HOJA YA MWAKA: Uchaguzi wa wabunge wa Finland na mafunzo kwa watanzania
Muktasari:
.Baada ya makala hii nitawaletea tena makala nyingine kuhusu uchaguzi mkuu wa Uingereza ambao ulifanyika Mei 7, 2015. Hivyo basi ninaomba ndugu msomaji wangu tufuatane ili tujifunze kutoka kwa wengine ili uchaguzi wetu mwaka huu uwe bora zaidi kuliko zilizotangulia.
Ndugu wasomaji wangu leo nimeona niendelee na mfululizo wa kuwandaa wananchi na Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 25 kwa kujifunza yanayotokea kwenye chaguzi za nchi nyingine duniani. Wiki mbili zilizopita niliandika tena kwa mara ya pili kuhusu uchaguzi wa Nigeria na kilichotokea katika ngazi mbalimbali za uchaguzi huo.Baada ya makala hii nitawaletea tena makala nyingine kuhusu uchaguzi mkuu wa Uingereza ambao ulifanyika Mei 7, 2015. Hivyo basi ninaomba ndugu msomaji wangu tufuatane ili tujifunze kutoka kwa wengine ili uchaguzi wetu mwaka huu uwe bora zaidi kuliko zilizotangulia.
Uchaguzi wa wabunge nchini Finland haufanyiki pamoja na uchaguzi wa rais kwani uchaguzi wa kiongozi wa nchi ulifanyika mara ya mwisho tarehe 5 Februari 2012 na kumuweka madarakani Tarja Halonen, ambaye alimaliza muda wake wa vipindi viwili vya urais wake na kumpisha Sauli Niinistö kutocha chama cha National Coalition Party. Alipata kura 1,802,328 ambazo ni asilimia 62.6 na uchaguzi ujao wa Rais sasa utafanyika mwaka 2018.
Nchini Finland pia kuna uchaguzi wa madiwani unaofanyika kwenye Manispaa zote haufanyiki sambamba na ule wa rais wala wa bunge, ingawa hufanyika mwaka mmoja. Hivyo uchaguzi huu wa madiwani kwenye manispaa zote ulifanyika mara ya mwisho tarehe 28 Oktoba 2012, Kwa sasa chama kipya tawala cha Finland’s Centre Party kina madiwani 3,077 kati ya jumla ya madiwani 9,614, wakati National Coalition kilichokuwa kinaoongoza serikali ya muungano kina madiwani 1,735 na chama cha Social Democrats kilichokuwa kimeshikilia urais kwa miaka 30 kina madiwani 1,729.
1.0. MATOKEO NA UCHAMBUZI
Uchaguzi wa ubunge ambao tunaweza kuuita kama ni uchaguzi mkuu ulifanyika Aprili 19, 2015 na chama cha upinzani kikiongozwa na Juha Sipilä wa Centre Party kiliibuka na ushindi wa kura 626,218 sawa na viti vya ubunge 49 sawa na asilimia 21.1 kati ya viti 200 vya ubunge. Katika nchi zinazoendesha demokrasia ya kibunge ni kwamba chama chenye wabunge wengi ndicho aidha kinaunda serikali peke yake au kinatafuta washirika wa mrengo wake kuunda serikali mpya. Chama cha pilikwa ushindi ni Finns ambacho kilinyakua kura 524,054 sawa na viti vya ubunge 38 ambavyo ni sawa na 17.7% na chama cha tatu kilikuwa Centre-Right National Coalition kilichonyakua kura 540,212 ambazo ni sawa na viti 37 vya ubunge, sawa na 18.5%.
Social Democratic Party ilichukua nafasi ya nne kwa kupigiwa kura 490,102 sawa na viti 34 vya ubunge ambayo ni sawa na asilimia 16.4. Chama cha tano ni Green Legue kilichopata kura 253,102 ambazo ni sawa na viti 15 vya ubunge (asilimia 8.5), chama cha sita ni Left Alliance ambacho kiliata kura 211,702 (viti 12, asilimia 7.1) na chama cha saba ni Swedish People’s Party ambacho kilichukua kura 144,802 (viti 9, asilimia 4.9) wakati Christian Democrats kilipata kura 105,134 ambazo zimezaa viti vya ubunge 5 sawa na 3.5%.
Katika nchi nyingi za barani Ulaya ambako demokrasia ya kibunge imeshamiri, ni mara chache sana kwa chama kimoja peke yake kuunda serikali kwani wapiga kura wameelimika vya kutosha kiasi kwamba hawawezi kuachia chama kimoja kuunda serikali kwa kuogopa chama kuweza kutumia vibaya wingi ilionao bila hofu na kujadiliana na mtu mwinine yoyote. Hivyo nchi nyingi hasa za Ulaya Magharibi vyama zaidi ya kimoja lazima vishirikiane kuunda serikali kwa manufaa ya wananchi wake.
Serikali mpya itakayoongozwa na Juha Sipila ambaye ni mfanyabiashara tajiri anayehusika na masuala ya mawasiliano anayeongoza Finland Centre Party, itachukua wiki kadhaa kuundwa na itahitaji vyama vingine viwili au vitatu ili kuweza kuunda serikali yenye wingi wa kutosha bungeni. Kwa kawaida nchini Finland chama kinachoshika nafasi ya pili kwa viti kinapewa nafasi ya Waziri wa Fedha, ingawaje kiongozi wa chama cha Finns, Timo Soini amesema anataka wizara ya mambo ya nje. Pamoja na kushika nafasi ya pili chama hicho kimepoteza kiti kimoja kwani mwaka 2011 kilipata viti 39 wakati National Coalition Party kimepoteza sana kutoka viti 44 sawa na 20.4% mwaka 2011 hadi viti 37 sawa na 18.5%.
