Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Bajeti imepita, twende kwenye vitendo

Waziri wa Fedha, Balozi Khamis Mussa Omar, akiwasilisha mapendekezo ya Serikali kuhusu makadirio ya mapato na matumizi kwa Mwaka 2026/2027, bungeni jijini Dodoma. 

 Hatimaye Bunge limehitimisha mjadala wa Bajeti ya Serikali kwa mwaka wa fedha 2026/2027 na kupitisha mapendekezo mbalimbali, yatakayoongoza matumizi na vipaumbele vya Taifa katika mwaka huo.

Kwa siku kadhaa, Watanzania walishuhudia mijadala yenye hoja nzito kutoka kwa wabunge waliotumia nafasi yao kuwasilisha maoni, ushauri na kilio cha wananchi wanaowawakilisha.

Katika mfumo wa kidemokrasia, Bunge ni sauti ya wananchi. Hoja zinazotolewa na wabunge ndani ya Bunge si maoni yao binafsi pekee, bali ni matokeo ya changamoto, matarajio na mahitaji ya wananchi waliowatuma kwenda kuwawakilisha.

Ndiyo maana mijadala ya bajeti huwa na umuhimu mkubwa, kwa sababu ndiyo jukwaa linalobeba sauti za wananchi kutoka pembe zote za nchi.

Sasa kwa kuwa hatua ya majadiliano imekamilika na bajeti imepitishwa, kilichobaki ni utekelezaji. Wito wetu ni kuona Serikali ikitekeleza kwa vitendo yale yote yaliyopitishwa na kupendekezwa, kwa lengo la kuleta manufaa kwa wananchi na kuchochea maendeleo ya Taifa.

Miongoni mwa hoja zilizojitokeza kwa nguvu wakati wa mjadala wa bajeti ni suala la kodi na tozo zinazowakabili vijana wanaojishughulisha na biashara ndogo ndogo na shughuli za kujitafutia kipato.

Vilevile, wabunge walieleza umuhimu wa kuweka mazingira rafiki kwa wananchi wanaoanzisha biashara. Uchumi wa Taifa hauwezi kukua bila sekta binafsi yenye nguvu.

Wakati Serikali ikiendelea kuhamasisha ujasiriamali na ubunifu, ni muhimu kuhakikisha mfumo wa kodi hauwi kikwazo kwa wananchi wanaojaribu kuanzisha au kukuza biashara zao.

Ndiyo maana mapendekezo ya wabunge ya kutaka nafuu ya kodi kwa biashara changa yanapaswa kupewa nafasi katika utekelezaji wa sera na mipango ya Serikali.

Sambamba na hilo, kulikuwa na wito wa kuboresha mifumo ya ukusanyaji kodi ili iwe ya kiutu zaidi na inayojenga ushirikiano kati ya mlipakodi na mamlaka husika.

Hakuna ubishi kuwa Serikali inahitaji mapato ili kutekeleza majukumu yake. Hata hivyo, uzoefu unaonyesha kuwa walipakodi wanakuwa tayari kutimiza wajibu wao wanapoona haki, usawa na heshima katika namna wanavyoshughulikiwa.

Aidha, hoja nyingine iliyojitokeza kwa nguvu ni pendekezo la kupunguza matumizi yasiyo ya lazima serikalini.

Hili ni pendekezo lenye mantiki kubwa katika kipindi ambacho mahitaji ya wananchi yanaongezeka kila siku. Kila shilingi inayookolewa kutokana na matumizi yasiyo ya lazima inaweza kuelekezwa katika kuboresha huduma za afya, elimu, maji, miundombinu, kilimo na sekta nyingine zinazogusa maisha ya wananchi moja kwa moja.

Tunafahamu kuwa mifano hiyo ni sehemu ndogo tu ya mapendekezo mengi yaliyotolewa wakati wa mjadala wa bajeti. Kulikuwa na hoja kuhusu uwekezaji, ajira, huduma za kijamii, maendeleo ya vijijini na masuala mengine mengi muhimu kwa ustawi wa Taifa.

Ndiyo maana tunasisitiza kuwa mafanikio ya bajeti hayapimwi kwa ukubwa wa fedha zilizopitishwa wala muda uliotumika kuijadili, bali kwa kiwango cha utekelezaji wake na matokeo yatakayogusa maisha ya wananchi.

Tunaamini Serikali ni sikivu na imekuwa ikionyesha utayari wa kupokea maoni ya wadau mbalimbali. Sasa ni wakati wa kuthibitisha usikivu huo kwa kuyatafsiri mapendekezo yaliyotolewa na wabunge kuwa hatua za vitendo.