Dira 2050; Mafanikio yanawezekana yakisimamiwa vema
Rais Samia Suluhu Hassan na viongozi wengine wakionesha nakala za vitabu vya Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050 mara baada ya uzinduzi uliofanyika katika ukumbi wa Mikutano wa Jakaya Kikwete (JKCC) Jijini Dodoma Julai, 17, 2025.
Tanzania imepitia hatua tatu muhimu za kimkakati katika kupanga mustakabali wa maendeleo ya Taifa. Dira ya kwanza ilikuwa ni ile ya kupigania uhuru wa kisiasa, iliyojikita katika misingi ya haki za binadamu. Baada ya uhuru mwaka 1961, ilionekana kuwa si kila Mtanzania alielewa wajibu wa kuijenga nchi huru, na ndipo kampeni ya "Uhuru ni Kazi" ilipoanzishwa ili kuhimiza uzalendo na uwajibikaji kwa maendeleo ya wote.
Dira ya pili ilikuwa Azimio la Arusha la mwaka 1967, lililojikita katika falsafa ya Ujamaa na Kujitegemea. Azimio hilo liliweka msingi wa ukombozi wa kiuchumi na kijamii, na kwa muda mrefu likaongoza sera, mipango na taasisi za maendeleo, likihamasisha usawa, umiliki wa rasilimali na huduma za kijamii kwa wote.
Dira ya tatu ni Maendeleo ya Taifa 2025, iliyozinduliwa mwaka 1999, ambayo ililenga kuipeleka Tanzania katika hadhi ya nchi ya kipato cha kati ifikapo mwaka 2025.
Katika utekelezaji wake, mafanikio kadhaa yalipatikana. Kati ya mwaka 1999 na 2024, GDP ya Tanzania iliongezeka kutoka USD 12.7 bilioni hadi USD 78.78 bilioni, ikiwa na wastani wa ukuaji wa asilimia 6 kwa zaidi ya muongo mmoja (World Bank, 2024; Data Commons). Tanzania iliingia rasmi katika kundi la nchi za kipato cha kati cha chini mwaka 2020. Kwa upande wa maendeleo ya binadamu, HDI ilipanda kutoka 0.381 mwaka 2000 hadi 0.555 mwaka 2023, ingawa bado ni chini ya viwango vya mataifa ya kipato cha kati cha juu.
Kiwango cha umasikini kilishuka kutoka karibu asilimia 85 mwaka 2000 hadi asilimia 45 mwaka 2018 kwa kipato cha chini ya Dola 2.15 za Marekani kwa siku.
Maendeleo haya yaliambatana na upanuzi wa huduma za elimu ya msingi, afya vijijini, barabara, nishati na Tehama. Hata hivyo, changamoto zilikuwapo. Ila lengo la ukuaji wa GDP la asilimia 8 halikufikiwa hadi 2025, ukuaji ulikuwa asilimia 5.5. Aidha, deni la umma lilifikia asilimia 47.3 ya GDP mwaka huo, juu ya lengo la chini ya asilimia 35. Sekta ya viwanda haijachukua nafasi kuu kama ilivyotarajiwa na ubora wa elimu ya sekondari, huduma za maji, na usawa wa kijinsia bado vinahitaji maboresho zaidi. Katika msingi huo wa historia, mafanikio na upungufu, Tanzania sasa inaingia kwenye hatua ya nne kupitia Dira ya Maendeleo ya Taifa 2050.
Hii ni hatua ya kimkakati inayolenga kusukuma mbele maendeleo ya kijamii, kiuchumi na kimazingira, kwa msingi wa kujitegemea, ustawi, usawa na mshikamano wa kitaifa. Katika mazingira ya ushindani wa kikanda na mabadiliko ya haraka ya kiuchumi duniani, mpango huu unatoa fursa ya kipekee kwa Tanzania kupiga hatua kwa kasi na kwa mtazamo wa muda mrefu. Lakini, swali muhimu ni je, tumejifunza vya kutosha kutoka kwa Dira ya 2025? Na tunawezaje kujifunza kutoka kwa nchi jirani na zile zilizoendelea ambazo zimefanikiwa kupitia mikakati kama hii?
Mataifa mengi yaliyoendelea yamefikia maendeleo ya juu kwa kuwa na dira za muda mrefu zilizoendana na sera, bajeti na utekelezaji wa miradi ya kimkakati.
Mfano, Malaysia, kupitia Vision 2020, ilipanga kuwa taifa la kipato cha juu lenye viwanda na jamii ya maarifa. Ingawa ilishindwa kufikia kipato cha juu ilipofika 2020, mafanikio yake ni dhahiri.
Umasikini ulipungua hadi chini ya asilimia moja, huku Pato la Taifa kwa kila mtu likipanda kutoka dola 2,800 mwaka 1991 hadi zaidi ya dola 11,000 mwaka 2019. Kiwango cha Maendeleo ya Binadamu (HDI) kilifikia 0.810, kikiwa juu ya wastani wa dunia.
Katika Afrika, Rwanda ilijenga dira baada ya kipindi kigumu cha mauaji ya kimbari, kwa lengo la kuimarisha uchumi wa maarifa, usawa wa kijinsia, afya kwa wote, na utawala bora. Kati ya mwaka 2000 na 2017, umasikini ulipungua kutoka asilimia 58.9 hadi 38.2.
Zaidi ya asilimia 90 ya wananchi wana bima ya afya kupitia mpango wa Mutuelle de Santé. Rwanda imekuwa kinara wa matumizi ya teknolojia, ikiwa nchi ya kwanza Afrika kutumia drones kusambaza dawa vijijini na mifumo kama Irembo kupeleka huduma zote mtandaoni. Kenya ilizindua Vision 2030 mwaka 2008 ikiwa na lengo la kuwa taifa la kipato cha kati kinachotegemea viwanda, huduma bora na Tehama. Kulingana na World Bank (2020), Kenya ilishika nafasi ya 56 duniani kwa urahisi wa kufanya biashara, ikiwa mbele ya majirani zake wa Afrika Mashariki.
Kwa mantiki hiyo, Tanzania haiwezi tena kutegemea mikakati ya muda mfupi au kukabiliana na changamoto kwa mtazamo wa mwaka hadi mwaka.
Dira ya 2050 ni nafasi ya kujibu maswali makuu ni Tanzania ya aina gani tunaitaka mwaka 2050, na tunaanza vipi leo? Katika maandalizi ya Dira hii mpya, Serikali imejidhihirishia kuwa mfano wa dhamira ya kisera. Rais Samia Suluhu Hassan ameonyesha kuwa mipango ya maendeleo ya muda mrefu haiwezi kufanikiwa bila ushirikishwaji mpana wa wananchi, wataalamu, sekta binafsi na mashirika ya kiraia. Dira ya 2050 haikuwa tu kazi ya wataalamu, bali mchakato wa kitaifa ulioendeshwa kwa uwazi, mijadala ya wazi, na vikao vya kitaifa vilivyolenga kupata maoni kutoka pande zote za jamii. Uongozi huu umesaidia kujenga dira inayoendana na mahitaji halisi ya kizazi cha sasa na kijacho. Ni wazi kwamba, Tanzania imeandaa dira kwa mtazamo jumuishi na unaojali uendelevu wa kisiasa, kiuchumi na kijamii.