Muungano ulioongozwa na National Coalition Party na kuvishirikisha vyama vingine kama Social Democratic Party, Swedish People’s Party na Christian Democrats ulishinda uchaguzi mwaka 2011 na kuwa sehemu ya muungano wa chama tawala na kumchagua Jyrki Katainen kuwa Waziri Mkuu ambaye alipata kura 118 dhidi ya 72 zilizomkataa. Baadhi ya vyama kama vile Left Alliance viliondoka kwenye muungano mwaka 2014 kwa sababu mbalimbali na kuuacha muungano huo ukipngua idadi ya wabunge kutoka 126 hadi 112.
Mwezi Aprili, 2014 Jyrki Katainen alitangaza kutogombea tena nafasi ya uenyekiti wa National Coalition Party (NCP) na badala yake alichaguliwa Alexander Stubb mwezi Juni 2014 na akawa Waziri Mkuu mpya. Mwezi Septemba 2014 chama cha kijani yaani The Green League kilitangaza kujitoa kwenye baraza la mawaziri kwa sababu za kisiasa na kuuacha muungano huo kubaki na wabunge 102 pamoja na Spika ambaye kwa kawaida hapigi kura. Kutokana na hali hiyo muungano huo ukawa dhaifu hadi wakati wa kuingia kwenye uchaguzi wa wabunge.
2.0. MAFUNZO KWA TANZANIA
Funzo la kwanza na kubwa kwa Tanzania ni kwamba Watanzania tusikubali kuacha wingi wa kutisha wa viti vya ubunge au udiwani kwa chama kimoja kwani tuna uzoefu wa chama chenye viti vingi kutumia wingi wake vibaya kupitisha maamuzi ambayo wakati mwingine hayana tija ya moja kwa moja kwa wananchi. Ukigawa viti kwa vyama kadhaa zaidi ya chama kimoja kunasaidia kuwa na mjadala na tafakuri ya kina juu ya maamuzi yanayochukulia ili yawe na manufaa kwa wananchi wanaowatumikia. CCM ina zaidi ya asilimia 75 ya wabunge wote na hivyo inaweza kufanya chochote ikiwemo kubadilisha katiba inavyotaka bila kuzuiwa na chama chochote kilichopo bungeni, jambo ambalo ni hatari sana kwa demokrasia ya vyama vingi. Ni ushauri wa kitaalamu kwamba chama chochote kisipewe zaidi ya nusu ya viti vyote ili kiwe na adabu na kulazimika kushirikiana na kujadiliana na vyama vingine kila wakati kunapotokea muswada au suala lolote bungeni.
Funzo la pili kutokana na uchaguzi wa Finland ni kwamba siyo lazima chama kilichopewa urais, kipewe pia uwingi wa nafasi katika bunge la kutunga sheria na siyo lazima kirundikiwe madiwani kwenye halmashauri kama ilivyokuwa kwa Finland kabla ya uchaguzi wa Jumapili kwani rais wa sasa anatoka chama National Coalition, wakati madiwani wengi wanatoka Finland’s Centre Party wakati huo huo wabunge wengi walitoka chama cha National Coalition. Baada ya ya uchaguzi wa Jumapili Rais anatoka chama cha National Coalition, wabunge na madiwani walio wengi wanatoka chama cha Finland’s Centre Party.
3.0. HITIMISHO
Toka nimeanza kuandika kwenye kolamu hii mwaka jana nimeandika sana kuhusu chaguzi za nchi mbalimbali ambazo nyingine nimeenda binafsi kushuhudia au hata kwa kusoma yaliyotokea katika nchi kama Afrika Kusini, India, Zambia, Malawi, Msumbiji, Scotland, Zimbabwe, Nigeria na sasa Finland. Kila ninapoandika habari za chaguzi za nchi nyingine nilikuwa siandiki tu kuwafurahisha wasomaji wangu lakini nimekuwa pia lazima niandike mafunzo kwa nchi yetu ya Tanzania ili tuweze kujifunza na kuboresha Uchaguzi Mkuu wetu wa mwaka 2015.
Ni matumaini yangu kuwa uchaguzi wa wabunge wa nchi ya Finland na nyingine za nyuma zitakuwa zimetupa mafunzo mengi sana na kutuwezesha tukijitazama sisi ndani ya nchi yetu na ni mambo gani tuige na mambo gani tuache. Kuna mambo ambayo serikali yetu inatakiwa kuchukua na kuyafanyia kazi lakini kuna mambo ambayo mwananchi na mpiga kura mmoja mmoja anaweza akayachukua na kuyafanyia kazi yeye mwenyewe na yote haya yataleta mabadiliko makubwa na chanya kwenye mifumo na matokeo ya uchaguzi mkuu huu wa mwaka 2015 ambao ni muhimu sana kuliko wakati mwingine wowote katika historia ya nchi yetu. Amka Amka ewe mwananchi kajiandikishe na ukapige kura yako ambayo ni haki yako.
*Mwandishi wa makala hii ni mchambuzi wa kisiasa na kijamii na msomaji wa gazeti la Mwananchi pia ni mwanafunzi wa shahada ya uzamivu (PhD) katika sayansi ya siasa na anapatikana kwenye simu namba 0713 612681 na baruapepe: [email protected]