Mbivu, mbichi mwaka mmoja wa utekelezaji wa 4R za Rais Samia

Rais Samia Suluhu Hassan akiongoza kikao cha majadiliano pamoja na viongozi wakuu wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) na CCM jijini Dodoma. Picha na Maktaba

Dar es Salaam. Leo umetimia mwaka mmoja tangu Rais Samia Suluhu Hassan alipotambulisha falsafa yake ya R nne (4R) ambazo anazitumia katika utawala wake.

Wanasiasa, wasomi na wachambuzi waliotafutwa na Mwananchi wamezungumzia utekelezaji wake na kueleza kuwa umekuwa na mwelekeo mpya wenye mafanikio, huku baadhi wakitilia shaka kuhusu utekelezaji na uharaka wake.

Julai Mosi, 2022, Rais Samia aliandika makala iliyochapishwa katika vyombo vya habari siku hiyo ikiwa ni kumbukumbu ya miaka 30 tangu kuanza kwa mfumo wa vyama vingi vya siasa nchini, Julai 1992.

Katika makala hiyo, Rais Samia ambaye pia ni Mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi (CCM), alijadili masuala mbalimbali, ikiwamo kutambulisha R nne ambazo ni maridhiano (Reconciliation), mabadiliko (Reforms), ustahimilivu (Resilience) na kujenga upya (Rebuilding).

Alihitimisha makala hiyo kwa kubainisha kwamba lengo kuu halikuwa kuwa na vyama vingi vya siasa, bali lilikuwa kujenga jamii yenye uzalendo, maridhiano, ustahimilivu na yenye uchumi unaokua kwa wote na endelevu.

Katika kipindi cha mwaka mmoja, Rais Samia ameondoa zuio la mikutano ya hadhara, Januari 3 na sasa vyama vya siasa vinafanya mikutano bila kubughudhiwa, tofauti na hali ya sintofahamu iliyokuwapo kwa takribani miaka saba iliyopita.

Pia, alihudhuria kongamano la wanawake lililoandaliwa na Baraza la Wanawake wa Chadema (Bawacha), kitendo ambacho kilileta taswira ya maridhiano ya kweli na ishara ya kiongozi aliyeamua kujenga umoja na mshikamano wa kweli baina ya vyama hivyo hasimu kwa muda mrefu.

Katika kipindi hicho, mazungumzo ya maridhiano baina ya CCM na Chadema yaliendelea, huku Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe akisisitiza hawatajitoa katika hilo, licha ya kutuhumiwa ‘kulamba asali’.

Ameonyesha kuwa na ustahimilivu, hasa pale anapokosolewa na upinzani. Watu wamekuwa huru kuzungumza na hakujasikika matukio ya unyanyasaji wa wananchi kwa sababu ya maoni yao kinzani dhidi ya Rais Samia.

Shughuli za kiuchumi zimeendelea kufanyika, ikiwamo mkataba wa uboreshaji wa bandari nchini ulioingiwa kati ya Serikali ya Tanzania na ya Dubai, huku ukiibua mjadala mpana wa kitaifa.

Hata hivyo, wadau wa demokrasia nchini wamechambua na kutoa maoni tofauti, wakipongeza kwa hatua zilizopigwa hadi sasa lakini wakieleza kwamba mengi yanahitaji kufanyika ili kufanikisha falsafa yake ya R nne.

Wengine wameenda mbali zaidi wakibainisha kwamba Rais Samia haiishi falsafa yake hiyo au watendaji wake hawajamwelewa, pia, wamehoji chanzo cha hizo R nne na kama ni shirikishi katika kuwaongoza wananchi.

Maoni ya wanasiasa

Mkurugenzi wa Itifaki, Mawasiliano, Uenezi na Mambo ya Nje wa Chadema, John Mrema alisema upande wa maridhiano kati ya CCM na Chadema, vikao vinaendelea lakini vinakwenda taratibu.

“Kwenye eneo hilo kunahitajika kasi ya makusudi ili tuweze kupata maridhiano ya kitaifa na kuridhiana kama Taifa ili tuweze kuanza upya,” alisema Mrema.

Kuhusu mabadiliko, alisema yapo mabadiliko mengi ambayo Rais Samia ameyafanya, lakini hayajawa mabadiliko ya kisera au kisheria. Alitolea mfano kuondolewa kwa zuio la mikutano ya hadhara, akisema Sheria ya Vyama vya Siasa na Sheria ya Jeshi la Polisi haijabadilishwa ili zizuie mtu anayetaka kuzuia mikutano hiyo.

“Mabadiliko yamefanyika, lakini siyo ya kisera au kisheria, ni matamko, ni decree, kitu ambacho kinategemea sasa na utashi wa rais aliyepo, kwa hiyo katika kuleta mabadiliko ni vizuri sana tukawa na mabadiliko ya kisera na kisheria ili hata akija Rais mwingine akute tuna sheria na sera ambazo hawezi kuzibadilisha,” alisema.

