Rais Samia ataja mambo sita ya utekelezaji wa Dira 2050
Muktasari:
- Rais Samia Suluhu Hassan ametaja mambo sita yanayopaswa kuzingatiwa ili kutekeleza Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050 aliyoizindua jijini Dodoma.
Dar es Salaam. Rais wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan, ametaka kubadilishwa kwa mitazamo, namna ya kufanya kazi, na kuandaliwe nyenzo za kupima matokeo ya utendaji kazi serikalini kwa kuzingatia malengo na shabaha ya Dira ya Taifa ya Maendeleo ya 2050.
Amesema itakuwa vigumu kwa Tanzania kuyafikia malengo ya dira hiyo ya kufikia uchumi wa kati ngazi ya juu wa dola trilioni moja, iwapo watu wataendelea kufanya kazi kwa mazoea bila kupimwa.
Sambamba na hayo, ameeleza kuwa kipimo cha mafanikio ya dira hiyo ni utekelezaji wake, akisisitiza kuwa nchi ijielekeze katika vitendo zaidi kuliko maneno.
Rais Samia amesema hayo leo, Alhamisi, Julai 17, 2025, wakati akihutubia kwenye hafla ya uzinduzi wa Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050 iliyofanyika jijini Dodoma.
Ametaka kubadilishwa kwa mtazamo na namna ya kufanya kazi na kuandaliwa namna ya kupimana ili kufanikisha malengo ya dira hiyo.
Amesema haitawezekana kufikiwa lengo la dira hiyo kama kazi zitaendelea kufanywa kwa mazoea, hivyo lazima fikra, mtazamo, na matendo yabadilike na kuwepo na kupimana kwa matokeo ya kazi.
Ameitaka Tume ya Mipango na Ofisi ya Waziri Mkuu ziandae nyenzo zitakazotumika kupima matokeo ya utendaji serikalini kwa kuzingatia malengo na shabaha za dira husika.
Pia, ametaka kila wizara ipitie sera zake kuhakikisha zinashabihiana na maudhui ya dira na iwapo haziendani, zirekebishwe haraka kabla ya kuanza utekelezaji na sekretarieti pamoja na tume ya mipango iratibu hilo.
Ameitaka Tume ya Kurekebisha Sheria na Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali zianze mchakato wa kuchambua na kupendekeza maboresho ya kisheria, ili kuwezesha utekelezaji kamili wa dira husika.
Ametaka kuimarishwa kwa mfumo wa ufuatiliaji na tathmini, akitaka uwe wa kitaasisi na uweke wazi majukumu muda wote, utekelezaji, na njia ya kupima mafanikio kwa kila hatua.
“Uratibu wa utekelezaji uzingatie mshikamano wa ngazi zote za Serikali pamoja na ushirikiano wa karibu kati ya Serikali na sekta binafsi,” amesema.
Rais Samia amesema kila taasisi ya Serikali italazimika kuwa na vigezo vya kupima utendaji vinavyoendana na malengo na shabaha za dira, na hilo lazima liendeshwe kwa uwazi na taarifa zipatikane kwa umma.
Ameitaka sekta binafsi ijipange kutekeleza malengo na shabaha za dira, huku akisisitiza kuwa utekelezaji wa dira hiyo unahitaji ushiriki wa dhati na kimkakati wa sekta hiyo katika maeneo yote ya kiuchumi, ikiwemo uwekezaji, ubunifu, na uundaji wa ajira zenye staha.
“Serikali imejipanga kuweka mazingira ya kuiinua sekta binafsi ya ndani, na shukrani zangu ni kwamba imekuwa kiasi kwamba inataka kufanya makubwa zaidi.
“Sasa kama tuko tayari, tujipange, twende tukafanye kwa pamoja. Ahadi yetu kwenu ni kuyazingatia yale yote mliyotuletea kuhakikisha tunafanya kazi pamoja nanyi,” amesema.
Ametaka elimu kwa umma, mawasiliano, na uhamasishaji wa dira ili wananchi waelewe nafasi ya michango yao kuelekea 2050.
Kuhusu haki na ulinzi wa maadili, amesema ni maeneo muhimu kwa ustawi wa nchi na kwamba Mahakama na taasisi nyingine za utoaji haki zitambue nafasi yao katika kufanikisha malengo ya dira na kutimiza wajibu wao bila upendeleo, ghuba, wala chuki au uonevu kwa yeyote.
Ametoa rai kwa taasisi za kijamii, zikiwemo za kidini ambazo ni muhimili wa kujenga jamii yenye maadili, zisimame kidete kuhakikisha zinaijenga maadili.
Rais Samia amesema, kwa ukubwa wa rasilimali za nchi, haina sababu ya kutojiwekea lengo kubwa kwa kesho na ustawi wa Taifa.
“Tumeweza kutekeleza mengi, tutaweza kutekeleza dira hii. Kwa hiyo, Watanzania tujipe moyo na tuwe tayari, na wote tuwe tayari kuchangia ili dira hii itekelezeke vizuri,” amesema.
Katika hotuba hiyo, Rais Samia amesema nchi ijielekeze katika vitendo zaidi kuliko maneno, akirejea msemo wa ‘lisilo budi hutendwa.’
“Sasa tuna tabia ya kusema sana kuliko kutenda, na mtu wa sekta binafsi alilitupa kwetu serikalini, lakini hii ni tabia ya Watanzania sote. Kwa hiyo, sasa sekta binafsi, Serikali, wananchi tutende zaidi kuliko kusema,” amesema.
Rais Samia amesema Tanzania haikutimiza yote iliyojipangia kwa asilimia 100 kutokana na mapungufu ya usimamizi katika sheria, kuthiriwa na sera za kiuchumi na dunia, utegemezi wa kifedha, kiufundi na kiteknolojia, majanga, na mabadiliko ya tabianchi.
Kutokana na uzoefu uliopatikana katika utekelezaji wa mipango ya maendeleo kwa muda mrefu, amesema wamejipanga kutekeleza dira hiyo kwa umakini zaidi.
Amesema wataweka umuhimu katika kupanga na kusimamia mipango ya maendeleo itakayotafsiri dira husika na kuendelea kujenga uwezo wa kifedha, kitaaluma, na kiutendaji pamoja na uwezo wa kukabiliana na misukosuko ya kikanda.
Rais Samia Suluhu Hassan na viongozi wengine wakionesha nakala za vitabu vya Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050 mara baada ya uzinduzi uliofanyika katika ukumbi wa Mikutano wa Jakaya Kikwete (JKCC) Jijini Dodoma Julai, 17, 2025.
Amesema misaada na mikopo ikitumika vizuri inaweza kuchangia maendeleo ya nchi, lakini haiwezi kuwa msingi wa maendeleo endelevu kwa sababu wakati mwingine inaambatana na masharti magumu yanayoathiri uhuru wa kujiamulia.
Kipaumbele, amesema, ni kulinda na kutumia rasilimali, kuzilinda na kujenga uchumi na ustawi wa wananchi ikiwa ni msingi wa kuelekea kujitegemea.
“Tunajua ni safari ndefu na ngumu, lakini kwa uwezo wa Mungu tutafika,” amesema.
Amesema maudhui ya dira husika yametokana na matakwa ya Watanzania. Kwa sababu hiyo, hata utekelezaji utafanywa na Watanzania wenyewe kwa kushirikiana na wale washirika.