ACT- Wazalendo, lakini walivuka salama kwa sababu Maalim Seif alijenga taasisi hakujenga mtu na ACT- Wazalendo imeendelea kuwa imara.

Katika hotuba yake, Kinana amempongeza Zitto anayemaliza muda wake kwa uongozi mzuri na madhubuti wenye busara na kukiwezesha chama hicho kuwa na hali ya utulivu.

"Sio hilo tu umekubali kuzingatia matakwa ya katiba ya mihula miwili umemua kukaa pembeni sio kustaafu Zitto hastaafu, anakaa pembeni, atakuwa mshauri mzuri wa chama chenu.

"Lazima nikiri nimefanya kazi kwa ukaribu na Zitto kupitia Kituo cha Demokrasia Tanzania (TCD) kwa ajili ya kujenga demokrasia, namshukuru sana nitachota ushauri wako wa mara kwa mara," amesema Kinana.

Amempongeza mwenyekiti anayemaliza muda wake Juma Duni Haji akisema uamuzi wake wa kujiondoa kwenye mchakato wa kuwania uenyekiti unaonyesha anajalia masilahi ya Taifa kuliko yeye mwenyewe.


Zitto alivyowaaga

Zitto akizungumzia kauli ya Kinana amesema, "Kinana ni muungwa, waungwana huwaheshimiwi kwa jambo lolote isipokuwa kauli zao, hii kauli tunaishika na akienda kinyume tutakwenda nyumbani kwakwe napajua, nitamwabia ulisema hivi mbona bado yale yale ya mwaka 2019 na 2020.

"Namfahamu Kinana ni mtu muungwa na neno lake naamini kabisa alichotueleza ndiocho kitakachokuwa," amesema Zitto.

Katika hatua nyingine, Zitto amemuomba Kinana kuzungumza na Rais wa Zanzibar, Dk Hussein Mwinyi ili kumaliza sintofahamu ya mabadiliko na mageuzi ya sheria mbalimbali ikiwamo za uchaguzi kama ilivyokuwa Tanzania Bara.

"Mheshimiwa Kinana mwambie Rais Mwinyi akunjue mikono tumalize mageuzi yanayotakiwa Zanzibar," amesema Zitto.

Pia, amesema viongozi wa chama hicho, wamejitoa sadaka kuhusu mchakato wa mageuzi lakini viongozi wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar wamekunja mikono.

“Nikiwa kiongozi nimejitahidi kwa hali na mali kwa kushirikiana na viongozi wenzangu kupata ufumbuzi wa mageuzi ya msingi Zanzibar. Nasononeka sana kuwa juhudi zetu hazileti matunda.

“Nilikiongoza chama chetu kufanya uamuzi mgumu sana wa kukubali kushiriki katika Serikali ya Umoja wa Kitaifa Zanzibar ili kushirikiana na wenzetu kupata jawabu la kudumu la hali ya Zanzibar. Naondoka kwenye uongozi nikiwa sijafanikiwa,” amesema Zitto.

 “Viongozi wenzangu wanaochukua jukumu hili nawaachia mzigo ambao nilipaswa kuwa nimeumaliza. Naomba niwasihi viongozi wa Serikali zote mbili, Serikali ya Muungano na Serikali ya Zanzibar tumalize huu mzunguko wa mauaji kila miaka mitano (kunapotokea uchagazi).

“Uchaguzi ujao Wazanzibari waende kupiga kura zao bila kupoteza maisha yao. Inatosha, inatosha inatosha,” amesema Zitto.

Kiongozi wa ACT-Wazalendo, Zitto Kabwe akizungumza katika mkutano Mkuu wa chama hico uliofanyika leo Machi 5, 2024 katika ukumbi wa Mlimani City jijini Dar es Salaam. Picha na Michael Matemanga

Mbunge huyo wa zamani wa Kigoma Kaskazini na Kigoma Mjini amesema anamaliza muda wake wa uongozi wa miaka tisa katika chama hicho

kikiwa kinaishi misingi ya kidemokrasia na kinaishi misingi ya kuanzishwa kwake.

"Nimejitahidi kulinda demokrasia hiyo kwa vitendo kwa miaka tisa ndani ya saa 24 kuanzia sasa chama chetu kitapata kiongozi mpya wa chama naahidi kutoa ushirikiano kwake na milango itakuwa wazi," amesema.

Zitto anamaliza muda wa uongozi wake baada ya kuhudumu kwa miaka tisa katika nafasi hiyo na wanaotajwa kumrithi ni Dorothy Semu na Mbarala Maharagande.

Wawili hawa wanatarajiwa kuchuana kesho, wajumbe wa mkutano mkuu watapiga kura nani achukue mikoba ya Zitto.

Semu ni kiongozi mzoefu ndani ya ACT- Wazalendo, akishika nafasi za idara ya fedha, ukaimu katibu mkuu, kaimu mwenyekiti wa chama, makamu mwenyekiti bara na waziri mkuu kivuli wa chama hicho.

Wakati Maharagande ni mzoefu katika masuala ya siasa takribani miaka 25, akianzia CUF kisha kuhamia ACT -Wazalendo mwaka 2018 na kushika nafasi mbalimbali ikiwamo ya Uwaziri Kivuli wa Katiba na Sheria na Katibu wa Idara ya Haki za Binadamu.

Nafasi ya mwenyekiti imebaki na mgombea mmoja aliyekuwa Makamu Mwenyekiti wake-Zanzibar, Othuman Masoud Othuman. Pia, ni Makamu wa Kwanza wa Rais Zanzibar. Amebaki pekee baada ya Juma Duni maarufu ‘Babu Duni’ kutangaza kujiondoa.