Mrema alizungumzia pia ustahimilivu katika uongozi wa Rais Samia, akisema wanaendelea kuona dalili za kuvumiliana kwa sababu tangu alipoanzisha hizo R nne, wanawake wa Chadema walimwalika, akashiriki.

“Ni ustahimilivu kwa kweli kwenda kushiriki tukio la chama kingine kwa Rais wa nchi ambaye ni mwenyekiti wa chama kingine cha siasa. Lakini yalipotokea maandamano, wanawake wa Chadema waliruhusiwa, ACT Wazalendo na wanaharakati wengine hawakuruhusiwa.

“Kwa hiyo, inaonyesha kwamba somo la ustahimilivu bado, inaonyesha inategemeana na huo ustahimilivu uko kwenye ajenda gani, kwa hiyo hapo inabidi ustahimilivu uwe kwenye mambo yote au wasaidizi wake hawajaelewa hilo somo,” alisema Mrema.

Akamalizia na dhana ya kujenga upya akisema, Taifa linatakiwa kujengwa kwa msingi imara na msingi imara wa kujenga nchi ni Katiba.

“Kumekuwa na maneno kwamba wako tayari kuandika Katiba, lakini hatuoni matendo yakiambatana na kauli hiyo. Lazima tukubaliane kwamba ni muhimu tuweke msingi imara ili tujenge Taifa letu kwa pamoja,” alisema.

Katibu Mkuu wa ACT Wazalendo, Ado Shaibu alisema chama chake kiliipokea kwa mikono miwili falsafa yake ya 4R wakiamini itakwenda kuiponya nchi kutokana na makovu yaliyotokana na miaka saba ya kuzimwa kwa uhuru wa kisiasa.

Alisema leo wakitazama nyuma baada ya kuanzishwa kwa falsafa hiyo, wanaona yapo mambo yaliyowaridhisha, yapo mambo yaliyowaridhisha kiasi na yapo mambo ambayo hatua stahiki hazijachukuliwa, hivyo hawajaridhishwa nayo.

Shaibu alibainisha mambo ambayo amepiga hatua kuwa ni pamoja na uhuru wa kisiasa, sasa wanafanya shughuli zao za kisiasa kwa uhuru, wanafanya mikutano ya hadhara na maandamano na hakujawa na changamoto kubwa kama za awali.

“Eneo ambalo linatutia wasiwasi ni kuwa na kalenda ya utekelezaji wa mageuzi ya kisiasa hapa nchini, kwa maana kwamba Serikali haijaweka bayana zile ahadi zake ambazo ilizitoa, utekelezaji wake utakuwa ni wa namna gani na wa kipindi gani.

“Mfano, maeneo kama Tume huru ya uchaguzi, Katiba mpya, mageuzi ya Jeshi la Polisi na vikosi vya ulinzi na usalama, kuwa na sheria mpya ya vyama vya siasa, kuandikwa upya kwa sheria ya kusimamia tasnia ya habari,” alisema.

Shaibu alisisitiza kwamba mambo hayo Rais Samia aliyatolea ahadi pamoja na mawaziri wake, ndani na nje ya Bunge. Alisema hadi sasa wadau hawafahamu ni lini sheria mpya ya uchaguzi itaandikwa na lini mchakato wa katiba mpya utaanza.

Mkurugenzi wa Habari, Uenezi na Uhusiano wa Umma, Chama Cha Wananchi (CUF), Mohamed Ngulangwa alisema licha ya Rais Samia kumwagiza Msajili wa Vyama vya Siasa kuitisha Baraza la Vyama vya Siasa kuelekea kufufua mchakato wa Katiba mpya mwezi mmoja uliopita, bado hakuna mwanga kuelekea maridhiano ya kweli.

“Hitaji la uchaguzi huru na wa haki ndiyo kipaumbele kinachobeba hoja zote nne kwenye tafsiri ya 4R. Uchaguzi huru na wa haki ndiyo kiini cha kuleta maridhiano, mabadiliko yanayokusudiwa, ustahimilivu na kujenga upya kulikofafanuliwa na Rais, Julai 2022,” alisema.

Ngulangwa alisema mwaka mmoja umepita bila kuwa na mchakato wa kupata Tume huru ya uchaguzi kuelekea kupata Katiba mpya.

“Kama ambavyo sisi CUF tuliweka bayana Novemba 2, 2020 mara baada ya Serikali ya CCM kuvuruga uchaguzi mkuu wa mwaka 2020, nchi inahitaji Tume huru ya uchaguzi sasa kuliko muda mwingine wowote,” alisema.

