ATCL irekebishe haya kuongeza ufanisi
Makamu wa Rais, Dk Philip Mpango amelitaka Shirika la Ndege la Tanzania (ATCL) kubadilika na kutafuta ufumbuzi wa tatizo la kuchelewesha na kuahirisha safari za ndege mara kwa mara.
Dk Mpango alitoa kauli hiyo juzi, katika hafla ya mapokezi ya ndege mpya aina ya Boeing 737-9 Max kutoka nchini Marekani na kuifanya ATCL kuwa na jumla ya ndege 14.
Tunaipongeza Serikali kwa juhudi zake za kuifufua ATCL kwa kununua ndege mpya na pia kuhamisha ndege za Serikali kwenda kumilikiwa na ATCL, ili zifanye biashara ya kusafirisha abiria.
Licha ya juhudi zote za Serikali, bado shirika hilo limekuwa likilalamikiwa na abiria kwa kuchelewa ratiba na kuahirisha safari, hali inayowalazimu abiria kupata hasara, kuharibu mipango yao na kukosa imani na huduma za shirika hilo.
Tunasema hivyo kwa sababu malalamiko ni mengi, kutokuwapo uhakika wa safari au kuchelewa kunasababisha usumbufu kwa abiri na wengine kuchelewa kuunganisha ndege nyingine kuendelea na safari nyingine.
Mfano, kuna abiria aliwahi kulalamika kuchelewa sherehe ya harusi kwa sababu ya ndege kuchelewa, fikra zake zilimtuma akiondoka siku ya harusi kwa kutumia ndege atawahi sherehe, lakini uchelewaji wa ndege ulisababisha akute harusi imeisha.
Kauli ya Dk Mpango iwaamshe ATCL waache kufanya kazi kwa mazoea, waone umuhimu wa Serikali wa juhudi zake za kulifufua shirika hilo, ambalo huko nyuma liliripotiwa kuwa na ndege moja, huku wafanyakazi wakiwa lukuki.
Rai yetu wafanyakazi wa ATCL waone fahari ya kuwa na ndege za kisasa na kubwa, wajivunie walicho nacho na kuwathamini abiria kwa kuwapa huduma iliyo bora na kuwarahisishia shughuli zao za kimaisha.
Ushindani wa kibiashara kwenye usafiri wa anga ni mkubwa, mashirika mengi yamebadilisha utendaji wao, mbali na unafuu wa nauli, vivutio kwenye biashara ya ndege ni vingi kumvutia mteja.
Wafanyakazi wa ATCL wanatakiwa kufahamu ucheleweshaji au kuahirishwa safari kunaumiza wateja, wengine ni wafanyabiashara, kuna wagonjwa na kuna watumishi wakiwa na ratiba za kuwahi makazini, wote wanapoharibiwa ratiba inawasababishia maumivu na hasara.
Mbali na kuumiza abiria, pia ucheleweshaji na kuahirisha safari kunalidhoofisha shirika lenyewe kwa kupoteza uaminifu na wateja na hatimaye kulikimbia.
Mashirika mbalimbali ya ndege duniani yamekuwa yakibuni namna bora ya kusafirisha abiria kwa raha mustarehe, lakini kwa ATCL licha ya juhudi za Serikali, bado kuna watu hawaoni thamani waliyopewa.
Rai yetu wazembe na wabadhirifu ndani ya shirika hilo wasifumbiwe macho, waondolewe na kufikishwa kwenye vyombo vya nidhamu na sheria.
Uongozi wa shirika hilo unapaswa kuachana na tabia ya kufanya kazi kwa mazoea, shirika lijitangaze, lionyeshe vivutio walivyonavyo kwenye ndege zao.
Na kama kuna sababu nyingine, kama inavyodaiwa kuwa baadhi ya ndege zilizopangwa kwa safari zinatumika kuwasafirisha viongozi, zifanyiwe kazi haraka na pengine kwa kutenganisha tena shughuli hizo, ili shirika liweze kuaminika na kusimama.
Abiria hawataki shida, wanatoa fedha zao kwa lengo la kupata wanachotaka, kama wanakutana na kero kwenye kuhudumia wateja, wanatafuta sehemu nyingine, mashirika ya ndege yako mengi duniani na kuna ushindani mkubwa.
Ndiyo maana tunasema alichoagiza Dk Mpango kifanyiwe kazi kwa haraka na watendaji ndani ya ATCL wabadilike.
Watanzania wanataka kuona ufufuaji wa shirika hilo unakuwa na tija.
(Mwananchi)