Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Dhihaka ya joho na shahada

Mackie Mdachi

Muktasari:

Hizi ndizo zinazoitwa shahada za heshima kwa Kiingereza huitwa ‘…honourary degree’; mtu hupitishwa na jopo maalumu la Chuo Kikuu, husika na kutoa taarifa au tangazo la wazi.

Hayati Mwalimu Julius Kambarage Nyerere, aliwahi kukataa kutunukiwa baadhi ya shahada hizo akizisemea kuwa ni sawa na kuvishwa kilemba cha ukoka

Joho, linaelezewa kuwa ni ‘vazi pana linalofanana na koti refu, ambalo mbele liko wazi na limenakshiwa au kushonwa kwa darizi katika sehemu ya shingoni na mbele’. Soma Kamusi ya Kiswahili Sanifu ukurasa wa 92, toleo la 1981. ‘Joho ni tofauti na mgolole au mgorore,’ wanavalishwa machifu wetu wa mila na jadi zetu.

Shahada nayo kwenye kamusi hiyo hiyo imeelezewa kwa kifupi kuwa ni ‘digrii’. Ni wazi kuwa hutolewa au kutunukiwa na Chuo Kikuu kinachotambulika kimataifa na siyo vinginevyo.

Graduesheni

Neno hilo nimeliandika hivyo ili lieleweke, bali ni neno la Kiingereza ‘graduation’, ambalo kwenye Kamusi ya Kiingereza limeelezwa kuwa ni ‘…the ceremony at which diplomas and degrees are given and received…’ na neno ‘graduate’ limeelezwa kuwa ni ‘…take a degree at a University’.

Tafsiri isiyo rasmi ni ‘…sherehe ya kutoa, kupewa na kupokea shahada na stashahada kutoka Chuo Kiuu. Hapa hakuna nyongeza ya ziada. Na yale ‘majoho’ yanayovaliwa wakati wa sherehe hizo kwa Kiingereza huitwa ‘…graduation gowns’ yaani ni maalumu kwa shughuli hiyo tu.

Shahada husika hutolewa kwa mwanafunzi au yeyote aliyesomea somo fulani na akatambulika kuwa amefaulu ipasavyo kwa viwango tofauti na jopo la waalimu au wakufunzi waliobobea kwenye somo husika. Pia ni wakufunzi wanaotambulika kitaifa na kimataifa.

Shahada za heshima

Zipo shahada zinazotolewa kwa mtu yeyote msomi, ambaye amefanya mchango mkubwa kwa fani fulani, ambao umetambulika kimataifa; tena wala siyo jambo la kutamka tu, au la mwaka mmoja hivi bali liwe tukio lililoleta mafanikio endelevu kwa ufanisi stahiki wa muda mrefu kwa wanajamii mbalimbali.

Hizi ndizo zinazoitwa shahada za heshima kwa Kiingereza huitwa ‘…honourary degree’; mtu hupitishwa na jopo maalumu la Chuo Kikuu, husika na kutoa taarifa au tangazo la wazi.

Zipo shahada za heshima kutokana na uwajibikaji katika matukio ya kuhimiza na kuleta amani, ama ukiwa ni nguli unatambulika wa somo fulani kama hisabati, au sayansi ya fizikia, jiografia, baiolojia, kilimo na kadhalika. Na hayo yafikie kiwango cha juu cha kipekee ulimwenguni, wala isiwe na shaka yeyote kwa wasomi na wanajamii. Hizi siyo shahada za heshima zinazotolewa kwa fadhili, urafiki, au hisani ya aina yoyote ile au upendeleo.

Dhihaka

Hivi sasa kumezuka tena kwa kasi kubwa sherehe za graduesheni mpaka kwenye shule za awali za watoto wadogo wanaoanza kuchipukia ; kwa Kiingereza ‘nursery schools, na wanavalishwa ‘majoho’ pia.

Sio hizo tu, bali hata shule za msingi na sekondari ambapo ‘majoho’ kama yale ya Vyuo Vikuu huvaliwa.

Miaka ya nyuma sherehe hizo na ‘majoho’ hayo tuliziona na kuvaliwa na vyuo vikuu tena yalikuwa na heshima kuu stahiki; hivi sasa ni kama dhihaka na mzaha tu; niseme ‘majoho’ yamechuja, heshima iko wapi?

Udaktari na uprofesa

Shahada hizo zilizo ‘tunu’ za kipekee, ambazo kwa lugha ya mjini, watu wanazisotea kwa bidii kubwa na kwa miaka mingi, hivi sasa zimeonekana kama ni tunda linalojiangukia tu likiiva na thamani yake imeporomoshwa kimzaha mzaha tu na akina pwagu na pwaguzi, mabazazi wachache, kwa kutaka sifa na kijikweza.

Upitapo mjini kandokando ya barabara, utayaona mabango tele yanayotangaza biashara ya tiba za jadi, nayo yakikuzwa kwa vyeo vya ‘madaktari na maprofesa,’ wa tiba hizo na hata kwenye vipindi vya redio na luninga. Hivi Serikali hawayaoni matangazo na mabango hayo dhalilishi?

Nakumbuka wakati fulani Serikali au manispaa waliamuru mabango yote ya hao waganga wa tiba za jadi, yaani madaktari na maprofesa wasioshindwa kutibu ugonjwa wowote yaondolewe. Lakini kwa lugha ya mjini, amri hiyo ni ya kisanii, ama nguvu ya soda kwani mabango hayo yametapakaa bwelelee. Je, ni nani zaidi Serikali au waganga wa ajadi na vyeo vyao feki?

Si hao tu, bali miaka fulani kulizuka mtindo wa baadhi ya viongozi wa kisiasa kwenda Ulaya kwenye nchi rafiki kupigwa msasa wa kisiasa na kurudi hapa baada ya miezi michache na vyeo vya udaktari. Ni mashaka matupu na udhalilishaji wa shahada hizo.

Hivi karibuni tumesikia na kusoma magazetini kuwa mke wa Rais wa Zimbabwe ametunikiwa shahada ambayo haileweki na hata andishi maalumu la somo husika ‘thesis’ halijulikani lilipo ama imetoweka.

Hayati Mwalimu Julius Kambarage Nyerere, aliwahi kukataa kutunukiwa baadhi ya shahada hizo akizisemea kuwa ni sawa na kuvishwa kilemba cha ukoka tena na vyuo ambavyo havistahiki na hakutaka makuu.