Alisisitiza kwamba Serikali imeshindwa kuweka bayana ratiba ya mchakato wa kupata tume huru ya uchaguzi itakayohakikisha chaguzi hizo zinakuwa huru na za haki.

Alisema muda unavyokwenda kwa kasi, ni vigumu kuuona mwanga unaoweza kutupelekea kupata maridhiano ya kweli na kutimia 4R za Rais Samia.

“Tunatoa wito kwa Rais na Serikali anayoiongoza kuongeza kasi ya kuhakikisha 4R zinaingizwa kwenye matendo zaidi kuliko mahubiri. Sheria itakayoongoza upatikanaji wa Tume huru ya uchaguzi ambayo watumishi wake watakuwa waajiriwa watakaopatikana kwa mchakato huru na wa wazi ni muhimu ikapatikana,” alisema.

Wachambuzi wafunguka

Mchambuzi wa masuala ya siasa, Buberwa Kaiza alisema kwa kuwa chanzo cha hizo 4R hakijulikani, hatujajua kama zilitokana na ushauri, utafiti au chochote, mawazo hayo hayakuwa na msingi wa mazingira halisi ya watu.

Alisema kama ingekuwa na mazingira halisi ya watu, 4R zisingeanzia kwake, bali zingeanzia kwa raia, pengine tungetathmini vizuri kwa sababu tungekuwa tunaona huko kilikoanzia, jitihada zake za kutekeleza zimerudisha nini.

Alisema suala la maridhiano haliwezi kuwa la wanasiasa tu, bali ni wananchi wote katika masuala ambayo yanaleta hali ya kutoelewana. Alitolea mfano sakata la mkataba wa DP World lilivyoleta mgawanyiko.

Mchambuzi huyo wa siasa alisema hajaona mabadiliko yoyote katika umasikini wa watu, uboreshaji wa huduma za afya.

Alisema kwenye mabadiliko hawajaona juhudi zozote zilizofanyika kwa upande wa sera na sheria, alisema kuna sheria zilizotungwa wakati wa awamu ya tano kama vile Sheria ya Vyama vya siasa, Sheria ya NGO, Sheria ya Huduma za Habari, lakini hawajaona zikifanyiwa mabadiliko.

Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dodoma (Udom), Dk Paul Loisulie alisema Rais Samia amefanikiwa kwa kiasi kikubwa katika kuiishi falsafa yake ya 4R kwa sababu kilichokuwa kikisumbua zaidi ni maridhiano ya kisiasa.

Alisema moja ya mambo yaliyofanikiwa ni maridhiano ambapo aliondoa zuio la mikutano ya hadhara na pili, ni kwenda kwenye mkutano wa wanawake wa Chadema, alisisitiza kwamba hayo ni mafanikio makubwa.

“Kwenye mabadiliko bado tuko hatua za awali kwa sababu maridhiano inabidi uweke kwenye sheria, kwa mfano suala la mikutano ya hadhara, tumeweka sheria gani ambayo itamzuia Rais mwingine yeyote.

“Eneo jingine ni Tume ya uchaguzi na mambo mengine, hiyo bado…tuko kwenye hatua za awali. Kufikia maendeleo tunahitaji muda kwa sababu tunahitaji kufikia hatua hizi za awali,” alisema mchambuzi huyo.

Mjumbe wa Kamati Kuu ya CCM Taifa, Lailah Ngozi alisema wanaona Rais Samia anakwenda vizuri na falsafa yake ya 4R, hasa ya maridhiano, sasa uhusiano wao na upinzani ni mzuri na hawawapi shida.

Aliongeza kwamba wapinzani nao wanaonekana kuelewa dhana hiyo ya 4R ndiyo maana wana uhusiano mzuri, licha ya kwamba wakati mwingine wanakuwa hawaeleweki, wakienda mbele na kurudi nyuma.

"Ukiangalia uhusiano wetu na upinzani, tunaona hawatusumbui na wao pia wamezielewa hizo 4R. Kwa hiyo, imekuwa tunakwenda na maono ya Rais Samia, wanaCCM pia tulikuwa tunayafuata, tunaishi nayo. Kila kitu kinakwenda vizuri na huu ni mwaka mmoja tu, huko mbele kuna mengi mazuri.

"Ingawa hawa wapinzani ni kama wanakwenda, wanarudi. Wakati mwingine unajiuliza, sasa hii kitu walitamani iwe hivi, Rais Samia kanyoosha mambo, lakini bado wanapiga kelele. Hiyo ni kwa upande wao, sisi wanaCCM tunaona anakwenda vizuri," alisema Ngozi.

Alisema kwa sasa nchi imetulia na harakati za maendeleo zinafanyika kwa uwazi, ikiwa ni sehemu ya utekelezaji wa 4R za Rais Samia kama alivyowaahidi Watanzania.