Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Wasira aagiza kuvunjwa makundi ya WhatsApp yanayochochea migogoro CCM

Makamu Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Tanzania Bara, Stephen Wasira, akizungumza na wanachama wa CCM Wilaya ya Moshi Mjini pamoja na viongozi wa mabaraza ya jumuiya na wazee wa chama hicho, katika ofisi za CCM Mkoa wa Kilimanjaro, ambapo alisisitiza mshikamano, uhai wa chama na utekelezaji wa majukumu ya kisiasa kwa kuzingatia maadili na taratibu za chama.

Muktasari:

  • Wasira amewataka wanaotaka uongozi ndani ya CCM kujipima uwezo wao kabla ya kugombea, akisisitiza uaminifu, msimamo na ushindani wa hoja. 

Moshi. Makamu Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Tanzania Bara, Stephen Wasira ameagiza kufutwa mara moja makundi yote ya WhatsApp yanayotumiwa kuchochea migogoro ndani ya chama hicho, akisisitiza kuwa chama hakiwezi kuendeshwa kwa malumbano ya mitandaoni.

Wasira ametoa agizo hilo leo Juni 6, 2026, mjini Moshi, baada ya mwanachama mmoja kumueleza kuwepo kwa makundi ya WhatsApp ambayo baadhi ya wanachama hutumia kurushiana maneno makali na wakati mwingine kuwatukana viongozi wa chama.

Makamu Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Tanzania Bara, Stephen Wasira, akizungumza na wanachama wa CCM Wilaya ya Moshi Mjini pamoja na viongozi wa mabaraza ya jumuiya na wazee wa chama hicho, katika ofisi za CCM Mkoa wa Kilimanjaro, ambapo alisisitiza mshikamano, uhai wa chama na utekelezaji wa majukumu ya kisiasa kwa kuzingatia maadili na taratibu za chama.

Amesema mijadala ya ndani ya CCM inapaswa kufanyika kupitia vikao rasmi vilivyoainishwa kikatiba, siyo kwenye mitandao ya kijamii ambayo inaweza kuchochea taharuki na kuvuruga mshikamano wa wanachama.

“Kama yapo makundi hayo, yafutwe. Ndani ya chama chetu kuna mambo tunayojadili ambayo ni ya siri, hivyo kuyajadili kwenye makundi hayo ni matumizi mabaya ya teknolojia,” amesema Wasira.

Kufuatia agizo hilo, baadhi ya wasimamizi wa makundi mbalimbali ya WhatsApp mkoani Moshi, yakiwemo Moshi ya Moto, Moshi Kwanza Group na Moshi ya Maendeleo, wameanza kuyafuta makundi hayo na kuwaondoa wanachama wake mara baada ya mkutano huo.

Aidha, Wasira amewataka wanachama wanaotamani kugombea nafasi mbalimbali za uongozi ndani ya chama hicho kujipima kwanza uwezo wao kabla ya kuingia kwenye kinyang’anyiro.


Amesema CCM inahitaji viongozi wenye uwezo, msimamo thabiti na wanaoweza kulinda maslahi ya chama bila kuyumbishwa na mazingira ya kisiasa.
“Mwaka ujao tutafanya uchaguzi. Kila anayetamani kugombea nafasi ya uongozi anapaswa kujiuliza kwanza kama ana uwezo wa kuongoza nafasi hiyo,” amesema Wasira.
Ameongeza kuwa kiongozi wa CCM anapaswa kuwa mwaminifu, mwenye msimamo na asiyeweza kuhamisha siri za chama kwa vyama vingine.
“Hatuhitaji viongozi wanaokwenda chama kingine kufichua siri za chama. Kiongozi wa aina hiyo hatufai,” amesisitiza.
Wasira pia amewataka wanachama kuacha makundi na badala yake kushirikiana katika kuimarisha chama na utekelezaji wa shughuli za maendeleo.
Amesema ushindani wa uongozi unapaswa kuzingatia uwezo wa mtu na mahitaji ya chama, si maslahi binafsi.


“Tunahitaji viongozi wanaoweza kujibu hoja za upinzani kwa hoja na sera, si kwa matusi. Kiongozi bora hushinda kwa hoja na uelewa,” amesema.
Aidha, amesisitiza kuwa CCM ni chama cha wanachama na si cha viongozi pekee, hivyo kila mwanachama anapaswa kushiriki kikamilifu katika ujenzi wake.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Kilimanjaro, Patrick Boisafi, amesema chama hicho kimeendelea kufanya vizuri katika mkoa huo, akibainisha kuwa katika kipindi cha miaka mitano serikali imetoa Sh1.57 trilioni kwa ajili ya miradi ya maendeleo.