Haki na jukumu la mkopaji kisheria
Muktasari:
Mkopaji katika benki au taasisi za fedha ana haki ya kuingia kwenye mkataba wa mkopo, kuusoma huo mkataba na kuuelewa kabla ya kutia saini.
Imekuwa ni kawaida sana kwa watu wengi kujikuta wameingia kwenye mkopo bila kujua majukumu au haki zao kama wakopaji na matokeo yake wanafilisiwa au wanashindwa kabisa kurudisha mkopo.
Mkopaji katika benki au taasisi za fedha ana haki ya kuingia kwenye mkataba wa mkopo, kuusoma huo mkataba na kuuelewa kabla ya kutia saini.
Mkopaji ana haki ya kumtafuta mdhamini anayemtaka wa mkopo wake, lakini mkopaji anapaswa kuwa makini na kuepuka wadhamini wanaotaka asilimia 10 ya mkopo maana ukitoa hizo fedha tayari ni hasara na kulipa ni ngumu sana. Tofauti ni kwamba, mdhamini ni yule anayeweza kukusaidia wakati upo katika hali mbaya ya marejesho.
Mkopaji ana haki ya kurudishiwa mali yake aliyoweka kama dhamana (Right to redemption). Makubaliano yanayochukua hii haki hayana uhalali kisheria. Kwa mfano ukaandika kuwa ukishindwa kulipa ardhi ni yangu, hicho kipengele kitakuwa hakina nguvu kisheria na ni batili. Hii haki ipo kisheria katika kipindi chote cha mkopo, lakini pia haki hii ipo kama endapo muda wa kulipa marejesho umefika lakini mtu bado anashindwa kulipwa ipo kama msaada (Equity right of redemption).
Haki hii inaweza kukoma endapo, mtu kwa hiyari yake mwenyewe ameamua kumpa mkopeshaji. Hii lazima isemwe kwenye mkataba lakini itatekelezwa baada ya mkopo kutolewa na mwenye uamuzi ni mwenye mali. Miaka 12 imepita tangu mkopeshaji ameingia kwenye eneo na wewe haujafanya lolote kwa mujibu wa Sheria ya Ukomo Sura ya 89 kama ilivyorejewa 2002, hautaweza kudai ardhi yako.
Mtu anaweza kukosa hii haki endapo mkopeshaji ataendesha haki yake ya kuuza eneo husika baada ya mkopaji kushindwa kulipa.
Kisheria mkopaji anawajibu wa kutimiza majukumu yake baada ya kukopa. Majukumu hayo ni kuheshimu mkataba.
Mkopaji anapaswa kuheshimu mkataba wa mkopo, mfano kutouza au kuharibu dhamana ya mkopo kwa makusudi. Kwa muda wote wa mkopo, mkopaji anapaswa kuheshimu mkataba huo.
Kupeleka marejesho kwa wakati. Msingi wa mkataba wa mkopo ni marejesho ya mkopo husika na mara nyingi huwa inakuwa ni kwa mwezi. Haya yameelezwa kwenye kitabu cha Mkufunzi Abdon Rwegasira “Land as Human Right” Ukurasa wa 193 cha Mwaka 2012.
Jukumu la kulipia kodi na tozo nyingine kwenye eneo ambalo ni dhamana ya mkopo inategemeana na aina ya mkopo. Siyo kila mkopo una jukumu hili kisheria.
Kama mkataba wa mkopo unahitaji kuwekea bima au mali yoyote, itakubidi kama mkopaji kufanya hivyo kwa wakati na kwa mujibu wa mkataba wenu.
Tena inapaswa kwenye shirika mlilokubaliana au kama hamjakubaliana basi kwenye shirika lolote la bima linalotambulika kisheria.
Kutoa taarifa za kweli wakati wa kukopa, mkopaji anapaswa kutoa taarifa za kweli wakati wa kukopa, kitendo cha kughushi nakala mbalimbali au kutoa taarifa za uongo zinaweza kusababisha mkataba wa mkopo kusitishwa au hata kuweza kushitakiwa kwa jinai au kwa madai.
Jukumu la kukopa kwenye taasisi yenye uwezo kisheria, hili ni kwa faida ya mkopaji mwenyewe. Unapaswa kuangalia mtu au taasisi inayoweza kukopesha.
Mikopo kwa watu wa mitaani au kampuni ambazo hazijasajiliwa kisheria na ambazo hazina nguvu za kisheria kufanya hivyo, huwa ni batili na mkopeshwaji atashindwa kudai vizuri makato yake, na hataweza kutoza riba kwa sababu hajasajiliwa kama mtoa mikopo.
Mwandishi ni Wakili wa Kujitegemea kutoka Kampuni ya Uwakili ya Law Guards Advocates, Dar es salaam