Zitto: 4R zitakuwa kitanzi kwa Rais Samia

Kiongozi wa Chama cha ACT-Wazalendo, Zitto Kabwe (kushoto) akizungumza katika mahojiano maalumu na waandishi wa Kampuni ya Mwananchi Communications Ltd, jijini Dar es Salaam. Picha na Sunday George

Muktasari:

Machi 29, 2024, Zitto atamaliza muda wake kama kiongozi wa chama, nafasi ya juu ya uongozi ndani ya chama hicho, akitarajia kukabidhi madaraka kwa mtu mwingine atakayechaguliwa kwenye mkutano mkuu ujao.

Dar es Salaam. Kiongozi wa Chama cha ACT Wazalendo, Zitto Kabwe amesema falsafa ya R nne (4R) ya Rais Samia Suluhu Hassan ni silaha inayoweza kutumika “kumsuta” pale anapokwenda kinyume nayo.

Zitto amesema hayo jana Februar 5, 2024 wakati wa mahojiano maalumu na Mwananchi yaliyofanyika makao makuu ya chama hicho, Magomeni jijini Dar es Salaam ambapo amezungumzia masuala mbalimbali, ikiwemo mafanikio, changamoto, fursa na mwelekeo wa chama katika miaka tisa aliyokuwa kiongozi.

Machi 29, 2024, Zitto atamaliza muda wake kama kiongozi wa chama, nafasi ya juu ya uongozi ndani ya chama hicho, akitarajia kukabidhi madaraka kwa mtu mwingine atakayechaguliwa kwenye mkutano mkuu ujao.

Katika mahojiano hayo, Zitto amezungumzia R nne za Rais Samia, akimpongeza kwa kuja na falsafa hiyo ambayo imesaidia kupiga hatua na inaweza kupima utendaji wake katika masuala ambayo yanaitafsiri.

Amesisitiza kuwa jambo muhimu ni kwamba R nne zijengewe misingi ya kisheria, isiwe ni falsafa inayotokana na imani ya Rais aliyepo. Amesema misingi hiyo ya kisheria itajengwa kwa kuwa na Katiba mpya.

“Hiyo falsafa ya Rais ya 4R, angalau inaonyesha mwelekeo, kwamba akienda kinyume mnaweza mkamsuta na kusema hii ndiyo 4R? Mfano, watu wangeandamana, wakazuiwa, wakapigwa, tungemsuta Rais, tumwambie hii ndiyo 4R? Haya ndiyo maridhiano? Haya ndiyo mabadiliko? Huu ndiyo ustahimilivu? Huku ndiyo kujenga upya? Mbona ni yaleyale, mbona watu bado wanapigwa?

“Kwa hiyo, angalau tuna jambo ambalo tunaweza tukalishika kumpinga au kumtetea kiongozi aliyepo. Kwa hiyo, ni hatua kubwa na kila Rais amekuwa na falsafa yake, Mwalimu Julius Nyerere ‘ujamaa’, Mzee Ali Hassan Mwinyi akafanya marekebisho ya uchumi, Benjamin Mkapa ‘ukweli na uwazi’, Jakaya Kikwete akaja na Ari Mpya, Nguvu Mpya, Kasi Mpa,” amesema.

Hata hivyo, amesema hizo zilikuwa ni slogans (kaulimbiu), lakini angalau Rais Samia amekuja na falsafa ambayo inaweza kutumika kumsuta kwamba amesema anataka maridhiano, watu hawawezi kufanya vikao vyao vya ndani, hayo ndiyo maridhiano?

“Kwangu binafsi nadhani Rais amefanya jambo jema kuja na falsafa ambayo inaongoza na sisi tutaitumia kwa kuonyesha hatua zinazopigwa lakini pia kwa kukosoa, kutokana na misingi ambayo imewekwa,” amesema Zitto.

Julai mosi, 2022, wakati Tanzania ikitimiza miaka 30 tangu kurejea katika siasa za mfumo wa vyama vingi, Rais Samia aliandika makala maalumu ambayo pamoja na mambo mengine alitambulisha falsafa ya 4R atakazozitumia katika uongozi wake.

Rais Samia, aliyeingia madarakani Machi 19, 2021 baada ya kifo cha mtangulizi wake, John Magufuli alisema, “ninaamini kwa jitihada zetu za R4, tutaweza kutimiza malengo ya kuwa na mfumo wa vyama vingi vya siasa.”

Alisema lengo kuu halikuwa kuwa na vyama vingi vya siasa, bali lengo lilikuwa kujenga jamii yenye uzalendo, maridhiano, ustahimilivu na yenye uchumi unaokua kwa wote na endelevu.


Mabadiliko ya sheria

Katika mahojiano hayo, Zitto amesema kupitia miswada iliyopitishwa hivi karibuni na Bunge, angalau kuna sheria, ambazo zinaweza zikawa si za kutosheleza, lakini kuna hatua imepigwa na matokeo yanaonekana kupitia michakato tofauti iliyofanyika na inayoendelea kufanyika.

Amebainisha kuwa angalau sasa hivi Rais hawezi kuamka asubuhi akatangaza Tume ya Uchaguzi, badala yake lazima kuwe na mchakato.

Amesema sasa hivi si “automatic” (moja kwa moja) kwamba mkurugenzi wa halmashauri anakuwa msimamizi wa uchaguzi, Tume inaweza kumteua mtu yoyote kuwa msimamizi wa uchaguzi.

