Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Wasira aiagiza Samwasa kuharakisha usambazaji wa maji Same mjini

Makamu Mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi (CCM), Tanzania Bara, Stephen Wasira wakati akizungumza leo Juni 8, 2026 katika mkutano wa shina namba tisa, tawi la Same mjini, katika kata ya Same, wilayani humo.

Muktasari:

  • Wasira amesema Serikali imetoa fedha zaidi ya Sh1.57 trilioni kwa ajili ya kutekeleza miradi mbalimbali ya maendeleo ikiwemo katika sekta ya maji.

Same. Makamu Mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi (CCM), Tanzania Bara, Stephen Wasira ameiagiza Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Same - Mwanga (Samwasa) kuharakisha uwekaji wa mfumo wa usambazaji wa maji safi na salama katika maeneo yenye changamoto ya upatikanaji wa huduma hiyo, Wilaya ya Same mkoani Kilimanjaro.

Amesema Serikali imetoa fedha zaidi ya Sh1.57 trilioni kwa ajili ya kutekeleza miradi mbalimbali ya maendeleo ikiwemo katika sekta ya maji.

Maagizo hayo ameyatoa leo Juni 8, 2026 wakati akishiriki mkutano wa shina namba tisa, tawi la Same mjini, katika kata ya Same, wilayani humo.

“Katika Mkoa wa Kilimanjaro, kwa kipindi cha miaka mitano ya Rais Samia Suluhu Hassan, tumewekeza Sh1.57 trilioni kwenye shughuli za maendeleo ikiwa ni pamoja na maji. Sasa maji yapo Same, ambacho hakijakuwepo ni mifereji mipya ya kusambaza maji,” amesema.

Ameongeza kuwa: “Sasa nawaambia watu wa maji, maji ya Same hayawezi kuwa na maana kama watu wa Same hawapati huduma hiyo, kwa hiyo tunawaelekeza kutoka shina namba tisa waharakishe mfumo wa kusambaza maji ili watu wapate maji, wasiwe wanayasikia, wawe wanayaona, kuyanywa na kuyaoga.”

Akizungumzia kero ya upatikanaji wa maji katika mkutano huo, mmoja wa wananchi wa shina namba tisa, Ibwe Shaban amesema licha ya kukamilika kwa miradi ya maji wilayani humo, wananchi bado hawapati huduma hiyo ipasavyo kutokana na ubovu wa miundombinu ya usambazaji huduma hiyo.

Amesema wilaya hiyo ina maji ya kutosha, lakini changamoto ipo kwenye miundombinu chakavu inayosababisha maji kupotea njiani kabla ya kuwafikia wananchi.

“Tumepata maji ya kutosha katika wilaya yetu na tunashukuru sana. Miundombinu ya maji ni chakavu, maji yanatoka lakini yanaishia porini huku sisi wananchi tukishindwa kuyapata kutokana na kukosekana kwa mfumo bora wa usambazaji wa maji,” amesema Ibwe.

Mkazi mwingine wa eneo hilo, Rose Mmbaga ameiomba Serikali pamoja na mamlaka husika kuchukua hatua za haraka kuhakikisha huduma ya maji safi na salama inawafikia wananchi katika maeneo yao, akieleza kuwa baadhi ya wakazi bado wanakabiliwa na ukosefu wa huduma hiyo.

Amesema changamoto hiyo imekuwa ikiathiri maisha ya kila siku ya wananchi, hivyo kuna umuhimu wa kuimarisha miundombinu ya usambazaji wa maji ili huduma hiyo iwafikie wote kwa wakati na kwa uhakika.