Nafasi ya makamu mwenyekiti bara ni Isihaka Mchinjita na Ismail Jussa upande wa Zanzibar, wote hawana wapinzani.


Waichambua kauli ya Kinana

Mchambuzi wa masuala ya siasa, Thabiti Mlangi amesema siku zote mabadiliko yanaanzia na dhamira inayoleta mabadiliko na Rais Samia ameonyesha kiongozi anayependa haki, ndio maana aliunda kikosi kazi cha wadau wa demokrasia ili kukusanya maoni ya kuboresha sheria za uchaguzi.

"Yote yaliyotokea nyuma huwezi kuwa na wasiwasi na kauli ya makamu mwenyekiti ( Kinana) kwa sababu matendo yanaongea mengi kuliko maneno. Rais Samia ameunda kikosi kazi, sheria za uchaguzi zimefanyiwa maboresho, kilichobaki kwenda katika uchaguzi wenyewe," amesema Mlangi.

Mchambuzi wa siasa mwingine, Ramadhan Manyeko amesema sheria na dhamira zinaweza kuwa nzuri kinachobakia ni utashi kwenye mamlaka au wanaopewa jukumu la kusimamia mchakato huo.

"Kinachonipa wasiwasi kuna chaguzi ndogo zimepita na Rais akiwa Samia kuna mambo yaliyotokea mwaka 2020 ikiwamo mawakala kuzuiwa kwa muda bado yanaendelea kujitokeza.Tunataka dhamira anayoisema ionekana kwa vitendo kwa sababu matukio yanaendelea.

"Kinachotakiwa haya maelekezo na dhamira njema yashushwe hadi kwa watendaji wa chini, ili mchakato uwe wa ufanisi," amesema Manyeko.

Makamu Mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi (CCM) Bara, Abdulrahman Kinana akizungumza katika Mkutano Mkuu wa ACT- Wazalendo jijini Dar es Salaam leo Machi 5, 2024. Picha na Michael Matemanga


Kwa upande wake, Nassor Seif Amour ambaye pia ni mchambuzi wa siasa, amesema kauli ya Kinana ni nzuri, lakini ili itekelezwe kwa ufanisi na kuwe na uchaguzi huru na haki basi ingeanzia kwenye vyama.

"Humu katika vyama vya siasa kuna wagombea wanapatikana kwa njia isiyo huru na haki kwenye kura za maoni. Bado kutakuwa na tatizo, unarekebisha huku lakini wanaoingia madarakani ni wale wanaovuruga wananchi," 

"Kuna Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) ianze kusimamia vyama hasa katika upatikanaji wa wagombea kwa sababu wenye vyeo ndio wanaotumia nguvu, kama tunataka uchaguzi huru na haki tuanzie kwenye vyama vya siasa," amesema Amour.


Ni mkutano wa kipekee

Katibu Mkuu wa ACT- Wazalendo, Ado Shaibu amesema mkutano mkuu huo wa nne ni tofauti na mikutano mitatu iliyopita tangu kuanzishwa kwa chama hicho mwaka 2014. Amesema mkutano wa mwaka huu umejumuisha wajumbe wengi kutoka kila kona ya Tanzania.

Ado amesema kwa mara ya kwanza mkutano huo umehudhuriwa na wajumbe wa 604 kutoka majimbo 264 ya Tanzania Bara na Zanzibar pamoja na mikoa yote ya kichama 39 ya chama hicho kikuu cha upinzani.

"Jitihada kubwa za viongozi kufanya kazi bila kuchoka zimechangia chama kukua na kuenea katika maeneo mbalimbali kwa muda mfupi, tumechora ramani yetu ya siasa, tupo tayari kwa uchaguzi wa Serikali za mitaa na uchaguzi mkuu wa mwaka 2025 kutokana na kuwa na muundo madhubuti wa kiungozi," amesema Ado


Alichokisema Martha Karua

Mgeni rasmi wa mkutano huo alikuwa, Martha Karua, aliyekuwa mgombea umakamu wa Rais wa Kenya kwa tiketi ya Muungano wa Azimio.

 Katika hotuba yake amesema hatua ya ACT -Wazalendo kuandaa mkutano huo na kuwaalika viongozi wa vyama vingine inaonyesha siasa sio uadui.

Karua amesema Tanzania kuna vyama vya siasa vinavyokuwa na kuwa demokrasia tofauti na Kenya ambapo vyama vinakuwa na kuleta watu pamoja nyakati za uchaguzi ambao ukiisha vyama vinaishia.

"Tunaomba kuiga mfano wenu kuwa, safari ya kushinda uongozi isififie kwa kukosa kura za kutosha, ni jukumu ka vyama kuelimisha wananchi na kuweka hoja au mjadala ili kujua kila mpiga kura kazi yake ni ipi," amesema Karua.


Msajili wa vyama vya siasa

Msajili Msaidizi wa Vyama vya Siasa, Sisty Nyahoza amempongeza Zitto kwa kumaliza muda wake wa uongozi, akisema amejenga taasisi inayokwenda vizuri. Amesema ACT- Wazalendo ni miongoni mwa vyama vinavyofanya siasa za kistaharabu.

"Tumekuwa tukifuatilia mchakato wa uchukuaji na urejeshaji wa fomu, tumeona demokrasia inavyofanya kazi na kanuni zinavyofuatwa ndani ya ACT- Wazalendo. Ofisi ya Msajili imefuatilia maandalizi ya mkutano na tunafarijika mnaheshimu na kufuata katiba yenu," amesema Nyahoza.

Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Kituo cha Demokrasia Tanzania (TCD), Benadeta Kafuko amesema,"Zitto ni shujaa kwetu TCD amejitahidi kuipigania taasisi hadi hapa ilipo nakuahidi tutasimamia maono yako."