Kiongozi huyo wa chama amesema wanafanya mikutano ya hadhara tangu Januari, 2023 na kuna vikao vya vyama vinafanyika na Janauri 24, 2024 watu waliandamana bila kuzuiliwa. Kwa hiyo, kuna hatua kubwa ambayo wamepiga lakini bado haitoshelezi.

Hata hivyo, amesisitiza kuwa hatua hizo zitatosheleza pale itakapopatikana Katiba mpya kwa sababu ndiyo itaweka misingi ya kuhakikisha kwamba mageuzi, ujenzi mpya wa Taifa, ustahimilivu na maridhiano ni vitu ambavyo vimetengenezwa kwenye mifumo.

“Ni mchakato, huwezi siku hiyo hiyo Rais ametamka 4R, halafu 4R zikawa, hapana. Lazima watu waresist (wapinge), lakini naamini kabisa ni mchakato ambao unaweza ukatupeleka mbele. Kuna hatua ambayo tumepiga.

“Itakuwa ni ukosefu wa shukrani tukisema hali ni ileile, hali si ileile. Mimi leo naendesha (gari) mwenyewe, miaka minne iliyopita ilikuwa ni lazima uwe na gari mbili na niwe na madereva na mlinzi, lakini sasa hawana kazi. Sina wasiwasi, tofauti na ilivyokuwa miaka minne iliyopita,” amesema Zitto.


Miswada sheria za uchaguzi

Katika kusukuma mabadiliko ya sheria, Zitto amesema kila chama kilikuwa na mkakati wake na maoni yake, hata hivyo, chama chake cha ACT Wazalendo kiliamua tangu mwaka 2022 kushirikiana na wadau wengine, ikiwemo Serikali katika kuyafikia mabadiliko hayo.

Amesema miswada ilipotoka, ilikuwa na hoja yao moja pekee ya watu kutochaguliwa bila kupingwa. Amesema chama chake kilifungua kesi mahakamani kuhusu jambo hilo na kushinda na jambo hilo pekee ndiyo lililoingizwa kwenye miswada.

Baadhi ya mambo waliyokuwa wamependekeza ni mwenyekiti na makamu wa Tume ya Uchaguzi nao waingie kwenye mchakato wa usaili, mkurugenzi wa Tume asiwe katibu wa kamati ya usaili, wakurugenzi wasitajwe kwenye sheria kama wasimamizi wa uchaguzi, uchaguzi serikali za mitaa usimamiwe na Tume.

“Kwenye Tume waligusa nusu nusu, sheria ya uchaguzi wakagusa nusunusu. Katika hali ya kawaida, watu wangehamaki, sisi tukasema tu-engage (tuwashirikishe), tuna hoja twendeni kwenye kamati, tukaenda na kamati kuu ikasema nenda wewe Kiongozi wa Chama,” amesema Zitto, aliyechaguliwa kuongozi chama hicho kwa mara ya kwanza Machi 29, 2015.

Hata hivyo, amesema waliendelea kuyapigia kelele masuala muhimu na katika miswada iliyopitishwa juzi, hoja zao sita kati ya 10 walizoziwasilisha mbele ya Kamati ya Bunge ya Katiba, Sheria na Utawala zimechukuliwa kama zilivyo.

 “Katika hoja 10 tulizopeleka kwenye kamati, hoja sita zimechukuliwa vilevile ambavyo sisi tumetaka, yaani wamehamisha maelezo yetu sisi ACT Wazalendo, wakayaingiza kwenye sheria kama yalivyo, nne tukashindwa.

“Sisi tunasema sawa, kama ulikuwa unamdai mtu Sh100, akakulipa Sh60, hauzikatai zile Sh60 akikuletea, unachukua hizo Sh60 unatia mfukoni halafu unadai Sh40 zilizobakia. Hiyo ndiyo approach (mtazamo) tuliyoitumia,” amesema mwanasiasa huyo.

Amesisitiza sasa wamepewa hiki kwenye miswada iliyopitishwa na Bunge, sasa wanakwenda kudai zaidi kwa sababu wasipofanya hivyo, hawatapata chochote. Amesema mwaka 2014 walitakiwa kuyapata hayo kwenye mabadiliko madogo ya Katiba, lakini walikataa.

“Ni muhimu sana, pamoja na changamoto zote zitakazotokea, msitoke kwenye reli ya kuwa na masuala, na hilo tumejitahidi sana na kweli inatugharimu, wakati mwingine tunakuwa tunajadiliana ndani lakini wanatokea watu wanasema mabadiliko hayaji mara moja, lakini mkiwa na masuala, yanakuja,” amesema Zitto, ambaye amekuwa mbunge kwa miaka tisa.

Amesisitiza kwamba ni muhimu watu wakajua unachosimamia, kama mnapinga kila siku, basi hamna chenu. Amesisitiza kwamba lazima vyama vya siasa vipinge na kutoa mbadala, ili Serikali ifanyie kazi masuala hayo.

Zitto amesema anaamini kwamba mazingira ya kisiasa sasa yanaanza kuwa bora taratibu, kuelekea kwenye demokrasia iliyokomaa.

Ametoa wito kwa vyama kujiimarisha kama taasisi, kuwa na hoja za watu na kutengeneza mbadala wa uhakika.