Rais Samia kutumia 4R kwenye uchaguzi ujao

Muktasari:

  • Rais wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan amesema Uchaguzi wa serikali za mitaa na Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2025 anauchukulia kwa uzito mkubwa hivyo amewataka viongozi wa vyama mbalimbali kuhakikisha wanateua wagombea wenye sifa na Watanzania wajitokeze kupiga kura.

Dar es Salaam. Rais wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan amesema ili kuwe na amani na mshikamano wa kitaifa, Serikali yake imekuja na falsafa ya 4R ambayo atazitumia katika uchaguzi wa serikali za mitaa pamoja na uchaguzi mkuu wa mwaka 2025.

Amesema ili nchi iweze kupiga hatua kubwa za kimaendeleo, lazima iendelee kuwa moja kwa kuishi kwa umoja na suala la uchaguzi litazingatia hilo.

Rais Samia ameyasema hayo leo Jumapili, Januari 21, 2024 wakati akishiriki ibada maalum ya kumuingiza kazini Mkuu wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT), Askofu Dk Alex Malasusa katika viwanja vya Kanisa Kuu la Azania Front, Dayosisi ya Mashariki na Pwani.

“Baba Askofu Malasusa, umezungumzia umoja, amani na mshikamano wa kitaifa, kuhusu amani nakubaliana nawe kwa asilimia 100 kwamba tukiwa wamoja tutajenga taifa lenye nguvu.

“Katika uongozi huu, tumekuja na falsafa ya R4, kiswahili chake ni maridhiano, mageuzi, ustahimilivu na kujenga upya taifa letu. Nizihusishe R4 na maneno yaliyosemwa kwenye kitabu cha Marko sura ya 3:25 ‘Hali kadhalika kama jamii moja imegawanyika yenyewe kwa yenyewe, jamii hiyo haiwezi kudumu’.”

Amesema kwa Waswahili husema nyumba isiyologwa, haimei lakini ikigawanyika haiwezi kusimama, hivyo Tanzania isiende kuwa nyumba hiyo.

“Nauchukulia uchaguzi huu kwa uzito mkubwa sana, ni uchaguzi unaotoa viongozi maeneo tunayoishi nililete kwa wananchi, wajitokeze kuchagua viongozi sahihi na kwa viongozi wa vyama chagueni watu sahihi ili wananchi wawe na uwanda mpana wa kuchagua viongozi,” amesema.

Rais Samia amesema ujenzi wa demokrasia unahitaji zaidi wana demokrasia kujenga si tu kuwepo demokrasia, bali inahitaji wana demokrasia.

“Si kila aliye kwenye michakato ya demokrasia ni mwanademokrasia, wengine ni wanaharakati, kuna tofauti na haya mawili, tutaendelea kulinda misingi ya demokrasia hapa nchini kwetu inayowezesha demokrasia kushamiri zaidi,” amesisitiza.

Rais Samia amesema amani ni kichocheo kikubwa, Serikali itaendelea kuilinda ikiwemo kutekeleza ahadi inazoziweka.

Amesema Tanzania ni salama na Serikali wajibu wake ni kuendelea kudumisha amani na usalama huo kwa kuendeleza ushirikiano mkubwa kati ya Serikai na Taasisi za dini.